“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatatu, Oktoba 13, 2025.
Juma la 28 la Mwaka
Rom 1: 1-7;
Zab 98: 1-4 (K) 2;
Lk 11: 29-32.
ISHARA YA YONA
Je, unatamani kwamba Mungu akupe ishara kutoka Mbinguni kama njia ya
kukuonesha njia iliyo sawa au muelekeo mzuri wa maisha yako? Je, unategemea
ishara kutoka kwa Mungu na kuitegemea? Kama Mungu alikuwa anatupa ishara ambayo
inafunua kuhusu maisha yetu tungepaswa kuitegemea na kuipokea kama zawadi.
Lakini kupokea ishara kutoka kwa Mungu ni tofauti na kutafuta ishara kutoka kwa
Mungu.
Leo, Yesu anawaonya wale wanaotaka ishara. Kwa nini Yesu anaongea kwa ukali
kuhusu kupinga ishara? Kwa sehemu kubwa, anataka sisi tumtafute yeye kwa njia
ya Imani, badala ya ishara. Yesu anasema hakuna ishara mtakayopewa isipokuwa
ishara ya Yona.
Ishara ya Yona ni ishara ya ufufuko. Sehemu ya kulinganisha inaoneshwa kwa
zile siku tatu ambazo Yona alikaa ndani ya tumbo la samaki na kukaa kwa Yesu
siku tatu katika tumbo la mama ardhi, na kufufuka siku ya tatu. Wote wawili
Yona na Yesu walihubiri toba. Kuhubiri kwa Yona tu bila hata ya ishara ilitosha
kabisa kwa watu wa Ninawi. Lakini, licha ya miujiza yote mikuu aliyofanya Yesu,
haikutosha kwa watu kuamini kiasi kwamba wanahitaji tena ishara, kwa kweli
mioyo ya Wayahudi ilikuwa migumu. Yesu anasema kwamba utume wake ni mkubwa hata
kuliko ule wa Yona lakini ni ajabu kwamba watu wamekataa kutubu. Ndio maana
Yesu anawaita kizazi kibaya na kilicho potoka, kwasababu hawaamini wala
kuongoka. Yesu anahakikisha wafuasi wake wanamuelewa na kufahamu ufalme wake
kwa uhakika.
Tafakari, juu ya “ishara” ambayo Mungu alishatoa. Na kama unajikuta
mwenyewe ukihangaika na maswali ya maisha, geukia na kumbuka ishara ambayo
Mungu alishakupa. Fungua macho na tazama kiini cha Imani yetu; uzima, kifo na
ufufuko wa Yesu Kristo. Ni katika hili kila swali linapata jibu na kila neema
inatolewa. Hatuhitaji kingine zaidi.
Sala: Bwana, maisha yako, kifo na ufufuko ndio yote ninayo hitaji katika
maisha yangu. Sadaka yako kamili inanipa mimi jibu kamili na kunipa kila neema.
Ninakuomba nikugeukie wewe ishara ambayo ninahitaji kila siku. Yesu, nakuamini
wewe. Amina
No comments:
Post a Comment