MASOMO YA MISA JUNI 2,
2021
JUMATANO, JUMA LA 9 LA
MWAKA
SOMO 1
Tob. 3:1-10, 16-17
Tobiti alisikitika
akalia, na katika huzuni yake aliomba akasema: Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye
haki, na matendo yako yote na njia zako zote ni rehema na kweli, nawe unahukumu
kwa kweli na kwa haki milele.
Unikumbuke, unitazame;
usiniadhibu kwa ajili ya dhambi zangu na makosa yangu; wala kwa ajili ya dhambi
za baba zangu walioasi mbele zako.
Kwa maana hawakuzitii
amri zako; kwa hiyo umetutoa tuwe mateka, hata na kuuawa; kuwa mithali ya
shutumu kwao mataifa yote, ambao kwamba tumetawanyika katikati yao.
Na sasa hukumu zako zi nyingi
na za kweli; hata uje unitende kwa kadiri ya dhambi zangu na za baba zangu; kwa
kuwa hatukuzishika amri zako; wala kuenenda kwa kweli mbele zako. Basi sasa
unitende kama uonavyo vema; uniamuru niondolewe roho yangu, ili niruhusiwe na
kuwa udongo tena; maana yanifaa kufa kuliko kuishi, kwa sababu nimesikia
mashutumu yasiyo haki, nami naona huzuni nyingi.
Uamuru, basi, nitolewe
katika msiba huu, niende mahali pa milele; wala usiugeuzie mbali nami uso wako.
Ikawa siku ile ile huko
ekbatana, mji wa Media, Sara binti Ragueli naye alishutumiwa na wajakazi wa
baba yake. Maana alikuwa ameolewa na waume saba, bali Asmodeo, yule jini,
aliwaua kabla hawajalala naye. Wakamwambia, Wewe hujui ya kuwa umewanyonga
waume zako? Umekuwa na waume saba, wala hata mmoja wao hukupata faida naye.
Mbona waturudia sisi? Ikiwa wao wamekufa, nenda zako nawe ukawafuate; tusikuone
kabisa una mwana wala binti. Alipoyasikia hayo alifanya huzuni nyingi, akaona
afadhali kujinyonga. Akafikiri, Mimi ni binti pekee wa baba yangu; basi nikitenda
hivi nitamwita shutumu; nitamshushia uzee wake kwa huzuni hata kaburini.
Basi ikawa sala zao wote
wawili zilisikiwa mbele za enzi yake Mungu Aliye juu. Rafaeli akatumwa ili
awaponye wote wawili.
Neno la Bwana...
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. Zab. 25:2 – 9 (K) 1
(K) Ee Bwana, nakuinulia
nafsi yangu.
Ee Mungu wangu,
Nimekutumaini Wewe,
nisiaibike,
Adui zangu wasifurahi kwa
kunishinda.
Naam, wakungojao
hawataaibika hata mmoja;
Wataaibika watendao
uhaini bila sababu. (K)
Ee Bwana, unijulishe njia
zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli
yako,
Na kunifundisha.
Maana Wewe ndiwe Mungu wa
wokovu wangu,
Nakungoja Wewe mchana
kutwa. (K)
Ee Bwana, kumbuka rehema
zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea
zamani.
Usiyakumbuke makosa ya
ujana wangu,
Wala maasi yangu.
Unikumbuke kwa kadiri ya
ujana wangu,
Wala maasi yangu.
Unikumbuke kwa kadiri ya
fadhili zako,
Ee Bwana, kwa ajili ya
wema wako. (K)
Bwana yu mwema, mwenye
adili,
Kwa hiyo atawafundisha
wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza
katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha
njia yake. (K)
SHANGILIO
Mt. 11:25
Aleluya, aleluya.
Nakushukuru Baba, Bwana
wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili,
ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.
INJILI
Mk. 12:18-27
Masadukayo, watu wasemao
ya kwamba hakuna kiyama, walimwendea Yesu, wakamwuliza na kusema, Mwalimu, Musa
alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto,
ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao. Basi kulikuwa na ndugu
saba; wa kwanza akatwaa mke, akafa, asiache mzao. Wa pili naye akamtwaa akafa,
wala yeye hakuacha mzao. Na wa tatu kadhalika; hata na wote saba, wasiache mzao.
Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama atakuwa mke wa
yupi katika hao? Maana wote saba walikuwa naye.
Yesu akajibu, akawaambia,
Je! hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu?
Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama
malaika walioko mbinguni. Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma
katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema,
Mimi ni Mungu wa Ibrahi- mu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Yeye si
Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment