Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA DESEMBA 3, 2021

 

MASOMO YA MISA DESEMBA 3, 2021

IJUMMA, JUMA LA 1 LA MAJILIO

 

SOMO 1

Isa. 29:17-24

 

Bwana Mungu asema: Je! Si muda mdogo uliobaki, na Lebanoni itageuzwa kuwa shamba lizaalo sana, na lile shamba lizaalo sana litahesabiwa kuwa msitu? Na katika siku hiyo viziwi watasikia maneno ya hicho chuo, na macho ya vipofu yataona katika upofu na katika giza. Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli. Kwa maana mwenye kutisha ameangamizwa, naye mwenye dharau amekoma, nao wote watazamiao uovu wamekatiliwa mbali; hao wamfanyao mtu kuwa amekosa katika neno, na kumtegea mtego yeye aonyaye langoni, na kumgeuza mwenye haki kwa kitu kisichofaa.

Basi, Bwana aliyemkomboa Ibrahimu asema hivi, katika habari za nyumba ya Yakobo; Yakobo hatatahayarika sasa, wala uso wake hautabadilika rangi yake. Basi atakapowaona watoto wake, walio kazi ya mikono yangu, katikati yake, wao watalitakasa jina langu; naam, watamtakasa Mtakatifu wa Yakobo, nao watamcha Mungu wa Israeli. Hao nao wakosao rohoni mwao watapata kufahamu, na hao wanung’unikao watalifunza elimu.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 27:1,4,13-14 (K) 1

 

(K) Bwana ni nuru ya wokovu wangu.

 

Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,

Nimwogope nani?

Bwana ni ngome ya uzima wangu,

Nimhofu nani? (K)

 

Neno moja nimelitaka kwa Bwana,

Nalo ndilo nitakalolitafuta,

Nikae nyumbani kwa Bwana,

Siku zote za maisha yangu.

Niutazame uzuri wa Bwana,

Na kutafakari hekaluni mwake. (K)

 

Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana,

Katika nchi ya walio hai.

Umngoje Bwana, uwe hodari,

Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)

 

SHANGILIO

 

Aleluya, aleluya,

Tazama Bwana wetu atakuja na nguvu, Na atayaangaza macho ya watumishi wake.

Aleluya.

 

INJILI

Mt. 9:27-31

 

Siku ile: Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana. Ndipo alipowagusa macho yao yakafumbuka. Naye Yesu akawaagiza kwa nguvu, akisema, Angalieni hata mtu mmoja asijue. Lakini wakatoka, wakaeneza habari zake katika nchi ile yote.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.

Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

No comments:

Post a Comment