MASOMO YA MISA, JANUARI 22, 2026
ALHAMISI, JUMA LA 2 LA
MWAKA
SOMO 1
1Sam. 18:6-9; 19:1-7
Walipokuwa wakienda,
hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika
miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka
na matari, na shangwe, na vinanda.
Nao wale wanawake
wakitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, na Daudi makumi elfu
yake. Basi Sauli akagadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema,
Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elf utu; kuna nini tena awezayo
kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.
Kisha Sauli akasema na
mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi. Lakini
huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na DAudi. Basi
Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi,
nakusihi, uiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha; na mimi
nitatoka nje na kusimama kando ya babangu huko shambani ulipo wewe, nami
nitazungumza na babangu habari zako; nami nikiona neno lolote nitakuambia.
Naye Yonathani akamsifu
Daudi kwa Sauli, babaye, akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake,
yaani, juu ya Daudi; kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako
yamekuwa mema sana. Kwa kuwa alitia uhai wake mkononi mwake, na kumpiga yule
Mfilisti, naye Bwana akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona
jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue
huyo Daudi bure?
Sauli akaisikiliza
sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo Bwana, yeye hatauawa. Basi
Yonathani akamwita Daudi aje, Yonathani akamjulisha mambo hayo yote. Kisha
Yonathani akamleta kwa Sauli, naye alikuwa akihudhuria mbele yake, kama kwanza.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 56:1-2, 8-12 (K) 4
(K) Nimemtumaini Mungu
sitaogopa.
Mungu, unirehemu, maana
yuko atakaye kunimeza,
Mchana kutwa ananionea
akileta vita.
Adui zangu wanataka
kunimeza mchana kutwa,
Maana waletao vita
yangu kwa kiburi ni wengi,
Ee Mungu wangu. (K)
Umehesabu kutangatanga
kwangu,
Uyatie machozi yangu
katika chupa yako,
Je! Hayamo katika
kitabu chako?
Ndipo adui zangu
watarudi nyuma,
Siku hiyo niitapo. (K)
Neno hili najua kuwa
Mungu yu upande wangu.
Kwa msaada wa Mungu
nitalisifu neno lake,
Kwa msaada wa Bwana
nitalisifu neno lake. (K)
Nimemtumaini Mungu,
Sitaogopa mwanadamu
atanitenda nini?
Ee Mungu, nadhiri zako
zi juu yangu,
Nitakutolea dhabihu za
kushukuru (K)
SHANGILIO
Zab. 119:135
Aleluya, aleluya,
Umwangazie mtumishi
wako uso wako, na kunifundisha amri zako.
Aleluya.
INJILI
Mk. 3:7-12
Yesu alijitenga, yeye
na wanafunzi wake, akaenda baharini. Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka Galilaya,
na Uyahudi, na Yerusalemu, na Idumaya, na ng’ambo ya Yordani, na pande za Tiro
na Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda,
wakamwendea. Akawaambia wanafunzi wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu
naye, kwa sababu ya mkutano, wasije wakamsonga. Maana aliponya wengi, hata wote
waliokuwa na misiba wakamrukia wapate kumgusa. Na pepo wachafu, kila
walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa
Mungu. Akawakataza sana, wasimdhihirishe.
Neno la Bwana… Sifa
kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright
© 2026, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora
– Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment