MASOMO YA MISA, FEBRUARI 15, 2022
JUMANNE, JUMA LA 6 LA MWAKAWA KANISA
SOMO 1
Yak. 1:12-18
Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea
taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao.Mtu ajaribiwapo, asiseme,
Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, mmoja hujaribiwa
na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha
kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.Ndugu
zangu wapenzi, msidanganyike. Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho
kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna
kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka. Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa
sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 94:12-15, 18-19 (K) 12
(K) Ee Bwana, heri mtu yule uliyemfundisha.
Ee Bwana, heri mtu yule umwadhibuye na kumfundisha,
Kwa sheria yako;
Mpate kumstarehesha siku ya mabaya. (K)
Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake,
Wala hutauacha urithi wake,
Maana hukumu itairejea haki,
Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata. (K)
Niliposema, mguu wangu unateleza;
Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza.
Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu,
Faraja zako zaifurahisha roho yangu. (K)
SHANGILIO
Yn. 14:23
Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu, na baba yangu atampenda, nasi
tutakuja kwake.
Aleluya.
INJILI
Mk. 8:14 – 21
Wafuasi wake Yesu walisahau kuchukua mikate, wala chomboni hawana ila
mkate mmoja tu. Akawaagiza, akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya
Mafarisayo na chachu ya Herode. Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana
mikate.Naye Yesu akatambua, akawaambia, Mbona mnabishana kwa sababu hamna
mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! Mioyo yenu ni mizito? Mna macho,
hamwoni; mna masikio, hamsikii? Wala hamkumbuki? Nilipoivunja ile mikate mitano
na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande?
Wakamwambia, Kumi na viwili. Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua
makanda mangapi yamejaa vipande? Wakamwambia, Saba. Akawaambia, Hamjafahamu
bado?
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright
© 2022, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora
– Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment