MASOMO YA MISA,
JUMANNE, OKTOBA 14, 2025
JUMANNE, OKTOBA 14, 2025
JUMA LA 28 LA MWAKA
________
SOMO I
Rum. 1:16-25
Siionei haya Injili; kwa sababu I uweza wa mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. Kwa maana haki ya Mung inadhihirishwa ndani yake, toka Imani hata Imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa Imani.
Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu. Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa Dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia. Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milelle na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru; kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kushukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo. Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.
Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
________
WIMBO WA KATIKATI Zab. 19:1-4
(K) Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu.
Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa.
Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
________
SHANGILIO
Zab. 19:8Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya.
________INJILI
Lk. 11:37-41
Yesu alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani. Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula. Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang’anyi na uovu. Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndania pia? Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu.
Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo
________
Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:
Post a Comment