“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatano,
Oktoba 21, 2020,
Juma
la 29 la Mwaka wa Kanisa
Ef
3:2-12;
Is
12:2-6;
Lk
12:39-48
UFUASI:
WITO WA KUWA MWAMINIFU, SI KWAAJILI YA MAFANIKIO!
Karibuni
ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Bwana katika adhimisho la Misa Takatifu
asubuhi ya leo. Leo basi tafakari yetu inaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya
wimbo wa katikati ambapo tunakutana na mzaburi akishangilia kwamba kwa furaha
tutateka maji katika kisima cha wokovu. Hii ni sababu yake yeye kushangilia.
Mzaburi anadiriki kusema hayo yote kwasababu anaona kwamba neema zote na baraka
anazopokea Israeli ni upendeleo wa pekee. Mara nyingi Israeli amekuwa mkaidi
lakini Mungu alizidi kumpatia neema. Hivyo basi Mzaburi anakiri kwamba
atahakikisha kwamba kila siku atamtukuza Mungu kila wakati na sifa zake
zitabakia kinywani mwake daima.
Zaburi
hii inatuunganisha vyema na somo la kwanza. Leo Paulo anasema kwamba hata yeye
na Waefeso wote wamepata baraka na upendeleo wa kufunuliwa siri ya Bwana-siri
ya kwamba Kristo ndiye anayewaokoa wote na hivyo wamwamini Kristo wapate
wokovu. Huyu Kristo aliwakomboa kwa kumwaga damu yake msalabani. Kila
anayemkiri Yesu kuwa ni mwana wa Mungu atapata wokovu. Kristo ameondoa uadui
kati ya makabila, rangi, tabaka na elimu zetu. Hii ni siri kuu ambayo basi
wengi hawakuifahamu na hii ilifunuliwa kwa wale walioiamini injili tu. Paulo
anawaeleza Waefeso kwamba wanayokila sababu ya kumshukuru Mungu kwa wao
kufunuliwa matendo makuu na siri kuu namna hii kwani wengi hawaijui. Wao
wamshukuru Mungu. Ni upendeleo wa karibu.
Somo
hili ni mwaliko kwetu ndugu zangu wa kutambua kwamba hata sisi tayari
tumebarikiwa na Bwana vya kutosha. Baadhi mwanzoni tulikuwa maskini kabisa
lakini sasa Mungu ametusaidia kupandisha kipato chetu. Wengine tulikuwa
tunaburutwa kwenye masomo lakini sasa basi Mungu ametuweka juu. Wengine
tumepandishwa vyeo na sasa ni watu wakubwa kabisa. Tunapaswa kumshukuru Mungu
kwa hili ndugu zangu. Tuone kama nafasi ya upendeleo, tusijivune bali
tushirikishane na wengine hizi neema za mwenyezi Mungu.
Katika
injili Yesu anazungumzia ujio wa nyakati za mwisho na anasisitiza kwamba siku
hiyo itakuwa ni siku ya watu kutoa hesabu. Kuna wale waliokabidhiwa mengi na
hivyo watadaiwa mengi toka kwao pia. Sisi ndugu zangu tujiangalie ni mangapi
tumekabidhiwa? Namna gani tumetumia kwenye kuwasaidia wenzetu au kuwatesa.
Tusitumie ujuzi wetu au cheo au pesa au maarifa kwenye kuwadanganya wenzetu.
Wengi tumetumia maarifa yetu kuwadanganya wenzetu, tumetumia mbinu kuwaibia
fedha zao au kushinda kesi kwa ujanja wetu na kuishia kuwadhulumu. Hapa
tutadaiwa mengi.
Tusiwadanganye
walio wadogo. Wasiojua lugha au kisomo tusiwatafsirie vitu vya uongo. Huku
ndiko kukesha atakakotukuta Yesu tukiwa tayari kumlaki na yeye atatuhudumia na
kutupatia nafasi ya pekee katika ufalme wake.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment