Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, MEI 14, 2024



MASOMO YA MISA, MEI 14, 2024
JUMANNE YA 7 YA PASAKA
SIKUKUU YA MT. MATHIA, MTUME


SOMO 1
Mdo. 1:15-17, 20-26

Siku zile Petro alisimama kati ya ndugu zake (jumala ya majina ilipata mia na ishirini), akasema, Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi. katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu, kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii. Kwa maana imeandikwa katika chuo cha Zaburi, Kikao chake na kiwe ukiwa,

Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo; tena, Usimamizi wake autwae mwingine. Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo wa Yohane, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi.

Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya. Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe. Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.


W1MBO WA KATI KATI 
Zab. 113:1-8 (K) 8

(K) Amketishe pamoja na wakuu, pamoja na wakuu wa watu wake. au: Aleluya.

Aleluya.
Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
Lisifuni jina la Bwana.
Jina la Bwana lihimidiwe 
Tangu leo na hata milele. (K)

Toka maawio ya jua hata machweo yake 
Jina la Bwana husifiwa.
Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote,
Na utukufu wake ni juu ya mbingu. (K)

Ni nani aliye mfano wa Bwana,
Mungu wetu aketiye juu;
Anyenyekeaye kutazama,
Mbinguni na duniani? (K)

Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Na kumpandisha maskini kutoka jaani.
Amketishe pamoja na wakuu,
Pamoja na wakuu wa watu wake. (K)


SHANGILIO 
Yn. 15 :16

Aleluya, aleluya, Ni mimi niliyewachagua ninyi, nikawaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kukaa. Aleluya.


INJILI 
Yn. 15:9-17

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.

Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.


Neno la Bwana.........sifa kwako Ee Kristo. 

Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment