MASOMO YA MISA, MEI 13, 2024
JUMATATU, JUMA LA 7 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 19:1-8
Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha
kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa
kadha huko; akawauliza, Je! mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La,
hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, basi
mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, kwa ubatizo wa Yohane. Paulo akasema,
Yohane alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye
atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.
Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana
Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja
juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri. Na jumla yao walipata wanaume
kumi na wawili. Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa
miezi mitatu, akahojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATI KATI
Zab. 68 :1-6 (K) 32
(K) Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu. au:
Aleluya.
Mungu huondoka, adui zake wakatawanyika,
Nao wamchukiao huukimbia uso wake.
Kama moshi upeperushwavyo,
Ndivyo uwapeperushavyo wao;
Kama nta iyeyukavyo mbele ya moto,
Ndivyo waovu wapoteavyo usoni pa Mungu. (K)
Bali wenye haki hufurahi,
Na kuushangilia uso wa Mungu,
Naam, hupiga kelele kwa furaha.
Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake,
Shangilieni mbele zake. (K)
Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane,
Mungu katika kao lake takatifu.
Mungu huwakalisha wapweke nyumbani;
Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa;
Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu. (K)
SHANG1LIO
Mt. 28 :19, 20
Aleluya, aleluya,
Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa
wanafunzi, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari.
Aleluya.
INJILI
Yn. 16:29-33
Wanafunzi walimwambia Yesu: Tazama, sasa wasema
waziwazi, wala huneni mithali yo yote. Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo
yote wala huna haja ya mtu akuulize; kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa
Mungu.
Yesu akawajibu, Je! mnasadiki sasa? Tazama. saa
yaja, naam, imekwisha kuja ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na
kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo
pamoja nami. Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni
mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment