Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA OKTOBA 30, 2026

 



MASOMO YA MISA OKTOBA 30, 2026 
IJUMAA, JUMA LA 30 LA MWAKA

SOMO 1
Fil 1:1-11

Paulo na Timotheo, watumwa wa Kristo Yesu, kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu, walioko Filipi, pamoja na maaskofu na mashemasi. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo, sikuzote kila niwaombeapo ninyi nyote nikisema sala zangu kwa furaha, kwa sababu ya ushirika wenu katika kuieneza Injili, tangu siku ile ya kwanza hata leo hivi. Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu; vile vile kama ilivyo wajibu wangu kufikiri haya juu yenu nyote; kwa sababu ninyi mmo moyoni mwangu; kwa kuwa katika kufungwa kwangu na katika kazi ya kutetea Injili na kuithibitisha, ninyi nyote mmeshirikiana nami neema hii. Maana Mungu ni shahidi wangu, jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote katika moyo wake Kristo Yesu. Na hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote; mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo; hali mmejazwa matunda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 111: 1-6

(K) Matendo ya Bwana ni makuu. 

Aleluya, Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
Matendo ya Bwana ni makuu.
Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo. (K) 

Kazi yake ni heshima na adhama,
Na haki yake yakaa milele.
Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu;
Bwana ni mwenye fadhili na rehema.  (K) 

Amewapa wamchao chakula;
Atalikumbuka agano lake milele.
Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake,
Kwa kuwapa urithi wa mataifa.  (K) 


SHANGILIO
Zab 119:135

Aleluya, Aleluya
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako
nitaitii kwa moyo wangu wote.
Aleluya


INJILI
Lk 14:1-6

Yesu alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. Na tazama, mbele yake palikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa safura. Yesu akajibu, akawaambia wana-sheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponya siku ya sabato, ama sivyo? Wao wakanyamaza. Akamshika, akamponya, akamruhusu aende zake. Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng'ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato? Nao hawakuweza kujibu maneno haya.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Copyright © 2026, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

KUSALI BILA KUCHOKA!



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Alhamisi, Oktoba 29, 2026
Juma la 30 la Mwaka wa Kanisa

Efe 6:10-20;
Zab 143:1-2, 9-10;
Lk 13:31-35


KUSALI BILA KUCHOKA!


Lengo la Barua kwa Waefeso ina lenga kujenga jumuiya ya Wakristo iliyo na upendo na umoja. Leo tuna maelekezo ya mwisho “salini nyakati zote daima katika Roho”. Mara nyingi sala zetu zinaishia katika kusema kwa fomula flani au kutafakari vifungu flani vya maandiko au tukiomba mahitaji yetu kutoka kwa Mungu na kwa kupitia kwa watakatifu.

Sala ni upendo wa kila mara kwa Mungu au “muonekano wetu unajiweka mbele ya Mungu” (Mt. Yohane Paulo II). Kusali nikuwa na umoja wa upendo wa ndani na Mungu, kushiriki kwenye upendo usio na mwisho wa Mungu. Ni kujiunga kwa mtu na Mungu katika muungano wa ndani. Hii inawezekana katika ukimya wa moyo. Uhusiano huu unaweza kujengwa tuu, kwa njia ya maisha ya fadhila. Hili ndilo tunalosikia katika somo la leo. Tunaalikwa tuwe makini dhidi ya ujanja wa yule muovu, tuzitambue mbinu zake katika jitihada zetu za kutaka kuwa na Mungu, kuwa mwaminifu, mwenye haki na mwenye Amani ya Injili. Maisha yetu ya fadhila yatakuwa ni maisha ya kusali daima katika Roho.

Sala. Ee Bwana, ninaomba unipe fadhila zote zinazo hitajika katika hali yangu ya maisha ili niweze kukuwa katika maisha yangu ya sala. Amina


Copyright ©2013-2026 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, OKTOBA 29, 2026



MASOMO YA MISA, OKTOBA 29, 2026
ALHAMISI, JUMA LA 30 LA MWAKA WA KANISA

SOMO 1
Efe. 6:10 – 20

Mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu war oho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya mani; zaidi ya yote mkitwaa ngao ya Imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili; ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika hiyo kunena jinsi inipasavyo kunena.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 144:1 – 2, 9 – 10 (K) 1

(K) Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu.

Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu,
Anifundishaye mikono yangu vita,
Vidole vyangu kupigana. (K)

Mhisani wangu na boma langu,
Ngome yangu na mwokozi wangu,
Ngao yangu niliyemkimbilia,
Huwatiisha watu wangu chini yangu. (K)

Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya,
Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia.
Awapaye wafalme wokovu,
Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu. (K)



SHANGILIO
Zab. 119:18

Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.



INJILI
Lk. 13:31-35

Saa ile ile, Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea Yesu, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.

Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka! Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa. Ninawaambia, hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana.’ 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.                        

UMOJA KATIKA WINGI !





“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatatu, Oktoba 28, 2026,
Juma la 30 la Mwaka wa Kanisa

Sikukuu ya Wat. Simoni na Yuda, Mitume.

Ef 2:19-22
Zab 18:2-5
Lk 6:12-16


UMOJA KATIKA WINGI !


Mungu humwalika mwanadamu daima katika kazi yake ya ukombozi. Yesu aliwachagua watu wa kawaida kabisa wa kipindi chake kuwa mitume wake. Anawapa nguvu na mamlaka na wakawa waaminifu katika kuendeleza kutimiza mapenzi ya Baba. Luka, anatuambia Yesu alienda mlimani kusali, na alikesha usiku kucha katika kusali. Ndipo baada ya kusali anawachagua mitume kumi na mbili. Na kati ya hao wawili ndio tunafanya sikukuu yao leo, Simoni na Yuda. Habari za hawa wawili zijulikanazo ni chache sana. Tunajua walichaguliwa na Yesu kuwa mitume wake. Mtume ni yule anayetumwa. Hawa walishirikiana kufanya kazi pamoja katika nchi ya Uajemi na huko waliuawa kwa ajili ya Kristo. Kwasababu hiyo sikukuu yao huadhimishwa pamoja. Mtume simoni aliitwa ‘Zeloti’ maana yake mwenye bidii kwasababu alifanya bidii kutangaza ujumbe kuhusu Yesu kokote. Mtume Yuda aliitwa ‘Tadayo’maanake ‘hodari’ili kumtofautisha na Yuda Iskarioti msaliti. Alikuwa ndugu yake Yakobo mdogo kama tunavyosoma katika Injili na kama anavyosema mwenyewe katika barua yake ‘Barua ya Yuda’na barua hii iliandikwa kwa ajili ya makanisa yaliokuwa karibu na nchi Takatifu kama alivyofanya nduguye Yakobo.

Unaweza kufikiria ni watu wa namna ghani aliokuwa nao Yesu. Petro aliyekuwa msemaji na mwenye hofu lakini bado Yesu alimchagua kuongoza. Yakobo na Yohane waliokuwa wakipigania kuwa karibu na Yesu katika ufalme walio utafsiri vibaya; Mathayo mtoza ushuru, nk. Tunaweza kufikiria kukaa kwao pamoja kulikuwa je hapo mwanzo. Pamoja na kutoelewana wao kwa wao waliponywa na upendo usiozuilika wa Yesu alioutoa kwao.

Somo la kwanza linamalizia vizuri kabisa: “tangu sasa ninyi si wageni tena wala wapitaji, bali ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu”. (Efe 2:19). Je, tupo tayari kumruhusu Yesu atujenge kama watu wa nyumba yake, hata ikiwa nikuwa pamoja na wale tusiowapenda?

Sala: Bwana Yesu, ninaomba upendo wako unipe nguvu kuwakubali wenzangu kama walivyo. Amina.

Copyright ©2013-2026 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA OKTOBA 28, 2026



MASOMO YA MISA OKTOBA 28, 2026
JUMATANO, JUMA LA  30 LA MWAKA

SIKUKUU YA WATAKATIFU SIMONI NA YUDA, MITUME

SOMO 1
Efe. 2:19-22

Tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kuku ahata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 19:1-4 (K) 4

(K) Sauti yao imeenea duniani mwote.

Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa. (K)

Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
Katika hizo ameliwekea jua hema. (K)


SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Ee Mungu, tunakusifu, tunakukiri kuwa Bwana. Jamii tukufu ya Mitume inakusifu.
Aleluya.


INJILI
Lk. 6:12-16

Yesu aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohane, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote, na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.        

UFALME WA MUNGU-UPO NA BADO UTAKAMILIKA



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne, Oktoba 27, 2026
Juma la 30 la Mwaka wa Kanisa

Ef 5: 21-33;
Zab 128: 1-5;
Lk 13: 18-21


UFALME WA MUNGU-UPO NA BADO UTAKAMILIKA

Katika somo la kwanza Mtume Paulo anaendelea na maelekezo yake kwa Waefeso jinsi ya kuenenda kama wafuasi wa Kristo na leo anaingia katika ngazi ya familia. Anawaambia wake wawatii waume zao na waume wawapende wake zao. Ni katika kuendeleza tunu hizi katika familia ndipo twaweza kusema kuwa tunajenga ufalme wa Mungu katika familia zetu. Tunapoishi vizuri na wenzetu kwa upendo na kwa fadhili za Kimungu kama alivyotufundisha Kristo tunakuwa tunaishi Ufalme wa Mungu tungali hapa duniani. Ni katika kuuishi vizuri ufalme huo hapa duniani inatupa kibali cha utimilifu wake katika maisha yajayo. Yesu anatoa mifano miwili katika akilielezea Ufalme huu wa Mungu.

Ni ufalme ghani unao hubiriwa na Yesu? Mfano wa punji ya haradali na chachu unaelezea sifa za muhimu za Ufalme wa Mungu alio hubiri Yesu: udogo wake, tabia yake yakutokuonekana kirahisi; kazi yake na uwepo wake.

Yesu leo anafananisha ufalme wa Mungu na punji ya haradali na chachu. Puche ya haradali ni ndogo tena sana. Inapopandwa ardhini inakuwa na kuwa mti mkubwa ambapo ndege wa angani hupata makao. Lakini, pamoja na kwamba ni ndogo, na haijulikani na kujificha inapokuwa ardhini haibaki hapo tu bali huchipua na kumea. Chachu kidogo sana, ambayo huwezi kuiona kwa macho baada ya kuwekwa katika unga, haibaki kama ilivyo bali huumua unga wote.

Tabia ya Uwepo wake na utimilifu wake ujao wa Ufalme wa Mungu unaweza kuwa wetu tu kama matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu.

Sala: Bwana, tunaomba ufungue macho yetu tuweze kutambua maajabu ya Ufalme wako, uliojificha na uwepo wake katika mambo madogo. Amina.

Copyright ©2013-2026 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, OKTOBA 27, 2026



MASOMO YA MISA, OKTOBA 27, 2026
JUMANNE, JUMA LA 30 LA MWAKA WA KANISA

SOMO 1
Efe. 5:21 – 33

Hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo. Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.

Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa atukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wal alolote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda wenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye navyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.

Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa. Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 128:1 – 5 (K)

(K) Heri kila mtu amchaye Bwana.

Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika njia yake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema. (K)

Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni
Wakiizunguka meza yako. (K)

Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana.
Bwana akubariki toka Sayuni;
Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako. (K)


SHANGILIO
1Pet. 1:25

Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.


INJILI
Lk. 13:18-21

Yesu alisema, Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini? Umefanana na punji ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake.

Akasema mara ya pili, Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pichi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com. 

HURUMA YA MUNGU!



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatatu, Oktoba 26, 2026
Juma la 30 la Mwaka wa Kanisa

Ef 4:32 – 5:8;
Zab 1:1-4, 6;
Lk 13:10-17


HURUMA YA MUNGU!

Katika Injili ya Leo Yesu anamponya Mwanamke mmoja mgonjwa aliyekuwa na pepo kwa muda wa miaka kumi nane. Lakini cha kushangaza viongozi wa Sinagogi hawakufurahi, kwasababu wao walijishughulisha na Sabato na si yule Mwanamke aliyekuwa mgonjwa akiteseka. Ndio maana Yesu anawaita “Wanafiki” kwasababu walishindwa kutoa mahitaji ya watu, na badala yake kuwafundisha watu woga na kujenga watu wasiwasi mioyoni mwao kuhusu Mungu. Walishindwa kuonesha upendo na kufundisha huruma na msamaha wa Mungu Baba na mara nyingi walielekea kwenye adhabu, na kushika sheria kwa nguvu.

Katika hali hiyo hiyo, Paulo anawaambia Waefeso wawe wakarimu, na wenye huruma moyoni na msamaha kwa wengine kwasababu Mungu amewaonesha huruma yake kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo. Anawaita wamuige Mungu kwa kumpenda Yesu Kristo kama njia pekee ya kumwendea Mungu, ni Yesu pekee aliyetupa akili kamili kuhusu Mungu. Hakuna aliyefahamu ufalme wa Mungu unafananaje, kabla ya Yesu kuja kutupa mifano mbali mbali. Leo Yesu anatualika leo tuwatembelee wagonjwa, wanaoteseka na kuwaonesha huruma ambayo Mungu ameionesha kwetu.

Sala: Bwana mpendwa, tusaidie tuweze kuhisi upendo wako na huruma yako ili tuweze kuwa mwanga wa kweli wa huruma na ukarimu wako kwa wanadamu wote.


Copyright ©2013-2026 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

MASOMO YA MISA, OKTOBA 26, 2026



MASOMO YA MISA, OKTOBA 26, 2026
JUMATATU,  JUMA LA 30 LA MWAKA WA KANISA


SOMO 1
Efe. 4:32 – 5:8

Iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi; tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato. Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wowote wala kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu.

Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi. Basi msishirikiane nao. Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 68:1, 3, 5 – 6, 19 – 20 (K)

(K) Mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa.

Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki; wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. (K)

Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)

Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo,
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki.
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)


SHANGILIO
Yak. 1:18

Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.


INJILI
Lk. 13:10-17

Siku ya sabato Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.

Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. Lakini Bwana akamjibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, Je! Hamfungi ng’ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha? Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato? Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.      

UPENDO:ALAMA YA UFUASI WA KIKRISTO!


“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumapili, Oktoba 25, 2026
Juma la 30 la Mwaka

Sikukuu ya Watakatifu Simon na Yuda, Mitume

Kut 22:20-26; 
Zab 17:2-4, 47, 51; 
1Thes 1:5-10; 
Mt 22:34-40


UPENDO:ALAMA YA UFUASI WA KIKRISTO!

Masomo ya leo yanatualika tutafakari juu ya msingi wa maisha ya kila mfuasi wa Kristo yalipojengwa: upendo kwa Mungu na jirani. Wakati mwingine tunapotezwa katika mawazo mabaya kuhusu upendo kwa Mungu na kwa jirani. Ni vizuri kutafakari juu ya hili mara kwa mara. Mwalimu wa Sheria alimuuliza Yesu swali ili kumtega. “ni Amri ipi iliyo kuu zaidi katika sheria?’ Ni wazi uhusiano wa Yesu na hawa viongozi wa dini unaonekana ulikuwa una malumbano. Walikuwa wakimjaribu hata kumtega. Lakini kama kawaida Yesu aliendelea kuwanyamazisha kwa maneno yake ya hekima.

Yesu alimjibu mwalimu wa sheria kwamba “umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote kwa akili zako zote… “hii ni amri kubwa kuliko zote na ya pili, “mpende jirani yako kama nafsi yako” (Mt 22:37-39). Yesu anatoa ufupisho wa sheria zote za maadili zinazo patikana katika Amri kumi za Mungu. Amri tatu za mwanzo, zinasisitiza upendo kwa Mungu kwa moyo wote. Na amri nyingine zinasisitiza upendo kwa jirani. Sheria ya maadili ya Mungu ni rahisi kama hizi amri mbili tu zinavyosema.

Mfuasi wa Kristo anapaswa kufuata sheria ya upendo. Sheria hii ina nyanja mbili –upendo kwa Mungu na upendo kwa jirani, na hii inakuwa ni alama ya ufuasi wetu. Nini maana ya kumpenda Mungu na jirani? Kwanza kabisa upendo wa Mungu ni kuuelewa upendo wa Mungu kwetu sisi. Sisi ni dhaifu kabisa na hatuwezi kumpenda Mungu kama inavyopaswa. Lakini kwa njia ya Kristo tunaweza kufahamu kwamba Mungu anatupenda. Hivyo kufahamu upendo wa Mungu licha ya kwamba mtu ni dhaifu inamfanya mtu ampende Mungu kama shukrani. Na huu ndio mwanzo wa upendo. Wakati mtoto mdogo anavyofahamu upendo wa mama juu yake, hauleti chochote kwa Mama. Huu ndio upendo wetu kwa Mungu. Wakati tunavyo ufahamu upendo wa Mungu sisi hatuongezi chochote kwa Mungu, hatuta anguka kwenye dhambi tutafana na yale yanayo mpendeza yeye. Inamfurahisha Mungu tunavyo pendana sisi kwa sisi. Mmoja akianza kumpenda Mungu, anaanza pia kuwapenda wengine.

Somo la kwanza leo kutoka katika kitabu cha kutoka linaelezea amri ya Mungu kwa wana wa Israeli: upendo kwa jirani. Ni wakati gani upendo wangu kwa jirani utakuwa mkamilifu? Tunapo wapenda majirani zetu tunatamani na wao wapate nafasi katika ufalme wa Mungu. Tunakuwa tunatamani kama wataishi katika neema ya Mungu siku zote za maisha yao. Na hivyo waweze kuishi milele kwa sababu ya neema tuliopokea kutoka kwa Kristo. Tukiwapenda wenzetu namna hii hatuwezi kuwanyima chochote au mahitaji yeyote wanayo taka kwetu. Tunakumbuka alichosema Yesu, kwamba mlicho watendea wadogo hawa mlinitendea mimi. Tunaenda kuwatembelea watu walio katika mahitaji mbali mbali kwa njia ambazo zipo katika uwezo wetu. Na huu ndio upendo kwa jirani.

Mt. Paulo katika barua yake kwa Wathesalonike katika somo la pili leo, anawakumbusha umuhimu wa kuongoka katika Imani ya maisha ya Kikristo, ambapo ni kumtumikia Mungu na kumtumikia Mwanae Yesu Kristo aliye mfunua Baba na Roho kwetu.

Tafakari juu ya wito wa kumpenda Mungu na jirani kwa jinsi ulivyo. Fikiria juu ya neno “wote” kupenda kwa moyo “wote”, na ukitafakari kuhusu hili utatambua njia ambazo umeshindwa kutoa kitu kwa ajili ya Mungu na hata kwa jirani. Ukiona upungufu wako, anza tena kwa kujikabidhi katika kuwa zawadi kwa Mungu na kwa jirani.

Sala: Bwana, ninachagua kukupenda wewe kwa Moyo wangu wote, akili na utashi wote na nguvu. Nipe neema niweze kuishi amri hizi mbili za upendo na kuziona kama njia za kuelekea kwenye utakatifu wa maisha. Ninakupenda Bwana wangu. Yesu nakuamini wewe. Amina


Copyright ©2013-2026 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com