Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

WAKRISTO WENYE KUTOA USHUHUDA!



“KUFUFUKA NA KRISTO”
Tafakari ya Pasaka
Jumatatu, Mei 13, 2024.
Juma la 7 la Pasaka

Mdo 19: 1-8;
Zab 67: 2-7 (R. 33);
Yn 16: 29-33.


WAKRISTO WENYE KUTOA USHUHUDA!


Ni rahisi kuwa mkristu na kumfuata Yesu wakati ukiwa na watu wengi na wakati wengine wakifanya hivyo. Lakini je, inakuwaje kuhusu wakati ambapo Imani yako inapo vamiwa au inazuiwa na kupingwa? Au wakati ambapo inakubidi kufanya uchaguzi wa kutoka katika utamaduni mbaya uliozoeleka na jamii yako na kusimama kwenye Imani yako? Kuna changamoto nyingi katika ufuasi wetu wa kumfuata Kristo. Katika Injili ya leo kuna watu ambao walikuwa wakiongelea mafundisho ya Yesu wakimsikiliza na kuongea kuhusu yeye. Wengi waliishia pia kuamini alikuwa Masiha. Walimsikiliza na kumwamini kwamba alitoka kwa Mungu. Yesu aliwongelea hao mara moja na kwamba ingawaje wanaamini sasa, kutakuwa na muda ambapo watamkataa na kumwacha peke yake. Moja ya jaribio kubwa la Imani yetu ni kuangalia ni kwa jinsi ghani tulivyo waaminifu katika Imani yetu tunapo mfuata Yesu bila kuwa na umati. Ni katika wakati huu, tunakuwa na muda wa kudhihirisha Imani yetu na kuzamisha maana yetu ya kuwa Wakristo.

Siku hizi tunaongea mara nyingi juu ya “uinjilishaji mpya” . Uinjilishaji huu hauwezi kufanya kazi tu kwa njia ya vyombo vya habari. Watu hawataguswa na maneno yetu: kwa njia ya tweeter, kuandika ujumbe, redio wala katika websites, bali ni njia ya mwanadamu kwa mwanadamu kushuhudia nguvu ya Roho ambayo itabadili maisha yetu na tabia zetu kama vile Roho alivyo mbadili Paulo kutoka katika hali ya kulitesa kanisa na kuwa mtangazaji mkubwa wa habari njema. Watu wa siku hizi na hasa wale waliyo batizwa na wameamua kuliacha kanisa wana hangaika kutafuta ishara ya Roho wa Mungu. Kama tunataka watu wasikilize habari njema, tunapaswa kufanywa upya na Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Fransisko alipendekeza kwamba wengi wetu tunaogopa kufanya mabadiliko, kwasababu hatuweze kukaa na Roho-kwasababu Roho anaweza kutupeleka sehemu ambayo hatupendi kwenda, kwa mtu binafsi na hata kwa pamoja. Tumuombe Mungu atujaze upya Roho Mtakatifu na tumruhusu Roho Mtakatifu atupe changamoto!

Sala: Bwana, naamini. Nisaidie Imani hiyo juu yako ibaki imara daima. Yesu, nakuamini wewe. Ee Roho Mtakatifu wa mapendo, shuka kwangu ili niweze kushuhudia ukweli wako. Roho Mtakatifu, nakuamini wewe. Amina.


Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment