“MBEGU ZA UZIMA”
Tafakari ya kila Jumapili
Jumapili, Januari 22, 2023
Juma la 3 la Mwaka A wa Kanisa
Is 8:23 – 9:3;
Zab 27: 1, 4, 13-14;
1Kor 1: 10-13, 17;
Mt 4: 12-23.
MWANGA KWA WALE WALIO GIZANI!
Watu wenye nguvu sio wale wanao jionesha na kujigamba kuwa na nguvu mbele
za watu, bali wale wanaoshinda katika vita hatujui chochote kuhusu wao. Leo
tunatafakari kuhusu wito wetu wa kumfuata Yesu.
Katika somo la kwanza Isaya anawahakikishia watu wa Israeli kwamba sasa
mambo yatakuwa shwari na mazuri. Analeta matumaini katika maisha yao kwamba
wote wanaotembea katika giza wataona mwanga mkuu, na wote wanoishi katika
huzuni watapata furaha kuu. Utabiri huu wa Isaya ni dhahiri umetimizwa kwa ujio
wa Kristo. Yesu ni “Mwanga mkuu” ambao Isaya anaongelea. Kwahiyo Isaya
anatabiri kuhusu habari hii ya kihistoria wakati Yesu akitokea ulimwenguni
kwetu akihubiri Neno lake la Kimungu. Lakini hili neno la Isaya, kwetu
lisiongelee tuu habari ya kihistoria ya utabiri wa ujio wa Kristo na utume
wake, linapaswa lidhihirishe ukweli kwetu kwamba “Yesu ndiye mwanga mkuu”
ambaye anangaa hata katika giza lolote lile ambayo tunakutana nalo katika
maisha.
Injili ya leo inatuambia kwamba Yesu ndiye Mwanga mkuu unaongaa, unao ondoa
giza na kuleta furaha, unaofungua maisha ya huzuni na kuleta furaha katika
maisha. Jaribu kufikiria giza kubwa nene lililo lifunika dunia nzima. Jaribu
kufikiria ukiwa katika jangwa usiku mkubwa na mawingu yamefunika kila kitu na
hamna hata nyota hata moja. Jaribu kufikiria wakati mawingu yakiondoka wakati
jua limeanza kuchomoza. Taratibu giza linaondoka na jua linatoa mwanga na
kuangazia nchi yote. Hii sio taswira ya yaliotokea tu kwa kipindi alichokuja
Yesu na kufanya utume wake tu, inatokea pia kila siku katika maisha yetu
tunapolisikiliza Neno la Mungu kwa uaminifu, na kuliruhusu kupenya akili na
mioyo yetu. Maneno ya Yesu yanapaswa kutujaza sisi na uwepo wa yeye mwenyewe,
kwani yeye ni Mwanga mkuu wa ukweli.
Yesu alikuwa mtu aliyekuwa katika utume, utume wa kutangaza Ufalme wa Mungu
kuwaokoa wanyonge na wadogo, ambao jamii iliwakataa. Utume wake wa wazi ni
alama ya kuanza kuwakomboa wale waliopotea na kuleta mwanga na furaha katika
maisha yao. Anahitaji watu washirikiane naye na kufanya naye kazi katika utume
wake. Aliwachagua mitume wake wa kwanza, aliwaita wakati wakiwa
wanajishughulisha na mambo yao, na mara moja walimfuata hata bila ya kufikiria
kitu kingine. Wafuasi wake wa kwanza walikuwa watu wa kawaida wavuvi,
wakitengeneza neti zao wakijiandaa kuvua samaki. Hawakuwa watu waliosoma au
watu maarufu. Wanaonekana kama hawakidhi kufanya utume wa Yesu, lakini cha
kushangaza upendo wa Mungu usio na kipimo umewabadilisha. Maisha yao yamepewa
thamani na kuwa ya mafanikio na juu yao Kanisa limeanza.
Yesu aliwaangazia akili na mioyo yao na kuwapa nguvu ya kubeba mwanga ambao
ni yeye mwenyewe na kuondoa giza lote na kuleta furaha ulimwenguni kwa ujumbe
wa upendo wa Mungu. Yesu bado anahitaji wafuasi katika nyakati zetu zilizo
vurugika, ambapo kila mtu anavutwa kwenda mwelekeo wake mwenyewe. Mungu
anawatumia watu wasiopendwa. Anawapa nguvu na utukufu. Hivyo tuitikie na
kujitoa kama mitume, walivyojitoa wenyewe kwa Mungu. Mungu anakuita kama ulivyo
uweze kumtangaza na kumshuhudia kwa matendo na maneno yako. Haitaji ubadilike
uwe kama mtu Fulani, bali anakuita kama ulivyo ukamshuhudie kila mahali ulipo.
Sala: Bwana, njoo ndani mwangu na ingia katika giza la akili yangu na moyo
wangu. Njoo uondoe huzuni na uchungu ninao hisi leo. Naomba ulete mwangaza
katika kuchanganikiwa na kuweka akili mpya ya mwanga wa uwepo wa upendo wako.
Bwana, tusaidie tuweze kuitika na kufuata wito wako. Katika wito wangu kama
Kasisi, Mtawa, mlei; ninaomba nijibu wito wako na kuleta mwanga wako kwa wote
walio katika giza. Yesu nakuamini wewe. Amina
No comments:
Post a Comment