MASOMO YA MISA, JANUARI 23, 2026
IJUMAA, JUMA LA 2 LA
MWAKA
SOMO 1
1Sam. 24:2-20
Sauli akatwaa watu elfu
waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na wa wake juu ya
majabali ya mbuzi-mwitu. Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko
kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake
walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana. Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama,
hii ndiyo siku ile aliyokuambia Bwana, Angalia, nitamtia adui yako mikononi
mwako, nawe utamtenda yoyote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka,
akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri. Lakini halafu moyo wake Daudi
ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli. Akawaambia watu wake,
Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa Bwana, neno hili, kuunyosha mkono
wangu juu yake, kwa maana yeye ni masihi wa Bwana. Basi Daudi akawazuia watu
wake kwa maneno hayo asiwaache kumwondokea Sauli.
Kisha Sauli akatoka
pangoni, akaenda zake. Daudi naye akainuka baadaye, akatoka pangoni, akamwita
Sauli, akisema, Bwana wangu, mfalme. Na Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama
uso wake hata nchi, akamsujudia. Daudi akamwambia Sauli, Kwa nini unasikiliza
maneno ya watu, wasemao, Tazama Daudi anataka kukudhuru? Tazama, leo hivi macho
yako yameona jinsi Bwana alivyokutia mikononi mwangu pangoni; na watu wengine
wakaniambia nikuue; lakini nikakuacha; nikasema, Sitaki kuunyosha mkono wangu
juu ya bwana wangu; kwa maana yeye ni masihi wa Bwana.
Tena, baba yangu,
tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa
nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu
wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho
yangu ili kuikamata. Bwana atuamue, mimi na wewe, na Bwana anilipizie kisasi
changu kwako; lakini mkono wangu hautakuwa juu yako. Kama vile walivyosema watu
wa kale katika mithali yao, Katika waovu hutoka uovu; ila mkono wangu hautakuwa
juu yako. Na mfalme wa Israeli ametoka ili kuatia nani? Unamwinda nani? Ni
kuwinda mbwa mfu, au kiroboto. Basi Bwana atuamue, akatuhukumu mimi na wewe,
akaone, akanitetee neno langu, akaniokoe na mkono wako.
Ikawa, Daudi
alipokwisha kumwambia sauli maneno hayo, Sauli alisema, Hii ndiyo sauti yako,
daudi mwanangu? Naye Sauli akapaza sauti yake, akalia. Akamwambia Daudi, Wewe u
mwenye haki kuliko mimi; maana wewe umenitendea mema, nami nimekutenda mabaya.
Nawe umeonyesha leo jinsi ulivyonitendea mema; kwani Bwana liponitia mikononi
mwako, hukuniua. Maana mtu akimwona adui yake, je! Atamwacha aende zake salama?
Basi Bwana na akulipe mema kwa haya uliyonitendea leo. Na sasa, angalia, najua
ya kuwa hakika utakuwa mfalme, na ufalme wa Israeli utafanyika imara mkononi
mwako.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 57:1-3, 5 (K) 1
(K) Unirehemu, Ee
Mungu, unirehemu mimi
Unirehemu, ee Mungu,
unirehemu mimi,
Maana nafsi yangu
imekukimbilia Wewe.
Nitaukimbilia uvuli wa
mbawa zako,
Hata misiba hii
itakapopita. (K)
Nitamwita Mungu aliye
juu,
Mungu anitimiziaye
mambo yangu.
Atapeleka toka mbinguni
na kuniokoa,
atukanapo yule
atakayenimeza.
Mungu atazaipeleka
fadhili zake na kweli yake. (K)
Ee Mungu, utukuzwe juu
ya mbingu,
Na juu ya nchi yote uwe
utukufu wako. (K)
SHANGILIO
2Kor. 5:19
Aleluya, aleluya,
Mungu alikuwa ndani ya
Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, naye ametia ndani yetu neno la
upatanisho.
Aleluya.
INJILI
Mk. 3:13-19
Yesu alipanda mlimani,
akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate
kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.
Akawaweka wale Thenashara; na Simoni akampa jina la Petro; na Yakobo, mwana wa
Zebedayo, na Yohane nduguye Yakobo, akawapa jina la Boanerge, maana yake, wana
wa ngurumo; na Andrea, na Filipo, na Bartholomayo, na Mathayo, na Tomaso, na
Yakobo wa Alfayo, na Thadayo, na Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, ndiye
aliyemsaliti.
Neno la Bwana… Sifa
kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright
© 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora
– Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment