Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUJAZWA NEEMA NA KUTANGAZA NENO LA MUNGU KWA MAPENDO



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Aprili 25, 2024 
------------------------------------------------
ALHAMISI, JUMA LA 4 LA PASAKA
SIKUKUU YA MT. MARKO, MWINJILI

Somo la 1: 1 Pet 5:5-14 Somo linaongelea kuhusu Marko, ambaye Patro alimchukua kama mtoto wake. 

Wimbo wa Katikati : Zab 89: 2-3, 6-7, 16-17 Maisha yote midomo yangu itatangaza ukweli wako. 

Injili: Mk 16: 15-20 Yesu anawambia wale kumi na mmoja waende ulimwenguni kote; wakahubiri kwa mataifa yote. 
------------------------------------------------

KUJAZWA NEEMA NA KUTANGAZA NENO LA MUNGU KWA MAPENDO 

Leo kanisa linasheherekea sikukuu ya Mt. Marko Mwinjili. Yohane Marko anatokea katika kitabu cha Matendo ya mitume (Mdo 12:12), na mara nyingi ametajwa katika katika barua za Petro na Paulo. Katika barua fupi ya filemoni Marko ananukuliwa kama rafiki wa karibu wa Paulo…’.. Marko Mwanangu”. Kuna mapokeo pia kwamba Marko alikuwa ni mwanzilishi wa kanisa la Alexandria, kaskazini mwa Misri. Mwandishi wa Injili ya Pili pia inasemekana pia ya Marko. Mapokeo yanasema pia wakristo wa Roma alimuomba Marko aandike maneno ya Petro. Na Injili inaoneakana kuandikwa kama utume wa Yesu kama alivyo uona Petro na hivyo Marko kuandika. Inasemekana ni Injili ya kwanza kuandikwa, na Mathayo na Luka inaonekana kupata kutoka kwake. Injili yake imejaa matendo ya Yesu, ambapo Yesu anafundisha zaidi yale anayotenda kuliko yale anayosema. 

Katika Injili ya leo Yesu anawapa mamlaka kutangaza Injili kwa kila kiumbe na kuna ahadi kwamba waamini watakuwa na uwezo wakutenda makuu-kutoa pepo, kunena kwa lugha, kukingwa na mabaya na kuponya wagonjwa. Na mwishoni somo linaonekana kuwa na maelezo kidogo kuhusu kupaa ambapo Bwana wetu alikuwa akirudi kwa baba yake, na kukaa mkono wa kuume wa Mungu. Marko anaelezea changamoto za wafuasi wa Kristo na katika kutimiza hali yao ya umisionari na kuanzisha Ufalme ambao mapenzi ya Mungu yatatendwa duniani. 

“Enendeni ulimwenguni mote mkahubiri Injili kwa kila kiumbe” (Mk 16:15). Amri iliyo ya kawaida kabisa. Na wimbo wa katikati unasema hivi “nitaimba daima sifa zako, ee Bwana, muda wote nitatangaza uaminifu wako…ni nani aliye kama Bwana.” Yesu aliwatuma wanafunzi wake ambao walikuwa watu wakawaida lakini wakiwa wamejaa nguvu ya ajabu ili kutangaza Injili yake na kuikomboa dunia. Cha muhimu haikuwa msingi wa wafuasi kuhubiri bali msingi wa kutegemea neema yake inayofanya kazi ndani yao na hivyo kwa namna tulivyo wawazi kwa neema ya Mungu, ndivyo neema yake inavyotiririka ndani yetu. Uwazi wetu kwa Mungu utasababisha matunda makubwa zaidi ya jinsi tusivyoweza kutegemea. 

Sala: Yesu, nisaidie mimi niweze kuwa wazi kwa neema yako. Tunakuomba utupe neema tuweze kumuiga Mt. Marko Mwinjili katika roho ya kutangaza Ufalme wako. Yesu, nakuamini wewe. Amina


Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment