Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

WEKA ULIMWENGU KWENYE MOTO WA MAPENDO YA MUNGU



“MBEGU ZA UZIMA”
Tafakari ya Pasaka
Jumapili, Mei 19, 2024

Sherehe ya Pentekoste

Mdo 2: 1-11;
Zab, 104: 1, 24, 29-31, 34;
1 Kor 12:3-7, 12-13 au Rom 8:8-17 
Yn 20:19-23 au Yn 14:15-16, 23-26


WEKA ULIMWENGU KWENYE MOTO
WA MAPENDO YA MUNGU

‘Pentekoste’ ni neno la Kigiriki lenye maana ya “Hamsini”. Wakristo wanasherekea sherehe hii siku hamsini baada ya Pasaka (Mdo 2). Ikiwa ni tamaduni iliyotoka Agano la Kale, yenye maana ya “sikukuu ya mavuno” katika siku ya hamsini baada ya “Pasaka ya Wayahudi” (Kut. 23:16, Hes. 28:26-31, Kum. 16:19-21). Siku hii ilikuja kuwa muhimu kwa Wakristo kwasababu, majuma saba baada ya ufufuko wa Yesu, wakati wa sikukuu ya mavuno ya Wayahudi, Roho Mtakatifu aliwashukia wafuasi wa kwanza wa Yesu, akiwapa nguvu na uwezo wakumtangaza Kristo na kuwakusanya pamoja kama Kanisa. Kama Wayahudi walivyokuwa wakitoa matunda ya mazao yao ya kwanza, wakijiandaa kwa mvua kwa ajili ya mazao yajayo; wafuasi, mazao ya kwanza ya utume wa Kristo yaliyoiva, wanapokea mvua ya Roho Mtakatifu, Roho atakaye wafanya wakue na kuwa mazao na mbegu kwa ajili ya vizazi vijavyo. Katika Siku hii, umoja wa watu wa Mungu kama Kanisa, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu ulianza.

Roho Mtakatifu alitumwa kama Yesu alivyo ahidi, ili kukamilisha kilele cha ufunuo wa upendo wa Mungu. Roho Mtakatifu hajiweki kwa Wayahudi peke yao, bali anafunua upendo wa Mungu usio na mipaka kwa watu wote, akileta Baraka, matunda katika nchi ambayo ilikuwa imelaaniwa kipindi cha Adamu na Eva. Lugha iliyoleta mtafaruku nakutoelewana katika mnara wa Babeli, inakuwa kiunganisho kikuu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Ukosefu wa urafiki na umoja na Mungu uliopotea katika Edeni, Roho Mtakatifu anaurudisha tena kwa kuwa na Kanisa daima.

Pentekoste tunasheherekea kazi na uwepo wa Roho Mtakatifu ndani yetu kama waumini na Kanisa. Mungu amemimina juu yenu wote Roho Mtakatifu (Rom 8:1-11) na tunapaswa kuishi ndani ya uwepo wa nguvu ya Roho wa Mungu. Roho Mtakatifu anatusaidia kumkiri Yesu kwamba ni Bwana wetu (1 Kor 12:3), akituwezesha kumtumikia Mungu (1 Kor 12:4-11), akituunganisha pamoja kama Mwili wa Kristu (1 Kor 12:12-13), anatusaidia kusali (Rom 8:26), anatuombea ndani ya Mungu Baba (Rom 8:27). Roho Mtakatifu anatuongoza (Gal 5:25) na Roho Mtakatifu anatusaidia tuishi kama Yesu (Gal 5:22-23). 

Baba Mtakatifu Fransisko anamuita Roho Mtakatifu “Upendo” unaokosekana ndani ya familia zetu na Ulimwenguni. Katika ujumbe wake ndani ya “Amoris Laetitia”, “Furaha ya Upendo” anamuonesha Roho Mtakatifu kama mfano halisi wa Familia za Kikristo na Kanisa. 

“Upendo ndani ya familia ya Kimungu, ni Roho Mtakatifu….tunaweza kutambua upendo wa Mungu ndani ya Roho Mtakatifu….kwa njia ya Kanisa, ndoa na familia zinapokea neema za Roho Mtakatifu kutoka kwa Kristo, ili tuweze kutoa ushuhuda wa Injili ya Upendo wa Mungu.”

Baba Mtakatifu anazialika familia zote za Kikristo “kila wakati kualika usaidizi wa Roho Mtakatifu anayetakatifuza umoja wenu, ili neema zake ziweze kutawala katika kila jambo mnalokutana nalo”. Pia anasema, bila Roho Mtakatifu umoja wa familia za Kikristo hauwezekani. “hakuna hata moja kati ya haya, litakalo wezekana bila kusali kwa Roho Mtakatifu ili amimine neema zake, nguvu zake na moto wa Roho, kutufanya wake, kutuongoza na kubadili mapendo yetu kwa kila hali”

Leo tunaitwa, tuweze kujali kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu binafsi, familia, jumuiya na Kanisa zima. Je sisi ni vyombo vya kazi ya Roho Mtakatifu? Je, tumekuwa wasikivu wakati Roho Mtakatifu anapotuongoza? Matunda ya Roho Mtakatifu (Upendo, furaha, Amani nk.) yanakuwa ndani mwangu? Sisi wote tunaishi ndani ya uwepo wa nguvu ya Roho Mtakatifu lakini katika viwango tofauti. Tunazuiwa na uoga wetu, dhambi zetu, Mapungufu yetu na uharibifu wetu wa kila siku unaotufanya tushindwe kuhisi uwepo wa zawadi ya Mungu ya Upendo ‘Roho Mtakatifu’. Pentekoste inatupa tena wakati wa kuhisi moto wa Roho Mtakatifu na kuuweka Ulimwengu kwenye moto wa upendo wa Mungu.

Sala: Nivuvie nguvu ya Roho Mtakatifu Bwana, ili mawazo yangu yaweze kuwa matakatifu. Nivuvie pia nguvu ya Roho Mtakatifu ili kazi yangu iweze kuwa takatifu. Gusa moyo wangu Roho Mtakatifu, niweze kupenda vile vitakatifu tu. Nipe ujasiri Roho Mtakatifu ili niweze kulinda kila kilicho kitakatifu. Nilinde Roho Mtakatifu, ili niweze kuwa Mtakatifu daima. Roho Mtakatifu, nakuamini wewe. Amina.


Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, JUMAPILI, MEI 19, 2024


MASOMO YA MISA, JUMAPILI, MEI 19, 2024
SHEREHE YA PENTEKOSTE


SOMO 1 
Mdo. 2:1-11

Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.

Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelani, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATI KATI 
Zab. 104:1, 24, 29-31, 34, (K) 30

(K) Waipeleka roho yako, Ee Bwana, Nawe waufanya upya uso wa nchi. au: Aleluya.

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wewe, Bwana, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
Dunia imejaa mali zako. (K)

Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wa nchi. (K)

Utukufu wa Bwana na udumu milele;
Bwana na ayafurahie matendo yake.
Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
Mimi nitamfurahia Bwana. (K)


SOMO 2 
1 Kor. 12 :3-7, 12-13

Hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.

Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO

Aleluya, aleluya, Uje Roho Mtakatifu, uzienee nyoyo za waamini wako uwatie mapendo yako. Aleluya.


INJILI 
Yn. 20 :19-23

Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.

Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

KUMFAHAMU YESU!



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Jumamosi, Mei 18, 2024 
Juma la 7 la Pasaka


Mdo 28: 16-20, 30-31;
Zab 11: 4-5, 7 (R. 7);
Yn 21: 20-25


KUMFAHAMU YESU!

Jaribu kufikiria ni mitizamo aliokuwa nayo Mama Bikira Maria kuhusu Mwanae. Yeye kama Mama yake, atakuwa aliona mambo mengi na kuelewa nyakati nyingi za maisha yake ambazo nyingine hatuzifahamu. Yeye alikuwa akimtizama akikuwa mwaka baada ya mwaka. Alikuwa akimtizama akiongea na watu na kushirikiana na wengine. Atakuwa alitambau alikuwa akijiandaa kwa utume wake. Na atakuwa ameshuhudia nyakati nyingi za utume wake Mtakatifu na maisha yake yote ambayo hayaja andikwa katika Injili. 

Maneno ya mwisho ya Injili ya Yohane yanatupa hali Fulani ya kutafakari zaidi. Mambo yote tunayo fahamu kuhusu maisha ya Yesu, yanapatikana katika Injili, lakini inawezekanaje Injili hizi kuweza kuelezea maisha yote ya Yesu, kila kitu alichofanya? Ni hakika kwamba haziwezi. Kufanya hivyo kama Yohane alivyosema, “nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.”

Injili inatuonesha ni kwa jinsi ghani tunamfahamu Yesu kidogo sana. Inapaswa pia kufungua akili kwamba tunapaswa kumfahamu Yesu zaidi. Tunapaswa kutamani kumfahamu zaidi na zaidi. Na hii itatufunga tukazane kumtafuta Kristo zaidi na zaidi kwa ndani. Pia, ingawaje mambo mengine ya maisha ya Yesu hayaja andikwa, haina maana kwamba hatuwezi kumfahamu Yesu, tunaweza kumfahamu Yesu Mwenyewe kwa yale yote yaliyo katika maandiko Matakatifu. Hakika tutakutana naye. Tutakutana na Neno wa Mungu mwenyewe akiishi katika Maandiko na kukutana naye huku tunapewa yote tunayo hitaji. 

Tafakari leo, ni kwa jinsi ghani unamfahamu Yesu. Je, una muda wakusoma Maandiko Matakatifu na kuya tafakari? Je, unamtafuta kila siku na kutamani kumfahamu na kumpenda? Je, yeye yupo ndani yako na unajitahidi kujiweka mbele yake kila siku? Kama jibu ya moja wapo la maswali haya ni “HAPANA” basi hii ni siku nzuri ya kuanza tena kujituma katika kusoma maandiko Matakatifu, neno la Mungu. 

Sala: Bwana, ninaweza nisiwe nafahamu yote kuhusu maisha yako, lakini natamani kukufahamu. Ninatamani kukutana na wewe kila siku, kukupenda wewe na kukufahamu. Nisaidie nizame ndani zaidi katika uhusiano wangu na wewe. Yesu, nakuamini wewe. Amina


Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, MEI 18, 2024



MASOMO YA MISA, MEI 18, 2024
JUMAMOSI YA 7 YA PASAKA

SOMO 1
Mdo. 28 :16-20, 30-31

Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda.

Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane; hata walipokutanika akawaambia, Ndugu zangu, ingawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali nimefungwa, tokea Yerusalemu. Na hao walipokwisha kuniuliza-uliza walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na sababu yo yote kwangu ya kuuawa. Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nalishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nalikuwa na neno la kuwashitaki watu wa taifa langu. Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli.

Akakaa muda wa miaka miwlli mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribi sha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI 
Zab. 11 :4-5, 7 (K) 7

(K) Wanyofu wa moyo wauona uso wake, Ee Bwana. au: Aleluya.

Bwana yu katika hekalu lake takatifu.
Bwana ambaye kiti chake kiko mbinguni,
Macho yake yanaangalia;
Kope zake zinawajaribu wanadamu. (K)

Bwana humjaribu mwenye haki;
Bali nafsi yake humchukia asiye haki,
Na mwenye kupenda udhalimu. (K)

Kwa kuwa Bwana ndiye mwenye haki,
Apenda matendo ya haki,
Wanyofu wa moyo watamwona uso wake. (K)


SHANGILIO 
Mt. 28 :19-20

Aleluya, aleluya, 
Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi. Mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, Hata ukamilifu wa dahari. 
Aleluya.


INJILI 
Yn. 21:20-25

Petro aligeuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata; (ndiye huyo aliyeegama kifuani pake wakati wa kula chakula cha jioni, akasema, Bwana, ni nani akusalitiye?). Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je? Yesu akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi.

Basi neno hilo lilienea katikati ya ndugu ya kwamba mwanafunzi yule hafi. Walakini Yesu hakumwambia ya kwamba hafi; bali, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Huyu ndiye yule mwanafunzi ayashuhudiaye haya, na aliyeyaandika haya; nasi twajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli. Kuna na mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo. 


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

18th MAY 2024






 

JE, WANIPENDA



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Ijumaa, Mei 17, 2024 
Juma la 7 la Pasaka

Mdo 25: 13-21;
Zab  103: 1-2, 11-12, 19-20 (K. 19);
Yn 21: 15-19.


JE, WANIPENDA?


Katika lugha ya Kigiriki, kuna maneno tofauti yanayo tafsiriwa kama “Upendo”. Agape ni aina ya upendo uliyo kamilika, safi, usio na ubinafsi, upo hai. Agape maana yake, kujali na kuwapenda wote, na kujali bila kuweka nafsi mbele. Kuna upendo pia ambao ni hafifu (Phileo), kumpenda mtu kwasababu yakutaka kupendwa naye au kwasababu yakutaka kupata vitu au kitu fulani kutoka kwake. 

Yesu anamuuliza Petro kwa mara zote mbili za kwanza, “je, Simoni wa Yohane, wewe wanipenda (Agape) kuliko hawa?” anasema “ndiyo Bwana, wajua nakupenda (Phileo).” Ingewezekanaje Petro aseme moja kwa moja bila wasi wasi Bwana nakupenda (Agape) baada ya kushindwa kwake kumkiri Bwana? Yesu anamuuliza mara ya tatu, Simoni mwana wa Yohane, je wanipenda (Phileo) mimi?” (angalia hapo Yesu amebadili upendo hapo kutoka Agape na kwenda Phileo). Petro “anahuzunika” si kwasababu tu Bwana alimuuliza mara ya tatu, bali ameshusha kiwango cha upendo, kutaka kumuonesha Petro upendo wake upo wapi!. Tunaweza kufikiri ni jinsi gani Petro alivyo huzunika moyoni. Isingekuwa ni kwasababu ya woga na hofu iliomkumba Petro wakati wa mateso ya Yesu, pengine kabla angeweza kusema kwanguvu zote kabisa, Bwana unaniuliza swali ghani? Bila shaka nakupenda (Agape). Lakini matendo yake yalionesha wazi ni kwa jinsi ghani alishindwa agape kwa Bwana. Alikana hata urafiki (phileo) na Bwana. Na sasa ana “huzuni” ya kweli wanavyo onana uso kwa uso na Bwana kwa yale aliyotenda.


Hili lina maana ghani kati yangu na wewe? Ina maana kwamba hatujachelewa sana. Tunaweza kuwa tumemkosea Bwana kabla, lakini kwa huzuni ya kweli, tuna nafasi nyingine yakumdhihirishia Yesu na sisi wenyewe, kwamba sisi ni Wakristo wa namna ghani. Tumejikuta tukimkana Yesu kwa kugeukia dhambi, turudi sasa na kumpenda kikamilifu (Agape). 

Yesu anamuambia Petro pia alipokuwa kijana alipenda kwenda popote pale alipopenda, pengine hata sisi tujaribu kujiuliza, sisi tukiwa bado tuna nguvu zetu tunafanya nini? Tunatumia nguvu zetu kusali au tunasubiri mpaka tuwe wazee ndio tuanze kusali? Pengine unaweza kujipa kisingizio cha kazi, je unasubiri mpaka ustaafu ndio uanze kwenda kanisani? Tujiwekee hazina tukiwa bado tuna nguvu, ili uzee wetu uwe na Baraka. Tujipatanishe na Mungu daima tukiwa bado na nguvu zetu, tusimuache Mungu kamwe.

Sala: Bwana, unafahamu kwamba nakupenda. Nafahamu unafahamu ni kwa jinsi ghani nilivyo dhaifu. Ninaomba nisikilize wito wa mwaliko wako wa kuonesha mapendo yangu kwako na hamu ya kupata huruma yako. Ninaomba nitoe upendo huu na hamu hii ya kupata huruma katika hali ya juu kabisa. Yesu, nakuamini wewe. Amina

Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, MEI 17, 2024


MASOMO YA MISA, MEI 17, 2024
IJUMAA YA 7 YA PASAKA

SOMO 1 
Mdo. 25 :13-21

Siku zile, Agripa mfalme na Bernike walifika Kiaisaria, wakimwamkia Festo. Na walipokuwa wakikaa huko siku nyingi, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake.

Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe. Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama nilivyodhani, bali walikuwa na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba yu hai. Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya. Lakini Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI 
Zab. 103 :1-2, 11-12, 19-20 (K) 19

(K) Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni. au: Aleluya.

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu 
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote. (K)

Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. (K)

Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni,
Na ufalmc wake unavitawala vitu vyote.
Mhimidini Bwana, enyi malaika zake,
Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake,
Mkiisikiliza sauti ya neno lake. (K)



SHANGILIO 
Kol. 3 :1

Aleluya, aleluya, 
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. 
Aleluya.



INJILI 
Yn. 21 :15-19

Walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohane, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wanakondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili. Simoni na Yohane wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu.

Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohane, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.

Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka. Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo, akamwambia, Nifuate.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo. 


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

17th MAY 2024






 

KWA NINI YESU ANASALI?

John 17:9. Jesus Prays for You - Wellspring Christian Ministries


“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Alhamisi, Mei 16, 2024
Juma la 7 la Pasaka


Mdo 22: 30; 23: 6-11;
Zab 16: 1-2, 5-11 (K. 1);
Yn 17: 20-26


KWA NINI YESU ANASALI?


Leo tunamuona Yesu akituombea sisi tunao muamini. Ni bahati ilioje kuwa na Mungu anayetuombea? Ni furaha ilioje kuona tumepewa heshima kwa kutajwa ndani ya Injili na kuongelewa na Yesu? Yesu anawaombea wale watakao kuwa wafuasi wake baada ya kuwasikiliza mitume wake. Hapa sisi tupo kwani tunaamini waliotuachia mitume.

Wakati Yesu anavyo nyanyua macho yake mbinnguni, anasali kwa Baba yake wa mbinguni. Ukweli huu wa kunyanyua macho yake, unafunua jambo moja muhimu la uwepo wa Baba yake. Unafunua kwamba “Baba yupo juu ya yote”. Kwa hiyo kwa kuongea na Baba yake, Yesu anaonesha ishara hii kwa kumkiri kwamba Baba yupo juu ya yote. Tunapaswa pia kutambua uhusiano wa pekee na Yesu na Baba yake. Uhusiano wao ni uhsiano wa asili yote. 

Sala ya Yesu kwa Baba ilikuwa sisi wote ambao tutamwamini tuweze kushiriki umoja wa Baba na Mwana. Kwanza kwabisa tunaanza kwa kuona ukuu wa Mungu, kunyanyua macho yetu mbinguni na kuona ukweli, utukufu, ukuu, nguvu, na Mungu wa Majeshi. Tunapaswa kumuona Mungu huyu mtukufu na mkuu akishukia mioyo yetu, akiwasiliana na sisi, akitupenda sisi, akianzisha uhusiano wa karibu na sisi. Tunapaswa kukubali uwepo wake, kumwabundu akiwa anaisha ndani yetu, tukiongea naye na kumpenda yeye. 

Kitu cha kwanza anachoomba ni sisi tuwe na umoja (Yn 17: 21-23). Umoja wetu katika Mungu matokeo yake ni utume, kama Yesu anavyosema, “Ili ulimwengu utambue kuwa umenituma mimi” na tena “..ili ulimwengu uweze kutambua umenituma mimi na unawapenda wao kama unavyo nipenda mimi”. Zaidi na zaidi watu watakuwa na imani ndani ya Yesu, kwa uwepo wa Kanisa, na kudhihirisha kwa kutoa ushuhuda wa upendo wa Mungu ndani ya Kristo. 

Na tena Yesu anaendelea kusali “..na pia wao, ulionipa mimi, waweze kuwa nami pale nilipo, waweze kuona utukufu ulionipa, kwasababu ulinipenda mimi kabla ya kuwepo misingi ya ulimwengu.” Anaongelea maisha yetu yajayo katika maisha ya milele. Huko tutaona utukufu wake, usiofifia wala kuisha. Hapo tutakuwa naye, na tutamuona uso kwa uso.
Sala: Bwana, ninaomba unisaidie niweze kunyanyua macho yangu kuelekea mbinguni kwa sala. Ninakuomba nikugeukie wewe na Baba. Katika sala hiyo naomba nitambue kuwa upo wazi katika moyo wangu ambapo una abudiwa na kupendwa. Yesu, ninakuamini wewe. Amina.

Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, MEI 16, 2024


MASOMO YA MISA, MEI 16, 2024
ALHAMISI YA 7 YA PASAKA

SOMO 1 
Mdo. 22 : 30; 23 : 6-11

Wakati ule, Jemadari alitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani Paulo ameshitakiwa na Wayahudi, akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta Paulo chini, akamweka mbele yao.

Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu. Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana. Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; bali Mafarisayo hukiri yote. Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, w'akisema, Hatuoni uovu wo wote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema naye, ni nini? Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome.

Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imeku- pasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.
Hilo ndilo neno la Mungu.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI 
Zab. 16:1-2, 7-11 (K) 1

(K) Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia Wewe. au: Aleluya.

Mungu unihifadhi mimi,
kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu, 
sina wema ila utokao kwako. (K)

Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku. 
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yako kuumeni kwangu, sitaondoshwa. (K)

Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
Nao utukufu wangu unashangilia,
Naam, mwili wangu nao utakaa kw;a kutumaini. 
Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu,
Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. (K)

Utanijulisha njia ya uzima;
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume 
Mna mema ya milele. (K)



SHANGILIO 
Yn. 16:28

Aleluya, aleluya, 
Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena naucha ulimwengu, na kwenda kwa Baba. 
Aleluya.



INJILI
Yn. 17 :20-26

Siku ile, Yesu alisali akisema: Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. 

Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu. Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo. 


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.