MASOMO YA MISA, OKTOBA 31, 2024
ALHAMISI, JUMA LA 30 LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Efe. 6:10 – 20
Mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu war oho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya mani; zaidi ya yote mkitwaa ngao ya Imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.
Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili; ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika hiyo kunena jinsi inipasavyo kunena.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 144:1 – 2, 9 – 10 (K) 1
(K) Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu.
Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu,
Anifundishaye mikono yangu vita,
Vidole vyangu kupigana. (K)
Mhisani wangu na boma langu,
Ngome yangu na mwokozi wangu,
Ngao yangu niliyemkimbilia,
Huwatiisha watu wangu chini yangu. (K)
Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya,
Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia.
Awapaye wafalme wokovu,
Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu. (K)
SHANGILIO
Zab. 119:18
Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.
INJILI
Lk. 13:31-35
Saa ile ile, Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea Yesu, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.
Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka! Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa. Ninawaambia, hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana.’
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright
© 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture
readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by
T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible
Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki:
see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment