AMETENDA MAMBO YOTE VEMA:
Viziwi amewafanya wasikie na bubu waseme.
MAINGILIO
Katika jamii zetu kuna makundi mbalimbali ya watu. Wapo watu ambao ni matajiri, masikini, wagonjwa na wenye afya. Cha kutambua ni kuwa sote tupo sawa mbele ya Mungu kwani tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.(Mw 1:27)
Hivyo sisi sote tu watoto wa Mungu .Je kama sote tu sawa mbele ya Mungu kwa nini wengine wazaliwe wakiwa na kasoro na wengine bila ta tizo lolote? Huo ni mpango wa Mungu, chochote afanyacho Mungu ni chema, hakuna kitu kibaya kinachotoka kwa Mungu. Mambo mengine Mungu anayaruhusu yatokee ili tuutambue ukuu wake. Mungu aliyeumba bubu, viziwi,vipofu na viwete ndiye aliyetuumba sisi tusio na kasoro yoyote.Hata sisi tungeweza kuumbwa kama wao.
Katika jamii ya Kiyahudi ugonjwa ulichukuliwa kama adhabu kutoka kwa Mungu, hivyo kuzaaliwa kiziwi au bubu lionekana kama laana sababuhali hiyo ilimfanya mtu asiweze kusikia neon la Mungu na kulitangaza. Wagonjwa pia walionekana kuwa ni wadhambi. ( Yoh 9:1-3 ) Yesu alikuwa akitembea pamoja na wanaunzi wake wakamwona mtu kipofu tangu kuzaliwa, wanafunzi wkamuliza “ ni yupi aliyetenda dhambi mtu huyu au wazazi wake? Yesu akajibu huyu hakutenda dhabmi wala wazazi wake, bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yae”
Ufafanuzi.
Somo la kwanza linatuletea hali ya jamii iliyo katika dhiki kubwa, watu waliokata tamaa, wenye hofu moyoni mwao, walio katika mazingira ya utumwa. Katika hali hiyo nabii Isaya anatumwa na Mungu kuwapelekea ujumbe wenye kuleta faraja, kwamba Mungu atakuja kuwaokoa kutoka katika hofu na mateso yao. Katika siku hizo furaha itashamiri mioyoni mwao,kwani macho ya vipofu yatafumbuliwa na masikio ya viziwi yatazibuliwa, vilema watarukaruka na bubu wataimba. Utabiri unaotolewa na nabii Isaya juu ya taifa la Israeli huko utumwani Babeli ni mfano wa kukombolewa kwetu kutoka utumwa wa dhambi na shetani. Utabiri huo umetimizwa katika nafsi ya Yesu Kristo kama tulivyosikia katika somo la Injili. Kristo anafanya miujiza na watu wanashikwa na mshangao na kusema amefanya yote vema, viziwi amewafanya wasikie an bubu waseme. Kwa njia ya mateso kifo na ufufuko Kristo amerejesha hali ile iliyokuwapo kabla ulimwengu haujaharibika kutokana na dhambi za mwanadamu. Yesu anautengeneza ulimwangu upya. Mtu mpya anaumbwa, anayeweza kusikiliza vizuri na kutangaza matendo makuu ya Mungu.
Katika somo la Injli, tunamwona mtu aliye katika vifungo vya mwili, mtu aliye bubu na kiziwi anaponywa na Bwana wetu Yesu Kristo. Huyu ni mtu aliyetengwa na jamii katika ulimwengu wa mawasiliano. Anaishi katika hali ya upweke kwani hawezi kuwasiliani na wengine na kushirikiana nao. Alihitaji mganga wa kimungu awezaye kuponya mwili na roho pamoja. Alimhitaji Yesu tunayemhitaji hata sisi leo katika hali yetu ya kuwa bubu na kiziwi kiroho.
Injili ya leo inatufanya tujiulize maswali matatu kuhusu muujiza aliyoufanya Yesu.
i) Kwanini Yesu alimchukua mgonjwa faraghani mbali na kundi la watu?
ii) Kwanini alimgusa kwa vidole masikioni na kupaka mate ulimi wake?
iii) Kwanini alikataza watu wasitangaze muujiza huo?
Jibu la swali la kwanza:Yawezekana njia aliyotumia Yesu kumponya huyu mgonjwa isieleweke kwetu, lakini katika kipindi cha Yesu ilikuwa ni kawaida kwa waganga au waponyaji kuwaponya wagonjwa walioletwa kwao kwa namna Yesu alivyomponya yule mgonjwa.Yesu alimtenga na kumhudumia kama mgonjwa wa pekee.
Swali la pili, kwa nini alimgusa kwa vidole masikioni na kupaka mate ulimi? Ndugu zangu katika Kristo, tukumbuke kuwa Yesu alikuwa Mungu na mtu. Katika kufanya miujiza kila mara alishirikisha ubinadamu wake katika matendo ya kimuungu, ingawa angeweza kumponya mgonjwa kwa neon moja tu. Anatufundisha kuwa tunapomtegemea Mungu tusiache kushirikisha bidii zetu pia.
Pia kwa wakati ule mate yalidhaniwa kuwa na pumzi ambayo ni uzima wa mtu, pia mate yaliaminika kuwa ni dawa, hivyo,Yesu alimpa yule mgonjwa pumzi yake au roho yake.
Swali la tatu, kwa nini Yesu aliwakataza watu wasitangaze muujiza huo? Yesu aliwakataza watu wasitangaze muujiza huo kwa sababu, hakupenda kujitambulisha mapema kuwa yeye ndiye Masiha. Ilikuwa ni vigumu kumuelewa na kumkubali kuwa ndiye Masiha. Kujitangaza mapema kuwa ndiye Masiha kungemzuia kuikamilisha kazi ilyomleta duniani. Hata alipofanya muujiza wa kugeuza mikate hawakumwelewa. Mitume walimwelewa Yesu ni nani baada ya kifo na ufufuko wake. Pia lengo la Yesu kufanya miujiza lilikuwa siyo kujionyesha na kupata sifa mbele za watu. Hilo pia lilikuwa fundisho kwa mitume wake na hata kwetu pia. Tusitafute sifa binafsi tunapofanya kazi ya Mungu.Yatupasa tuseme “sisi ni watumishi tusio na faida, tumefanya tu yale yanayotupasa”.
Katika Maisha:
Katika injili ya leo mtu aliyezaliwa kiziwi na bubu anawakilisha wale wote ambao masikio yao yamefungwa, hawawezi kusikiliza neon la Mungu na kumsifu kwa midomo yao.
Mt Paulo Rom 10: 17 anasema “basi imani chanzo chake ni kusikia na kusikiliza huja kwa neon la Kristo.” Kabla ya kuja Kristo watu wote masikio yao yalikuwa yamefunngwa katika kuupata ujumbe wa Mungu. Hata wayahudi japo manabii waliwahubiria, waliacha kuwasikiliza na hivyo wakabaki kuwa viziwi. Kwa kumponya bubu kiziwi, Yesu anatufundisha kuwa mazunngumzo mapya kati ya mbingu na dunia yameanza. Wayahudi, wapagani na wengine wote masikio ya mioyo yao yamefunguliwa tayari kupopkea ujumbe wa Mungu.Wakati tunapobatizwa, tunaponywa kutoka hali yetu ya kuwa kiziwi na bubu kiroho, tunaweza kusikiliza nenola Mungu na hivyo tunatengwa na kundi la wapagani.Hatutengwi kimwili bali kiroho kwa sababu tumepokea maisha mapya. Tendo alilofanya Yesu la kuweka vidole masikioni, linafanyika pia wakati wa ubatizo. Anayebatiza anasema “ Bwana Yesu aliyefanya viziwi wasikie na bubu waseme, akujalie uweze kusikia kwa masikio neno lake na kuungama kwa mdomo imani ya kikristo, kwa sifa na utukufu wa Mungu baba”.
