“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya Kwaresima
Jumatatu,
Februari 22, 2021.
Juma
la 1 la Kwaresima
Law
19: 1-2, 11-18;
Zab
19: 8-10, 15;
Mt
25: 31- 46
NI
NANI NDUGU YANGU ALIYE MDOGO?
Karibuni
ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana
tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza toka katika kitabu cha Walawi ambapo
tunamkuta Mungu akiwakumbusha wana wa Israeli kwamba Mungu wao ni mtakatifu na
hivyo wajitahidi ili wahakikishe kwamba na wao wanakuwa watakatifu. Ni kwa
namna hii tu ndio watakapoweza kuungana na Mungu na kumfikia kama wanadamu na
taifa teule la Bwana Mungu wetu.
Hivyo,
Mwenyezi Mungu anawaeleza kwamba lazima wazishike amri-amri zitakazowafanya
kuwa watakatifu. Amri hizi zinasisitiza juu ya kumpa Mungu nafasi ya kwanza
kuliko vitu vyote-kuepuka kuabudu miungu mingine. Hilo ndilo linalosisitiziwa.
Halafu, zinatuambia pia tuwaheshimu binadamu wenzetu tunaoishi nao hapa
duniani. Tuwaone kama viumbe viteule vya Mungu na hivyo tusiwaonea bali
tuwaheshimu na kuwapatia heshima zao. Namna hii tutaweza kuwa watakatifu na kwa
huu ndio wito tulioitiwa na Mungu ndugu zangu.
Hivyo,
duniani hatuwezi kuishi kirahisi kirahisi tu. Lazima tuwe na majukumu ya
kutekeleza, lazima tujitoe sadaka ili kumpendeza Mungu na wenzetu wapate
kuishi. Mara nyingi wanaoharibu ni wale wanaopendelea mambo yawe kirahisi
rahisi tu, tusibanwe banwe sana, mambo yaende tu, nifanye mambo yangu. Watu
wengi wanataka hivyo na watu wa namna hii huwa wabinafsi na hawa ndio
wanaoiletea dunia matatizo.
Ndugu
zangu, unapokiuka na kukataa kuishi amri ya Bwana, unamuumiza mwenzako na Mungu
pia. Hili tumelisikia katika injili ya leo. Unamfanya mwenzako akose chakula,
afungwe gerezani kwa dhuluma, akose hata nguo ya kuvaa na wagonjwa wafe kwa
kukosa dawa. Mfano. Angalia rushwa zinavyowafanya watu wasisome, au uzembe
wangu daktari umewaua wangapi au mimi hakimu mla rushwa nimewafunga wangapi
bila hatia au mimi mzazi nisiyetimiza wajibu wangu nimewafanya watoto wangu na
mke wangu wateseke namna gani. Yote haya ni kukosa kutimiza amri ya Mungu.
Na
katika injili yetu atatuhukumu kwa kututupa katika tanuru ya moto kwani matendo
yetu yamewaumiza wengi na wenzetu wanapoumia wanamlilia na wakimlilia Mungu
anajibu kama tulivyosikia katika injili.
Hivyo,
ndugu zangu, kabla ya kufanya tendo lolote tuchunguze hasara zake kwetu na kwa
wenzetu. Kama unataka kupokea rushwa jaribu kuangalia ni watu wangapi
wanateseka kutokana na wewe kufanya hivyo, kama ni hakimu mla rushwa au daktari
mzembe au mzazi mzembe, askari mla rushwa, dereva asiyejali-angalia ni watu
wangapi wanaumia kutokana na uzembe wako. Angalia laana inayokuelekea kutokana
na kilio cha hao watu, kutokana na uzembe wako, angalia pia kilio cha watoto
wao watakapokuwa wanakulaani. Tumuombe Mungu tutafute utakatifu zaidi ili
tupate kustahilishwa kumuona Mtakatifu mwenyewe.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment