MASOMO YA MISA, JANUARI 22, 2023
DOMINIKA YA 3 YA MWAKA A
WIMBO WA MWANZO:
Zab. 96:1, 6
Mwimbieni Bwana wimbo mpya, mwimbieni Bwana,
nchi yote. Heshima na adhama ziko mbele zake, nguvu na uzuri zimo katika
patakatifu pake.
SOMO 1
Isa. 9:1 – 4
Hapo kwanza aliingiza nchi ya Zabuloni na nchi
ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa
tukufu, karibu na njia ya bahari; ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa.
Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru
kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza. Umeliongeza
taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, kama furaha ya wakati wa
mavuno, kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara.
Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo
la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midani.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 27:1, 4, 13-14 (K) 1
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani? (K)
Neno moja nimelitaka kwa Bwana,
Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana
Siku zote za maisha yangu.
Niutazame uzuri wa Bwana,
Na kutafakari hekaluni mwake. (K)
Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)
SOMO 2
1Kor. 1:10 – 13, 17
Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu
Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu
katika nia moja na shauri moja. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu
na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana
yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu husema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni
wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika?
Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizawa kwa jina la Paulo?
Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali
niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristu usije
ukabatilika.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Mt. 4:23
Aleluya, aleluya,
Kristo alihubiri Habari Njema ya ufalme, na
kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.
Aleluya.
INJILI
Mt. 4:12 – 23
Basi Yesu aliposikia ya kwamba Yohane amefungwa,
alikwenda zake mpka Galilaya; akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji
ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali: ili litimie neno lililonenwa na
nabii Isaya, akisema, Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari,
ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa, Watu wale waliokaa katika giza wameona
mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti mwanga umewazukia.
Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na
kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.
Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya
Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye,
wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni,
nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.
Akaendelea mbele, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohane
nduguye, ambao walikuwamo chomboni pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza
nyavu zao; akawaita. Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata.
Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote,
akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya Ufalme, na
kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment