Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUTAMBUA NGUVU YA MUNGU



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Kila siku
Ijumaa, Oktoba 9, 2026,
Juma la 27 la Mwaka

Gal 3:7-14
Zab 111:1-6 (K) 5
Lk 11: 15-26


KUTAMBUA NGUVU YA MUNGU


Yesu alikataliwa na kulaaniwa na baadhi ya watu. Lakini kuna kila sababu na vithibitisho kwamba Yeye ndiye ajaye. Wakati Yesu alipo samehe dhambi za yule mtu aliyepooza viongozi wa Wayahudi walimlaani Yesu kwa kukufuru Mungu, na baada ya yule mwanamke mdhambi kumpangusa Yesu kwa nywele zake na kumpaka mafuta Mafarisayo walimlaumuYesu kwanini anamruhusu amguse. Wakati Yesu alivyo mtoa pepo yule mtu aliye kuwa amepagawa na pepo watu walionesha mioyo migumu.

Leo katika somo la Injili Yesu anasema “kama ni kwa kidole cha Mungu natoa pepo, mjue kwamba ufalme wa Mungu umeshakuja kati yenu”. Yesu anasema hivi kujulisha watu kwamba Masiha ameshakuja kati yao.

• Ufalme na nyumba-Yeye ni Ufalme mwingine na tofauti na nyumba ya muovu.
• Mtoa Pepo-alihitahi kuheshiwa angalao basi kama viongozi wengine.
• Kidole cha Mungu-Yeye ana nguvu zote.
• Mtu mwenye nguvu. Yeye ana nguvu kuliko shetani.
• Nyumba iliyo tupu-alipenda kila mtu asafishe nyumba yake ili yeye aje akae na kujaza neema.

Je, tunajibuje katika alama ya Mkono wa ukomozi wa Mungu katika maisha yetu na katika maisha ya wengine? Kazi ya ukombozi ya Mungu inahitaji ushirikiano kutoka kwetu. Je, tupo tayari kumgeukia Bwana na kuamini?

Sala: Baba, tufundishe kutambua nguvu yako na kazi yako katika ulimwengu huu na kukugeukia kwa Imani. Yesu, nakuamini wewe.


Copyright ©2013-2026 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

MASOMO YA MISA, OKTOBA 9, 2026




MASOMO YA MISA, OKTOBA 9, 2026
IJUMAA, JUMA LA 27 LA MWAKA WA KANISA


SOMO LA 1 
Gal 3:7-14

Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani.  Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.  Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.

Neno la Bwana………….Tumshukuru Mungu


WIMBO WA KATIKATI 
Zab 111:1-6

(K) Alikumbuka agano lake milele.

Aleluya Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano. 
Matendo ya Bwana ni makuu, 
Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo. 

Kazi yake ni heshima na adhama, 
Na haki yake yakaa milele. 
Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu; 
Bwana ni mwenye fadhili na rehema. 

Amewapa wamchao chakula; 
Atalikumbuka agano lake milele. 
Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake, 
Kwa kuwapa urithi wa mataifa.

Aleluya, aleluya,
Nena, Bwana, kwakuwa mtumishi wako anasikia:
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.


INJILI
Lk.11:15-26

Wengine wa makutano walisema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia. Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli. Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake.

Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu aliyekusanya pamoja nami hutawanya.

Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitarudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

KUOMBA!




“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Kila siku
Alhamisi, Oktoba 8, 2026, 
Juma la 27 la Mwaka wa Kanisa

Gal 3: 1-5; 
Lk 1: 69-75; 
Lk 11: 5-13


KUOMBA!

“Ombeni nanyi mtapewa…” nimeomba mara nyingi, lakini sikupata hata kimoja. Haya ni majibu yetu kila mara kwenye huo ujumbe katika Injili. Lakini tujiulize, tunatulia nakujitafiti na kutafakari; je, nimeomba kwa ajili ya malengo sahihi? Je, ninafahamu thamani ya vitu ninavyo omba? Je, vitu ninavyo omba na kuhitaji nivya lazima kabisa? Mtoto asiye na meno anaweza kumuomba baba yake mua. Je, baba yake atampa? Hapana. Baba atasubiri mpaka akue awe na meno ndio ampe. 

Nyani hafahamu thamani ya dhahabu ulioshika. Lakini aweza kunyosha mkono kuomba, je utampatia? Hapana, haumpi. Kwasababu unafahamu thamani yake! Ni katika hali hiyo tunaweza tusijue tunanyoosha mkono kuomba nini, lakini Mungu anajua. Hii haimanishi tusiombe chochote tunacho penda. Tunaweza kuomba lakini kama hatuvipati tunavyo omba, tusikatishwe tamaa. Mungu anajibu katika hali ambayo itakunufaisha na njia ambayo itakufanya ulicho omba kisikutenge naye. 

Sala: Bwana, naomba mapenzi yako yatendeke. Amina

Copyright ©2013-2026 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, OKTOBA 8, 2026




MASOMO YA MISA, OKTOBA 8, 2026
ALHAMISI, JUMA LA 27 LA MWAKA

SOMO 1
Gal. 3:1 – 5

Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na Imani? Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili? Mmepatikana na mateso makubwa namna hii bure? Ikiwa ni bure kweli. Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na Imani?

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WAKATIKATI
Lk. 1:69 – 75 (K) 68

(K) Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajia watu wake.

Ametusimamishia pembe ya wokovu
Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake.
Kama alivyosema tangu mwanzo 
Kinywa cha manabii wake watakatifu. (K)

Tuokolewe na adui zetu
Na mikononi mwao wote wanaotuchukia;
Ili kuwatendea rehema baba zetu,
Na kulikumbu agano lake takatifu. (K)

Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yeu, 
Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu,
Na kumwabudu pasipo hofu,
Kwa utakatifu na kwa haki
Mbele zake siku zetu zote. (K)


SHANGILIO
1Per. 1:25

Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.


INJILI
Lk. 11:5-13

Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu, kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake; na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe? Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.

Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nayi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au samaki, badala y asamaki atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?

Neno la Bwana… sifa kwako Ee Kristo.

Copyright © 2026, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

NAMNA YA KUSALI




“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatano, Oktoba 7, 2026
Juma la 27 la Mwaka wa Kanisa

Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Rozari

Gal 2: 1-2, 7-14; 
Zab 116: 1-2; 
Lk 11: 1-4


NAMNA YA KUSALI

Maana rahisi ya sala twaweza sema, ni kuongea na Mungu. Biblia inatupa mfano wa Yesu anamkaa mapema na kupanda mlimani kusali. Katika sala tunaleta nini? Tunaweza kuleta chochote kinacho tusumbua wakati wa sala zetu, matatizo ya familia, matatizo ya mahusiano, matatizo ya afya au mambo ya kiroho. Katika Injili ya leo Yesu anawafundisha wafuasi wake kusali kwa ajili ya kuanzishwa kwa Ufalme wa Mungu, ambao ni kupenda na kutumikia mbele ya Mungu. Ana waambia wafuasi wa sali kwa ajili ya mkate wetu wa kila siku ambao unatupatia nguvu za kimwili na kwa wakati huo, “mkate wa uzima”- Ekaristi Takatifu ambayo ni kwa ajili ya uzima wa roho zetu. Na zaidi ya hayo anawaambia wasali kwa ajili ya msamaha, uponyaji wa hali yetu iliovunjika. Ni njia ipi sahihi ya kusali? Abudu kwa ukimya na ongea na Mungu mbele ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Wamonaki, Watawa husali na kuimba zaburi. Watu husali rosari wakati flani kabla ya kulala, wengine wakati akitembea mwenyewe njiani, Wakaresmatiki husali kwa sauti hata kunena kwa lugha. Kila mtu ana namna yake ya kuwasiliana na Mungu. La muhimu zaidi ni kuwasiliana na Mungu kweli bila kujibakiza. 

Sala: Bwana Yesu, tufundishe kusali kama ulivyo wafundisha wafuasi wako na utusaidie tuwe waaminifu na wanyovu kama watoto na kujiamini katika sala zetu. Amina.

Copyright ©2013-2026 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, OKTOBA 7, 2026




MASOMO YA MISA, OKTOBA 7, 2026
JUMATANO, JUMA LA 27 LA MWAKA WA KANISA0

Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Rozari

SOMO 1
Gal. 2:1-2, 7-14

Baada ya miaka kumi na mine, nalipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja nami. Nami nalikwenda kwa kuwa nalifunuliwa, nikawaeleza injili ile niihubiriyo katika Mataifa, lakini kwa faragha kwa hao walio wenye sifa, isiwe labda napiga mbio bure, au nalipiga mbio bure. Bali, kinyume cha nayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa. Maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa mataifa. Tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohane, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara; ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya.
Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu. Kwa maana kabla hawajaja watu kadha wa kadha waliotoka kw Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini walipokuja wao, akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa. Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao. Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha mataifa kufuata desturi za Wayahudi?

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 117 (K) 16:15

(K) Enendeni ulimwenguni wote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
Aleluya.

Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
Enyi watu wote, mhimidini. (K)

Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)


SHANGILIO
Yak. 1:18

Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.


INJILI
Lk. 11:1 – 4

Yesu alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, Msalipo, semeni: Baba, Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, Utupe siku kwa siku riziki yetu. Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

KUMWELEKEA YESU!



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne, Oktoba 6, 2026 
Juma la 27 la Mwaka


Gal 1:13-24; 
Zab 139: 1-3, 13-15;
Lk 10: 38-42.


KUMWELEKEA YESU!

Wakati Yesu alivyo watembelea Martha na Maria, Martha alikuwa akijishughulisha jikoni na pale Maria anakaa karibu na miguu ya Yesu huku akimsikiliza akiongea. Martha anamuomba Yesu amwambie Maria amsaidie. Yesu anamwambia Martha ana hofu na mambo mengi, wakati Maria amechagua njia sahihi zaidi. Tunaweza kushangaa kwani Martha hakuwa anafanya jambo lilo sahihi ambalo angepaswa kufanya? 

Katika maisha yetu ya kila siku pia, mara nyingi tunafanya kazi tena na tena na wakati mwingine tunasahau kwanini kumekuwa na muda maalumu wa kazi. Watu wa ndoa wake kwa waume, wanapoteza muda mwingi katika kazi, na kuwa na muda kidogo tena sana wakuwa pamoja wao kwa wao na pia kuwa na watoto wao. Mapadre na wale wa maisha ya wakfu, hujikuta wanakuwa na muda mwingi wa kufanya utume na kazi nyingi na hata kuwa na muda mchache wakuwa pamoja na kwasababu ya kuchoka huenda kuacha kusali. Na hii huaribu maisha ya jumuiya kwa sababu muda wa kupanga mambo pamoja hukosekana. 

Katika Injili Maria anachukua nafasi sahihi kwa kuchagua kubaki na Yesu. Na hapa tunaona matokeo ya uchaguzi wa mtu binafsi. Uchaguzi wa mtu unampa uzima wa milele au kifo na uharibifu. Kila mmoja wetu anaitwa kufanya uchaguzi sahihi kwa maisha yake. Mfanye Mungu rafiki yako na utafurahia urafiki wake milele.

Sala: Ee Bwana nichague wewe uliye njia sahihi. Amina



Copyright ©2013-2026 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

MASOMO YA MISA JUMANNE, OKTOBA 6, 2026



MASOMO YA MISA 
JUMANNE, OKTOBA 6, 2026
JUMA LA 27 LA MWAKA

SOMO 1
Gal. 1:13 – 24

Mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili  niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu; wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski. Kisha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana. Na hayo ninayowaandikia, angalieni, mbele za Mungu, sisemi uongo. Baadaye nalikwenda pande za Shamu na Kilikia. Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri Imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 139:1 – 3, 13 – 14 (K) 24

(K) Uniongoze, Ee Bwana, katika njia ya milele.

Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu zazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote. (K)

Niende wapi nijiepushe na roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko;
Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. (K)

Ningezitwaa mbawa za asubuhi,
Na kukaa pande za mwisho za bahari;
Huko nako mkono wako utaniongoza,
Na mkono wako wa kuume utanishika. (K)

Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. (K)


SHANGILIO
Yn. 14:5

Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: 
mimi ndimi njia, 
na ukweli, na uzima; 
mtu haji kwa Baba, 
ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.


INJILI
Lk. 10:38-42

Yesu aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie.
Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

“KATIKA JIONI YA MAISHA YAKO UTACHUNGUZWA TU JUU YA UPENDO”



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Jumatatu, Oktoba 5, 2026 
Juma la 27 la Mwaka


Gal 1: 6-12 
Zab 111: 1-2, 7-10 
Lk 10: 27-37


“KATIKA JIONI YA MAISHA YAKO UTACHUNGUZWA TU JUU YA UPENDO” (Mt. Yohane wa Msalaba)

Leo katika Injili mwalimu wa sheria anamuuliza Yesu swali ambalo, sisi tungeweza kujiuliza katika maisha yetu ya kila siku. “Bwana, nifanye nini niurithi Ufalme wa milele?” (Lk 10: 25). Yesu, lakini, tena katika hekima anajibu kwa yale yalioandikwa katika Maandiko: ‘kumpenda Bwana Mungu wako na jirani yako kama nafsi yako’ (rej. Lk 10: 27). Kupenda maana yake ni kujitoa kwa wengine kwa yote tulio nayo na yote jinsi tulivyo. Kujitoa kusikiliza wengine kujitoa kuelewa wengine na kuwa na subira kwa ajili ya wengine. Huo ndio upendo. Upendo huu unakuwa na asili ya Kimungu tunapo ueneza zaidi kwa wale walio tuumiza katika maisha au kwa wengine tusio waona hata macho kwa macho. Upendo unakuwa na Mguso wa Kimungu tunapo toka njee kwenda kuwasaidia hata watu tusio wafahamu. ‘Kama mtu mmoja anateseka, watu wote wanateseka naye, kama mmoja anaheshimiwa, watu wote wanashiriki katika furaha yake’ (1 Cor 12: 26). Hii ndio fadhila ya Msamaria Mwema. 

Sala: Bwana naomba nisitoe kisingizio chochote kwenye amri ya “Mpende jirani yako kama nafsi yako”. Amina.


Copyright ©2013-2026 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

MASOMO YA MISA, OKTOBA 5, 2026



MASOMO YA MISA, OKTOBA 5, 2026
JUMATATU, JUMA LA 27 LA MWAKA WA KANISA


SOMO 1
Gal. 1:6 – 12

Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe. Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo. Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu. Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 111:1 – 2, 7 – 10 (K) 10

(K) Alikumbuka agano lake milele.

Aleluya.
Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
Matendo ya Bwana ni makuu,
Ukawafunulia watoto wachanga. (K)

Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu,
Maagizo yake yote ni amini.
Yamethibitika milele na milele,
Yamefanywa katika kweli na adili. (K)

Amewapelekea watu wake ukombozi,
Ameamuru agano lake liwe la milele.
Jina lake ni takatifu la kuogopwa.
Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima,
Wote wafanyao hayo wana akili njema,
Sifa zake zakaa milele. (K)


SHANGILIO
2Kor. 5:19

Aleluya, aleluya,
Mungu alikuwa ndani ya Kristo,
 akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, 
ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya.


INJILI
Lk. 10:25-37

Mwana-sheria mmoja alisimama akamjaribu Yesu, akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zote; na jirani yako kama nafsi yako. Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi.

Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipitia kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapitia kando.

Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na lipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na chochote utakachogharimiwa Zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.

Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake, yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.