“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya Kila siku
Jumatano,
Novemba 3, 2021.
Juma
la 31 la Mwaka
Rom
13: 8-10;
Zab
112: 1-2, 4-5, 9 (K) 5;
Lk
14: 25-33.
GHARAMA
YA KUWA MFUASI!
Karibuni
ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana
asubuhi ya leo linaendeleza kile tulichoanza kusikia siku ya jana kwamba mwaka
wa kanisa unaelekea ukingoni na masomo tunayoanza kuyasikia hasa somo la injili
ni kuhusu nyakati za mwisho na maandalizi yetu kwa maisha ya baadaye. Katika
injili hii, Yesu anaweka dhahiri juu ya kinachohitajika kwa yeyote yule
anayetaka kuwa mfuasi wa Yesu-ni lazima ajikane nafsi yake achukue msalaba wake
na kumfuata. Anayetaka kuwa mfuasi wa Yesu lazima akubali hata kumchukia baba
yake na mama yake na hata nafsi yake. Ni lazima ukae chini na upime je kweli
nitaweza?
Ndugu
zangu, Yesu anatumia maneno yote haya tena yakiwa ni makali kabisa, yanachoma
sana na kwa baadhi yetu tunaweza kufikiri kwamba yanakwaza kuonyesha jinsi
ilivyo makini kumfuata Yesu. Itakubidi upingane na mitindo mbalimbali na
kasumba mbalimbali na hata mila na desturi mbalimbali za kabila lako, familia
yako na wenzako. Itakubidi ubakie siku zote ukitetea ukweli wa injili na hapa
ndipo kasheshe itaanza, nakwambia utagombana na baba, ndugu, na hata watu wa
kabila lako.
Kwa
mfano, kwa ukristo itakulazimu uwe na mke mmoja-hii kwa baadhi ya makabila
hutaeleweka, itakubidi uache mila kama kuridhi mke wa kaka yako na kuzaa
naye-hapa unaweza usieleweke kabisa, itakukataza usipige ramli au kufanya
mazindiko mbalimbali. Nakwambia hapa mtanishuhudia kwani wanaokataa kufanya
mambo haya unakuta familia au ukoo wote unakutenga. Haukuelewi kabisa. Naamini
kuna wale wanakaresmatiki wamekumbana na kitu kama hiki. Kuna sehemu fulani
ukikataa kushiriki katika matambiko au mazindiko yanayofanywa na familia
unatengwa. Na hapa unabii wa Yesu unatimia.
Halafu
nakwambia ukishikilia msimamo wako wa dini hata ukiwa kazini kwako, nakwambia
unashangaa unaona hata baadhi ya watu, wale unaofikiri kuwa ni rafiki zako,
waliokutegemea upige nao dili na wewe usipige, nakwambia wanakutenga.
Hawakualiki kwenye masherehe yao tena, wanakuacha huko, wanakusema, na wewe
kama huna moyo unaweza kwenda kuwaomba msamaha ili uungane nao.
Huu
ndio ukristo ndugu yangu. Kumfuata Yesu, msimamo wako wa kiimani umesababisha
utengwe, uonekane kama nuksi kwa wenzako. Hili ni fundisho kwetu ndugu zangu
ili pale mambo kama haya yakitokea, tusishtuke au kuogopa sana kiasi cha kwenda
kuwaomba msamaha na kujiunga na makundi yao. Wewe bakia na Mungu na pia fuata
kile anachosema Paulo katika somo la kwanza kwamba usiwe na deni jingine kwa
mwenzako isipokuwa kupendana. Wewe bakia katika kuwapenda hata kama
watakuchukia wewe usiwatendee ubaya wowote au kuwalipiza. Jua kwamba Yesu
amewahi kuyatabiri haya na injili ya leo ikutie moyo hasa wakati huu ambapo
kanisa hututafakarisha juu ya ujio wa mwisho wa maisha yetu.
Copyright ©2013-2020 ©FurKat,
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment