ASALI MUBASHARA-Jumanne 19/11/2019*

*ASALI MUBASHARA-Jumanne 19/11/2019*

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza Bwana anatupatia habari za kifo dini cha Mzee Eleazari. Huyu alikuwa mzee maarufu, mwenye heshima zake kwa Uyahudi wote. 

Lakini kwa siku ya leo Mfalme Antiokus anaamua kumwaibisha hadharani, anamweleza aende kinyume na desturi zake takatifu, afanye kitu kilicho kinyume na desturi za dini yake. Naye anakataa kwani anajua kwamba haishi ili awe kibaraka wa wafalme wa dunia bali yeye maisha yake yanapaswa yamtumikie Bwana. Hivyo anakataa kuwa kibaraka wa Mfalme, kwa kukataa kuvunja desturi za dini yake. 

Kishawishi kinachompata Eleazari kinafanana na kishawishi alichokipewa Yesu na shetani kwamba amsujudie na hapo atamkabidhi yote. Yesu alikishinda kishawishi hiki kwa kuonesha kwamba hapaswi kuwa kibaraka wa shetani au wa falme za kidunia. Eleazari alitambua kwamba ikiwa atakuwa kibaraka wa mfalme wa kipagani, hakika ataacha mfano mbaya kwa kizazi kijacho. Hakuna atakayeheshimu dini ya Kiyahudi na pia vijana wengi wangeiga mfano wake mbaya na kuangusha tamaduni za Kiyahudi na hakika kwa kosa lake, angeiachia dunia mfano mbaya. Aliamua kuvumilia mateso na mateso yale yaliiokoa maisha yake na kuisaidia dini ya Kiyahudi iendelee kustahimili vyema mapigo toka kwa watesi wao. 

Sisi tuige mfano wa mzee Eleazari. Tujue kwamba maisha yetu yanapaswa kuwa mfano. Tusisite kuwa shahidi kwa ajili ya Kristo. Tendo moja la kisadaka lenye kuitetea imani yetu litaikuza imani yetu kwa kiasi kikubwa sana. Maadili ya dini yetu yanapuuzwa sehemu nyingi kwa sababu sisi wenyewe hatujali na hatupo tayari kujitolea sadaka kwa ajili ya Kristo. 

Pia baadhi yetu ni watu wa njaa, tunathamini fedha kuliko maadili ya dini yetu. Rushwa yaweza ikaonekana kwamba inanifaidisha mimi lakini kwa kiasi kikubwa inaimomonyoa jamii ya kesho na kuifanya ipotee zaidi. 

Kwenye somo la injili, Zakeyo anakuwa tayari kupanda juu ya mti ili apate kumwona Yesu. Na alipopanda juu ya mti, Yesu aliweza kumwona na kumtambua mara moja na huu ukawa mwanzo wake wa kubadilika. 

Tujichunguze na sisi pia. Labda tupo kama Zakayo. Kazi tunazofanya na mazingira tunayokaa yanatuzuia kukutana na Yesu. Lazima tufanye kama Zakayo, tupande juu na hapo tutaweza kuonana na Yesu vyema. Hivyo tuchunguze mazingira yetu, wakati mwingine ndiyo kikwazo kinachotuzuia tushindwe kuonana na Yesu. 

Pia maneno yetu, ndiyo kikwazo kinachotuzuia tushindwe kuonana na Yesu. Pia baadhi ya marafiki-yaweza wakawa ndio kikwazo kinachonifanya nishindwe kukutana na Yesu. Panda juu ya mti kama Zakeyo na hivyo uonane na Yesu. Waache kukuzuia. 


KUWA WAZALISHAJI KWA AJILI YA UFALME WA MUNGU!

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatano, Novemba 20, 2019. 
Juma la 33 la Mwaka2 Mak 7: 1, 20-31;
Zab 17: 1, 5-6, 8, 15 (K) 15;
Lk 19: 11-28.KUWA WAZALISHAJI KWA AJILI YA UFALME WA MUNGU! 

Katika Mfano wa Injili, wakati Mfalme alivyorudi alihitaji hesabu ya kila mmoja. Sehemu hii inamalizia kwa kusema “kila mmoja aliye na vingi ataongezewa, na asiyenacho hata kile kidogo kitachukuliwa. Lakini kwa hao maadui wangu ambao hawakupenda mimi niwe mfalme wao, walete hapa na kuwangamiza mbele yangu”. Yesu yupo mkali kweli kwa hao wanaoenda kinyume na mapenzi ya Mungu. 

Watumishi watatu walikuwa wamepewa talanta. Mmoja alitumia vizuri akapata zaidi, wa pili alitumia akapata zaidi, lakini watatu hakufanya kitu. Ni huyu mtumishi ambaye hakufanya kitu ndiye anaye lengwa. Tumekuwa tukiongea mara nyingi kuhusu huruma na ukarimu wa Yesu na tupo sawa kuongea hivyo. Yeye ni mwenye huruma na mkarimu kupita yote. Lakini pia ni Mungu wa haki kweli. Katika mfano huu tuna makundi mawili ya watu wanaopokea haki ya Kimungu.

Kwanza kabisa tuna wale Wakristo ambao wanashindwa kuhubiri Injili na kushindwa kutumia kile walichopewa. Wanakaa tu kimya na Imani yao, na mwishowe wanaishia kupoteza hata Imani kidogo walio nayo. Pili, kuna wale ambao wanapinga Ufalme wa Yesu na ujengaji wa utawala wake hapa duniani. Hawa ni wale wanahusika katika kujenga utawala wa shetani katika hali mbali mbali. Matokeo ya maovu yao ni maangamizi yao wenyewe. 
Katika somo la kwanza tunaona uaminifu wa mama na watoto wake licha ya kutishiwa kuuwawa kwasababu ya kutokula nyama haramu iliowekwa kwa miungu ya mfalme. Walisimama imara katika sheria ya Mungu. Uaminifu huu unahitajika kwa Imani yetu. Tafakari leo juu ya umuhimu wa Injili na kumfuata kwako Yesu. Kama kuna kitu kinapungua, omba neema ya kupewa ujasiri na kuwa shuhuda wa Yesu na ufalme wake. 

Sala: Bwana, ninaomba nisichezee neema ulizonipa wewe. Nisaidie daima nizitumie daima kueneza ufalme wako. Nisaidie niweze kuona furaha na neema kwa kufanya hivyo. Yesu, nakuamini wewe. Amina


Copyright ©2013-2019 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

MASOMO YA MISA NOVEMBA 20, 2019

MASOMO YA MISA NOVEMBA 20, 2019
JUMATANO, JUMA LA 33 LA MWAKA


SOMO 1
2 Mak. 7:1,20-31

Ilitokea ya kuwa ndugu saba, pamoja na mama yao, walikamatwa kwa amri ya mfalme na kuteswa sana kwa mijeledi na mapigo ili kuwashurutisha kuonja nyama marufuku ya nguruwe.
Aliyekuwa wa ajabu hasa, na kustahili kumbukumbu la heshima, ndiye yule mama. Maana aliwaona wanawe saba wakifa kwa siku moja, akistahimili kwa moyo thabiti kwa ajili ya matumaini aliyoyaweka kwa Bwana. Kwa roho hodari aliimarisha tabia yake ya kike kwa ushupavu wa kiume, akamfariji kila mtoto kwa lugha ya wazee wao, akisema, Jinsi mlivyoingia tumboni mwangu sijui. Si mimi niliyekupeni roho na uzima, wala si mimi niliyeziunga sehemu za miili yenu. Bali ni yeye, Muumba ulimwengu; yeye aumbaye wanadamu na kukikusudia chanzo cha vitu vyote; naye kwa rehema zake akakurudishieni roho zenu na uzima wenu, kwa kuwa ninyi sasa mnajihesabu kuwa si kitu kwa ajili ya amri zake.
Antioko alijiona anafedheheshwa, lakini bila kuangalia mzaha wa maneno yake, alimsihi yule mdogo, maana alikuwa  yungali hai, akamwambia, si kwa maneno tu ila pia kw auapa, ya kuwa, akama ataziacha sheria za wazee wake, atampatia mali nyingi na hali njema; tena, atamfanya mmoja wa rafiki zake na kumkabidhi kazi za ufalme. Yule kijana asipokubali, alimwita mama yake, akamtaka amshawishi mtoto ajiokoe. Akasema naye kwa maneno mengi, hata mwisho alikubali kumshauri mwanawe.
Akamwinamia na huku anamdhihaki yule mfalme mkali akasema hivi kwa lugha ya wazee wake: Mwanangu, unirehemu mimi niliyekuchukua tumboni mwangu kwa miezi tisa, na kukutunza na kukulea mpka sasa. Nakusihi, mwanangu, inua macho yako utazame mbingu na nchi, ukaone vitu vyote vilivyomo; fahamu kwamba Mungu hakuviumba kwa vitu vilivyokuwapo. Na ndivyo alivyofanya wanadamu pia. Usiogope mwuaji huyu; jionyeshe umestahilika sawasawa na dnugu zako. Kubali kufa kwako, ili kwa rehema ya Mungu nikupokee tena pamoja na ndugu zako. Hakudiriki kuyamaliza maneno yake, ila yule kijana alisema, Mnamngoja nini? Mimi siitii amri ya mfalme, bali naitii amri ya sheria waliyopewa baba zetu kwa Musa. Wewe, uliyebuni kila namna ya uovu juu ya Waebrania, hutaokoka kabisa katika mikono ya Mungu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 17:1,5-6,8,15 (K) 15

(K)  Nishibishe kwa sura yako, Ee Bwana.

Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiotoka katika midomo ya hila. (K)

Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako,
Hatua zangu hazikuondoshwa.
Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitikia,
Utege sikio lako ulisikie neno langu. (K)

Unilinde kama mboni ya jicho,
Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako.
Nikutazame uso wako katika haki,
Niamkapo nishibishwe kwa sura yako. (K)


SHANGILIO
Yn. 10:27

Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.

INJILI
Lk. 19:11 – 28 
Makutano waliposikia, Yesu aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara. Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi. Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja. Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.
Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake. Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi. Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi. Akaja wa pili, akasema, Bwana fungu lako limeleta mafungu matano faida. Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano. 
Akaja mwingine akasema, Bwana hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso, Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda. Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi. Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi, Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho.
Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwanchinje mbele yangu.
Na laipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.Copyright © 2019, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

*MASOMO YA MISA, JUMANNE NOVEMBER 19, 2019*

*MASOMO YA MISA, JUMANNE NOVEMBER 19, 2019*
*JUMANNE JUMA LA 33 LA MWAKA C⛪*

*SOMO 1*
2Mak 6:18-31

Eliazari, mmoja wa waandishi wakuu, mkuu wa umri mkubwa na sura njema, alishurutishwa kufunua kinywa chake kulishwa nyama ya nguruwe. Lakini akaitema ile nyama, akasogea mwenyewe kwenye mahali pa kuteswa, akiona afadhali kufa kwa heshima kuliko kwa unajisi. Akatenda kama yampasavyo mtu aliyekaza nia yake kuvikataa vitu visivyo halali kuonjwa hata kwa kutaka kujiokoa maisha. Basi, wale waliosimamia dhabihu hiyo haramu, kwa kuwa wamejuana naye kwa miaka mingi walimchukua kando wakamsihi alete nyama yake mwenyewe, iliyo halali ya kuliwa, na kufanya kana kwamba anaila nyama ya dhabihu, kama mfalme alivyoamuru. Hivyo atajiponya na mauti, na kutendewa nao kwa hisani kwa sababu ya urafiki wao wa tangu zamani. Lakini yeye aliikaza nia yake madhubuti, nia iliyostahili umri wake na jadi yake, na mvi zake stahivu, na mwendo wake wa adili tangu utoto wake katika kuzishika amri takatifu zilizotolewa na Mungu. Akakataa kabisa, na kuwaambia wampeleke kuzimuni upesi akisema haipatani na miaka yetu kudanganya, isije vijana wengi wadhani ya kuwa Eliazari, katika mwaka wake wa tisini, ameicha dini yake kwa dini ya kigeni; na hivyo, kwa sababu ya udanganyifu wangu, watapotoshwa na mimi mwenyewe nitajipatia unajisi na aibu katika uzee wangu. Na hata nikiepukana na adhabu ya wanadamu sasa, lakini sitaweza kuepukana na mikono ya Mwenyezi, nikiwa hai au nimekufa. Basi, nikitoa maisha yangu sasa kwa ushujaa, nitajionyesha kuwa nimestahili miaka yangu mingi, na kuwaachia vijana mfano wa kufa mauti ya fahari kwa hiari na kwa uthabiti, kwa ajili ya amri takatifu zenye heshima. Alipokwisha kusema hayo, alipaendea mara mahali pa kuteswa. Nao waliokuwa wakimwonyesha urafiki walibadili nia zako kwa wabaya kwa sababu ya maneno yake waliyoyaona ya kiwazimu. Naye alipokuwa kufani kwa ajili ya mapigo yake, aliugua akasema, kwake Bwana ajuaye yote ni dhaniri ya kuwa, ingawa ningaliweza kuepukana na mauti, lakini ninavumilia maumivu makali mwlini mwangu; hata rohoni mwangu ninayavumilia kwa furaha kwa sababu ya kicho changu kwake. Hivyo alikufa; na kwa kufa kwake aliacha mfano wa unyofu na ukumbusho wa wema, si kwa vijana tu, ila kwa jamii yote ya taifa lake.

*Neno la Bwana.....Tumshukuru Mungu*

*Wimbo wa katikati*
Zab 3:1-6

*(K) Bwana ananitegemeza*

Bwana, watesi wangu wamezidi kuwa wengi, 
Ni wengi wanaonishambulia,
Ni wengi wanaoiambia nafsi yangu, 
Hana wokovu huyu kwa Mungu.
*(K)*

Na Wewe, Bwana, U ngao yangu pande zote, 
Utukufu wangu na mwinua kichwa changu.
Kwa sauti yangu namwita Bwana 
Naye aniitikia toka mlima wake mtakatifu.
*(K)*

Nalijilaza nikalala usingizi, nikaamka, 
Kwa kuwa Bwana ananitegemeza.
Sitayaogopa makumi elfu ya watu, 
Waliojipanga juu yangu pande zote.
*(K)*

*INJILI*
Lk 19:1-10

Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake. Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

*Neno la Bwana.....Sifa kwako ee kristo*

FURAHA YA UPENDO WA YESU

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne, Novemba 19, 2019, 
Juma la 33 la Mwaka wa Kanisa

2 Mac 6:18-31
Zab 3:2-7
Lk 19:1-10


FURAHA YA UPENDO WA YESU

Ni kitu ghani kilichomfanya Zakayo akafungua moyo wake, katika Injili ya leo? Ni furaha ya upendo wa Yesu. Watu walimchukia Zakayo sana na kadiri walivyo mchukia ndivyo alivyo jitenga mbali nao. Yesu anaingia katika nyumba ya Zakayo na tazama mtu aliyekuwa na moyo mgumu, unayeyuka nakuanza kuahidi maisha ya fadhila ya baadae. Je, ni kitu ghani utafanya Yesu akija kugonga katika moyo wako leo nakusema “nataka kukaa katika nyumba yako leo?” je utafurahi au utakuwa na mashaka na kudhani utadhalilika? Bwana yupo tayari daima kufanya maskani yake ndani mwetu. Je, unampa nafasi katika moyo wako na nyumbani mwako? 

Sala: Jaza nyumbani mwangu kwa uwepo wako Ee Bwana, nisaidie niweze kuonesha ukarimu na huruma kwa wote, hata kwa wale walioniumiza. Amina


Copyright ©2013-2019 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

*ASALI MUBASHARA-Jumatatu 18/11/2019*

No.2 (Namna nyingine yakutafakari masomo ya leo)

*ASALI MUBASHARA-Jumatatu 18/11/2019*

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. –Neno la Bwana katika somo la kwanza, tunasikia habari za Mfalme Antiokus na kuingia kwa upagani katika Israeli ambapo Yuda analazimishwa kuziacha tamaduni zake zilizomfikisha hapo alipo na kukumbatia tamaduni nyingine za kigeni. 

Siku ya leo anatokea Mfalme Antiokus analazimisha kwamba watu waache kumwabudu Bwana Mungu wa Israeli, waache tamaduni zao, na vitabu vya sheria, yaani Biblia takatifu ichanwe halafu zifuatwe tamaduni za taifa jingine. Kwa Israeli, kama inavyooneshwa katika Kumbukumbu la Torati 6:4, tamaduni zao na sheria zilikuwa takatifu na waliambiwa kwamba ndio zitakazowalinda kama taifa. Hivyo walielezwa kwamba wasizitupe, bali wawafundishe na vizazi vijavyo. 

Sasa leo Antiokus anawaeleza kwamba wasizifuate. Na mbaya zaidi wapo baadhi ya Wayahudi waliotaka kuzitupa tamaduni zao. Lakini wengi kati ya Israeli watanyanyuka na kupambana na uonevu huu. 

Somo hili litoe kwetu pia hamasa kuzitetea tamaduni zetu kama wakristo. Siku hizi tumevamiwa na kundi la utamaduni wa ukisasa unaoona kama tamaduni zetu kama kanisa zimekwishapitwa na wakati. Hivyo wanataka nyingine zijitokeze juu yao. Sisi tuwe  tayari kupambana na uonevu wa namna hii. Hatuwezi kuutupa utamaduni wetu pembeni kwani huu ndio uliotufikisha hapa tulipo.

Pia hatupaswi kutupa baadhi ya tamaduni na desturi zetu za makabila ya asili kwani nazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kutufikisha hapa tulipo. Ukweli ni kwamba vipo baadhi ya vitu ndani ya tamaduni za makabila yetu ya asili vinavyopaswa kuboreshwa lakini hatupaswi kutupa desturi na tamaduni zetu zote. Mara nyingi waliolelewa kufuatana na mila na desturi za kabila lao wanakuwa wafanisi, wenye heshima kwa wazee, hofu ya Mungu na sio wabinafsi kwani tamaduni za makabila mengi hupinga ubinafsi. Waliokosa malezi toka kwa makabila yao mara nyingi huwa wabinafsi. Hivyo tujifunze kuheshimu tamaduni zetu. 

Katika somo la injili, kipofu wa Yeriko anapata uponyaji. Kipofu huyu kwa hakika alianza kwa kunyamazishwa na waliokuwa pembeni lakini yeye akagundua kwamba wao sio watu wema. Hivyo aliamua kujitosa mwenyewe na kumwita Yesu. Na kwa hakika alitumia muda ule vizuri kwani hii ilikuwa ni mara ya mwisho ya Yesu kuja Yeriko. Hivyo alitumia muda huu kama "golden chance". 

Nasi tujifunze kutumia fursa zetu vizuri. Upo wakati ambao fursa nyingi zitajitokeza lakini haitakuwa hivyo kwa kipindi chote. Tujifunze kutumia chance vyema. Kila fursa inayojitokeza kwa hakika itumiwe, isitupwe pembeni.

ASALI MUBASHARA-Jumatatu 18/11/2019*

*ASALI MUBASHARA-Jumatatu 18/11/2019*

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika asubuhi ya leo linaongozwa na maneno ya mzaburi katika wimbo wa katikati-Ee Bwana unijalie uhai nami nitazitii kanuni zako. Maneno haya siku ya leo yanatuchimbulia chimbuko la somo letu la kwanza leo. 

Hapa tunakutana na simulizi ya mfalme aitwaye Antiochus Epiphanes aliyewaletea madhara makubwa sana Waisraeli; alitaka kuangamiza Imani na tamaduni za Kiisraeli na kufanya Mungu asiheshimiwe tena. Akaweka amri ati atakayekutwa amebeba kitabu cha maandiko matakatifu auawe. Akawaambia watu wageukie kwenye uabudu wa sanamu na kutolea uvumba masanamu na baadhi ya Wayahudi hasa wale vijana vijana walikubaliana na hili wakaona sawa wakasema tuachane na hivi visheria vyetu vya Kiyahudi, vinatubana sana, tunashindwa kuoana hata na watu wa mataifa, tunashindwa kula raha kama watu wa mataifa. Hivyo, walianza kukumbatia haya mambo ya kimataifa na kuiacha Imani yao.

Kitu hiki kiliwauzi baadhi ya Wayahudi na hivyo kulitokea kikundi cha Wamakabayo kilichopingana na huyu mfalme na wafuasi wake wote waliokuwa na lengo la kuiteketeza dini ya Kiyahudi (Judaism). Hivyo, wimbo wa katikati unaakisi dhamira ya hiki kikundi cha watu-unijalie uhai ee Bwana nami nitalisifu jina lako. 

Hii ndio nia ya hawa Wamakabayo ambao kitabu chao tutakisikia kwa siku kadhaa kadhaa. Hawa ni watetezi wa dini ya Kiyahudi. Wanasema unijalie uhai ee Bwana nami nitakuonesha jinsi nitakavyolifanya jina lako lisifiwe, sitaliacha lidhihakiwe na hawa watu.

Katika somo la injili, tunakutana na kipofu anayelia Bwana nionee huruma-nionee huruma Bwana nipate kuona. Huyu naye ukimchunguza utaona kwamba mawazo yake ni kwamba nijalie nipate kuona ee Bwana halafu nitakuonesha namna jinsi ninavyokupenda, nitawasimulia watu wote juu ya ukuu wako. Niponye tu na hapo utashuhudia mwenyewe.

Ndugu zangu, makundi yote mawili-Wamakabayo wa somo la kwanza na kipofu wa somo la injili walifanikiwa kwa kile walichoomba. Hawakushindwa ndugu yangu kutokana na kupania kwao kumtumikia Bwana.

Ndugu zangu, hapa nasi tunajifunza kitu. Sisi tunashida mbalimbali, twende kwa Bwana, mwambie ee Mungu niponye tu, nisaidie tu jamani, fanya kitu na watu wote watashuhudia-watashuhudia jinsi nitakavyokutangaza, yaani wekeza kwangu ee Bwana na nakwambia sitakuangusha, mwambie Bwana hivi ndugu yangu na nakwambia atakusikiliza tu.

Lakini siku zote uwe na lengo jema, sio kwa ajili ya kuwatesa wengine au kuwaonea wengine au utembee mbele uitwe bosi, bosi bosi au uitwe mkuu mkuu-lengo lisiwe hili. Lengo liwe ni kumfanya Mungu atukuzwe na si wewe uitwe mkuu, mkuuu, jembee, jembee!

Kingine ni kwamba huzunika popote uonapo jina la Mungu likidharaulika kama wale Wayahudi tuliosikia katika somo la kwanza. Yaani ilifikia mahali ikawa kushika hata yale maandiko yao matakatifu ikawa ni adhabu. Jina la Mungu wao likawa linadhihakiwa lakini baadhi hawakuvumilia hili. Nawe ndugu yangu usikubali jina la Mungu lidhihakiwe. Ukipita ukikutana hata na rozari imetupwa inakanyagwa kanyagwa huko iokote, ukiona picha ya Yesu inakanyagwa huko iokote, ukiona Biblia ipo kwenye sehemu chafu iokote na usafishe hilo eneo, ukiona vitambaa vya altare ni vichafu na vimeshachakaa tayari kazana vingine vinunuliwe. Jina la Bwana lisidhihakiwe hata kidogo. 

MWAMBIE BWANA EBU NIPATIE KAUHAI TU NA WATU WOTE WATAKUTAMBUA KUWA WEWE NI BWANA. NAWE BWANA KAKUPA UHAI-WATU WOTE WAMTAMBUE BASI KWAMBA YEYE NI BWANA.

FUNGUA MACHO YA MOYO WANGU, NINATAKA KUKUONA WEWE

“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatatu, Novemba 18, 2019.
Juma la 33 la Mwaka wa Kanisa

1 Mak 1: 10-15, 41-43, 54-57, 62-64; 
Zab 118: 53, 61,134, 150, 155, 158; 
Lk 18: 35-43.


FUNGUA MACHO YA MOYO WANGU, NINATAKA KUKUONA WEWE 

“…Wamefunga macho yao, hivyo macho yao hayaoni, wala mioyo yao haiwezi kuelewa, na hawawezi kunigeukia na kunifanya mimi niwaponye (Mt 13:15-16).” 

Yesu wakati anakaribia Jeriko, akiwa njiani kuelekea Yerusalemu. Anarudia tena kuhusu kifo chake, ambacho ni sehemu muhimu katika utume wake. Lakini Wafuasi walishindwa kumuelewa. Wafuasi wa Yesu wanawakilishwa na alama ya mtu kipofu. Ni mhitaji, kwani ni muombaji. Hayupo kwenye njia bali pembeni. Analia ‘Mwana wa Daudi’, umuhimu wa Petro kumuungama. 

