“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatatu, Oktoba 24, 2022
Juma la 30 la Mwaka wa Kanisa
Ef 4:32 – 5:8;
Zab 1:1-4, 6;
Lk 13:10-17
HURUMA YA MUNGU!
Katika Injili ya Leo Yesu anamponya Mwanamke mmoja mgonjwa aliyekuwa na pepo kwa muda wa miaka kumi nane. Lakini cha kushangaza viongozi wa Sinagogi hawakufurahi, kwasababu wao walijishughulisha na Sabato na si yule Mwanamke aliyekuwa mgonjwa akiteseka. Ndio maana Yesu anawaita “Wanafiki” kwasababu walishindwa kutoa mahitaji ya watu, na badala yake kuwafundisha watu woga na kujenga watu wasiwasi mioyoni mwao kuhusu Mungu. Walishindwa kuonesha upendo na kufundisha huruma na msamaha wa Mungu Baba na mara nyingi walielekea kwenye adhabu, na kushika sheria kwa nguvu.
Katika hali hiyo hiyo, Paulo anawaambia Waefeso wawe wakarimu, na wenye huruma moyoni na msamaha kwa wengine kwasababu Mungu amewaonesha huruma yake kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo. Anawaita wamuige Mungu kwa kumpenda Yesu Kristo kama njia pekee ya kumwendea Mungu, ni Yesu pekee aliyetupa akili kamili kuhusu Mungu. Hakuna aliyefahamu ufalme wa Mungu unafananaje, kabla ya Yesu kuja kutupa mifano mbali mbali. Leo Yesu anatualika leo tuwatembelee wagonjwa, wanaoteseka na kuwaonesha huruma ambayo Mungu ameionesha kwetu.
Sala: Bwana mpendwa, tusaidie tuweze kuhisi upendo wako na huruma yako ili tuweze kuwa mwanga wa kweli wa huruma na ukarimu wako kwa wanadamu wote.
No comments:
Post a Comment