Mtu aliyeponywa katika injili ya leo aliishi kati ya jamii ya watu. Kwa kuwa watu waliomzunguka walikuwa na huruma na upendo walimpeleka kwa Yesu. Wana imani kuwa Yesu atawasikiliza, na anaweza kumponya mgonjwa wao. Wanampeleka ili aponywe, awe mshiriki mwenzao katika furaha wanayopata katika maisha ya kila siku. Wependwa katika Kristo kila mmoja wetu amejaliwa na Mungu mambo kadhaa ambayo pengine jirani yake hana. Wengine wamejaliwa afya njema lakini hawana amani katika familia zao. Jukumu letu sote katika hali hizo tofauti ni kupelekana kwa Yesu. Yawezekana tukajifikiria kuwa sisi tu wazima sio viziwi wala bubu, na hivyo hatuihitaji kupelekana kwa Yesu. Yawezekana sisi ni viziwi na bubu kiroho.
i) Viziwi wa kiroho: Hawa ni wakristo wasiopenda hata mara moja kusikia mambo yanayohusu roho zao, wanapenda yanayohusu miili yao tu. Yanayohusu Mungu na neema zake wanayakwepa. Hawapendi kusikiliza neon la Mungu, wanaziba masikio yao kwa makusudi ili wasisikie, na hata wakisikia wanayaacha hapapa kanisani. Viziwi wa kiriho daima hawapendi kushauriwa au kuonywa kuhusu purukushani za roho zao.
ii) Bubu wa kiroho: Hawa ni wale wasioopenda kusali, sala zinawakera. Sala zao ni harakaharaka au kuacha kabisa. Pia hawa ni wale wasioppenda kuitangaza habari njema. Wapo bubu wakongwe zaidi, ni wale wanaokwepa kuhoji dhamiri zao na kukiri dhambi zao katika kitubio. Wapendwa katika Kristo, watu hao niliowataja wapo na tunaishi nao. Je tunawasaidia ili wabadilike? Tunawashauri waje kanisani? Au tunawaona hawana thamani tena mbele ya Mungu? Tunapaswa tuwapelekee ujumbe wa Mungu kama nabii Isaya alivyofanya.Tunawajibika kwa maisha yetu na yawenzetu pia. Kamwe tusitoe majibu kama Kaini alivyomjibu Mungu.Baada ya Kaini kumuua ngugu yake Abeli Mungu alimuliza yulo wapi ngugu yako? Akajibu mim siyo mlinzi ……
Yesu daima yupo, anangoja tumpelekee matatizo yetu. Yeye ni daktari wa roho zetu. Daktarri hawezi kutoka hospitalini akufuate wewe mgonjwa nyumbani, bali wewe wapaswa kumfuata. Anasubiri tumpelekee bubu na viziwi wa kiroho walio katika jumuiya zetu. Tukifanya hivyo tutawaleta wengi kwa Yesu. Tunapomsaidia mwenye dhambi mmoja akatubu na kurudi, Malaika mbiguni hushangilia na hufurahi.
Jambo la kujifunza kwa yule aliyepelekwa kwa Yesu, ni kuwa alikubali kwenda. Angekataa wasingemlazimisha na angebaki na tatizo lake. Ukweli ni kwamba ukipelekwa kwa Yesu kwa kulazimishwa huwezi kuponywa kwa sababu huna imani. Masharti ya kuponywa na Yesu ni kuwa na imani (Mt 9:27).
Tukiwaendea wenye shida na kuwaudumia bila ubaguzi tutakuwa tunafanya kazi ya Kristo isiyo na mipaka. Yakobo mtume katika somo la pili anatuasa tusiwe na imani inayobagua. Kristo alikuja kwa ajili yo wote na alikufa kwa ajili ya wote. Tunapaswa kuzifanya jumuiya zetu ziwe ishara wazi ya matumani kwa watu wote hasa waliokata tama. Tuwapokee wale wote walioathirika kwa dhuluma, magonjwa na wale wote wanaonyimwa haki zao kwa kutopewa nafasi katika jumuiya zao.
Hitimisho
Mungu ametujalia kila mmoja yale anyoona kuwa yanatufaa katika kumtafuta yeye. Hapendi kuona kiziwi kiroho asiyelisikia neon lake, au bubu kiroho asiyelitangaza neno lake. Mara nyingi ukiziwi na ububu tunajitafutia wenyewe kwa kuambatana na shetani.
Nabii Isaya anatuambia, jipeni moyo msiogope, naye Kristo anatuambia maneno hayohayo msiogope jipeni moyo nimeushinda ulimwrngu.Tumfuate Kristo nasi tutakuwa washindi kama yeye.
Amen Sana barikiwa na bwana🙏🙏
ReplyDeleteBaraka za bwana ziwe juu yako #Amina
ReplyDelete