Yesu, hamuiti huyu mtu mwenyewe bali anamuita kupitia kwa jumuiya iliyo mzunguka. Yesu hajifanyi kwamba anafahamu anachotaka huyu mtu, bali anamuuliza. Unataka nikufanyie nini? Huyu mtu ingawaje ni kipofu, anaweza kuona mambo ya zamani. Ilikuwa ni katika hali hiyo hiyo kama wafuasi. Waliona wakati Yesu alivyo waita, waliona wakati akiwa anawaponya watu, waliona wakati akiwalisha watu wengi. Lakini waliendelea kusahau, wakaendelea kuharibiwa na mambo,wakaendela kupoteza mwangaza wa mioyo yao. Kama walikuwa wanaelewa mafundisho yake, ingekuwa ni yeye anayewapa mwangaza. Yesu anamhakikishia yule kipofu kwamba ni Imani yake iliyo msaidia aweze kuona. Njia pekee ambayo mitume wangepaswa kuwa nayo ili waone. Ni Imani tu hakuna kitu kingine, inayowafanya mitume waweze kumfuata katika safari yake kwenda Yerusalemu, kwenda kwenye msalaba. 

Katika safari yetu ya maisha pia, sisi pia tumekutana na Yesu, kwa namna ya pekee katika sakramenti. Lakini baadae tumefunga macho na kumfuata Yesu nusu nusu. Tumekuwa watu wakushangaa njia badala ya kumfuata moja kwa moja. Kama kipofu, kukaa karibu, tunapaswa kulia kwa sauti kutoka katika magumu yetu. Yesu atasikia sauti yetu, kwani anatutaka sisi tutembee naye njiani, kwenye njia pekee inayo ongoza kwenye maisha ya kweli. 

Sala: Bwana, wewe ni mwanga wa ulimwengu. Ninataka kukufuata wewe uliye mwanga wakutupeleka kwenye uzima. Ninaomba ufungue tena macho yangu, ili niweze kukuona na kukufuata. Yesu nakuamini wewe. Amina.
Copyright ©2013-2019 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 18, 2019

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 18, 2019
JUMATATU, JUMA LA 33 LA MWAKA 

SOMO 1
1Mak. 1:10-15, 41-43, 54-57, 62-64

Kulichipuka chipukizi chenye dhambi, ndiye Antioko Epifani, mwana wa mfalme Antioko, ambaye alikuwa amewekwa amana kwa Warumi. Naye alitawalishwa katika mwaka wa mia thelathini na saba wa enzi ya Wayunani.
Siku zile walitokea wahalifu sheria katika Israeli, wakashawishi wengi, wakisema, Twende tufanye maagano na mataifa wanaotuzunguka, maana tangu tulipofarakana nao misiba mingi imetupata. Jambo hilo likapendeza machoni pao, hata watu Fulani wakafanya hima kwenda kwa mfalme, naye akawapa ruhusa kuzifuata kawaida za mataifa. Wakafanya kiwanja cha michezo Yerusalemu kama kawaida ya mataifa, wakajifanya kana kwamba hawakutahiriwa wakajitenga na agano takatifu. Hivyo walijiunga na mataifa na kujiuza wafanye uovu.
Mfalme Antioko akaziandikia milki zake zote, kwamba wote wawe taifa moja, kila mtu aache sheria zake za asili. Watu wote wa mataifa wakaikubali amri ya mfalme, hata wengi katika Israeli walifuata ibada yake, wakitoa dhabihu kwa miungu ya uongo na kutia unajisi Sabato.
Siku ya ishirini na tano ya Kislevu, mwaka wa mia arobaini na tano, waliweka chukizo la uharibifu juu ya madhabahu, na katika miji ya Uyahudi kila upande walijenga vimadhabahu vya miungu, wakavukiza uvumba milangoni pa nyumba na njiani. Na vitabu vya sheria walivyovipata waliviparua vipande vipande wakaviteketeza. Mtu yeyote aliyepatikana na kitabu, au aliyeonekana anaifuata sheria, alihukumiwa kufa kama alivyoamuru mfalme.
Hata hivyo wengi katika Israeli walikaza nia zao kwa uthabiti wasile vitu vilivyo najisi. Waliona afadhali kufa kuliko kutiwa unajisi kwa vyakula au kulivunja agano takatifu. Wakafa. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 119:53, 61, 134, 150, 155, 158 (K) 88

(K) Unihuishe kwa fadhili zako, nami nitazishika shuhuda za kinywa chako.

Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki,
Waiachao sheria yako.
Kamba za wasio haki zimenifunga,
Sikuisahau sheria yako. (K)

Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu,
Nipate kuyashika mausia yako.
Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki,
Wamekwenda mbali na sheria yako. (K)

Wokovu u mbali na wasio haki,
Kwa maana hawajifunzi amri zako.
Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa,
Kwa sababu hawakulitii neno lako. (K)

SHANGILIO
Zab. 147:12, 15

Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya.

INJILI
Lk. 18:35-43

Yesu alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka; na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini? Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita. Akapiga kelele, akisema, Yesu Mwana wa Daudi, unirehemu. Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee mwana wa Daudi, unirehemu.
Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona. Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya. Mara hiyo akapata kuona. Akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2019, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

*ASALI MUBASHARA-Jumamosi 16/11/2019*

*ASALI MUBASHARA-Jumamosi 16/11/2019*

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho takatifu la misa siku ya leo. Neno la Bwana katika zaburi ya wimbo wa katikati leo linatuasa juu ya kuyakumbuka maongozi ya Mungu, yote ambayo Mungu ametujalia maishani mwetu. Yafaa tuyakumbuke, tusisahau hata moja. Kuyasahau matendo makuu ya Mungu ni mwanzo wa maafa katika maisha ya taifa teule la Israeli.

Kusahau ni tendo la kukosa shukrani. Ni kuwa kama baadhi ya wanyama. Wapo wanyama wenye kuwadhuru hata wale wenye kuwatunza bila kutambua kwamba pale wanapowadhuru, watakaopata shida ni wao wenyewe. 

Katika somo la kwanza, Mwenyezi Mungu anawaeleza kwamba miongoni mwa matendo wanayopaswa kuyakumbuka ni lile tukio la wao kukombolewa nchini Misri, pale Mwenyezi Mungu alipowapendelea wanyonge na kuwaadhibu watesi waliowakandamiza. Walipaswa kuwaeleza hata watoto wao ukuu wa tukio hili kwani siku hiyo, kulikuwa na kilio kwa taifa la Misri lakini mbele yao kulikuwa na furaha. 

Nasi tusiache kuyakumbuka matendo makuu tuliyotendewa na Mungu. Pia tunapaswa kuyatolea ushuhuda mbele ya watu. Usiache kutangaza makuu uliyotendewa na Mungu. Ni ishara ya imani, ni ishara kwamba unamsadiki Mwenyezi Mungu na hapa ni kumpatia Mungu sifa na utukufu. Tusibane kueleza matendo makuu ya Mungu. Kila mmoja leo ayakumbuke makuu yote aliyowahi kutendewa na Mungu na kumtolea utukufu. 

Pale tunapokaa kimya, na kuelezea tu historia za matatizo ya maisha yetu, bila kutaja makuu ya Mungu na kulalamika jinsi tunavyoumwa, jinsi tunavyoumwa njaa-ikiwa tutayaelezea haya tu hakika hapa ni kumkosea Mweneyezi Mungu haki. Tuwe watu wa kushuhudia pia na mazuri tuyapatayo maishani mwetu. 

Katika somo la injili, Bwana Yesu anatufundisha kuhusu kusali. Kusali kwahitaji uvumilivu mkubwa, kwani mawazo yetu, nia zetu mara nyingi ni tofauti na Mungu. Mungu kwa baadhi ya nyakati hunia yaliyotofauti kwetu. Ipo namna Mungu anavyotaka maisha yetu yaende lakini sisi pia tunayomitazamo yetu ya jinsi tunavyopendelea maisha yetu yaende. Tunataka maisha yetu yafanane naya wenzetu waliofanikiwa lakini Mungu huweza kuwa na mawazo na nia na mtazamo tofauti juu yetu.

Hivyo, tujifunze kuzipokea na kuzitii nia za Mwenyezi Mungu na kuacha matendo yake yatimie ndani yetu. Tunaposali tuwe wavumilivu na wapole na pia tuyakubali mapenzi ya Baba.