Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, OKTOBA 9, 2024




MASOMO YA MISA, OKTOBA 9, 2024
JUMATANO, JUMA LA 27 LA MWAKA WA KANISA

SOMO 1
Gal. 2:1 – 2, 7 – 14

Baada ya miaka kumi na mine, nalipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja nami. Nami nalikwenda kwa kuwa nalifunuliwa, nikawaeleza injili ile niihubiriyo katika Mataifa, lakini kwa faragha kwa hao walio wenye sifa, isiwe labda napiga mbio bure, au nalipiga mbio bure. Bali, kinyume cha nayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa. Maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa mataifa. Tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohane, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara; ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya.
Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu. Kwa maana kabla hawajaja watu kadha wa kadha waliotoka kw Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini walipokuja wao, akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa. Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao. Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha mataifa kufuata desturi za Wayahudi?

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 117 (K) 16:15

(K) Enendeni ulimwenguni wote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
Aleluya.

Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
Enyi watu wote, mhimidini. (K)

Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)


SHANGILIO
Yak. 1:18

Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.


INJILI
Lk. 11:1 – 4

Yesu alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, Msalipo, semeni: Baba, Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, Utupe siku kwa siku riziki yetu. Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment