“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Januari
22 2026
1Sam.
18:6-9; 19:1-7
Zab.
56:1-2, 8-12 (K) 4
Mk
3: 7-12
KATIKA
SAFARI YA KUKUTANA NA YESU!
Karibuni ndugu zangu
kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo neno la Bwana katika asubuhi ya leo
linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunakutana na ugomvi ukitokea
kati ya Daudi na Sauli baada ya Daudi kumwua Goliathi. Ukweli ni kwamba Sauli
kama mfalme wa Israeli ndiye aliyepaswa kwenda kupigana na Goliathi lakini
alimwogopa Goliathi. Daudi akajitolea kwenda kupigana naye na kumshinda na watu
wakafurahi-wanawake wa Israeli waliusifu ushujaa wake. Lakini Sauli
anakasirika, anamuona Daudi kama mshindani anayetafuta kuuchukua ufalme wake na
hivyo anaanza kutaka kumwangamiza.
Lakini uamuzi huu wa
Sauli ulikuwa ni shida tupu kwani kwani Mungu yupo upande wa Daudi. Mwishowe
Sauli anaanza kujitutumua kupigana na Daudi mwishowe Sauli atakufa tena kifo cha
aibu.
Ndugu zangu, Sauli
angemkubali Daudi na kumpokea, angesaidia katika kuuimarisha ufalme wake.
Lakini badala yake alimuona kama adui wa Ufalme wake na ndio maana aliishia
kuupoteza ufalme badala ya kuuimarisha ufalme. Hili liwe fundisho kwetu ndugu zangu.
Katika maisha tutakutana na watu ambao kwa kweli Mungu kawabariki na wanauwezo
kuliko sisi. Tuwakubali na kuwapokea watu hawa kama zawadi. Tusiwaone kana
kwamba ni tishio kwetu. Mara nyingi huwa tunaanza kupambana na kuwapiga vita na
mwishowe tunaishia kupoteza. Lakini tukiwakubali, nakwambia huwa wanatusaidia
na sisi kungaa. Wengi wetu ni maskini kwa sababu tumepambana na waliobarikiwa,
kupingana nao bila sababu, kushindana badala ya kuwafanya watusaidie watufanye
tungae.Tumeishia kuwaonea wivu na kubakia katika umaskini kila siku.
Katika injili, fundisho
hili linadhihirika rasmi. Wale wanaomkubali mwenye uwezo, wale wanaomkubali
Yesu ndio tunaosikia anawaponya. Wangemkataa Yesu na kuanza kupambana naye,
wasingefika popote. Hivyo, ndugu zangu, tujifunze kuwapokea wale waliopewa
uwezo kwani watatufanya nasi tungare. Ukipambana nao unazidi kuwa maskini
mwenyewe kiroho kwani hutakubali hata kupewa tafakari na mtu fulani kwani
utajiona najua kila kitu. Kubali kipaji na uwezo wa mwenzio na shirikiana naye utashangaa
Mungu naye atakuinua pia.
Copyright ©2013-2026 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment