“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumanne, Novemba 7, 2023
Juma la 31 la Mwaka
Rom 12: 5-16;
Zab 131: 1-3 (K) 3;
Lk 14: 15-24.
MAJUKUMU YA KIKRISTO!
Leo somo la kwanza kutoka katika barua ya Mtume Paulo kwa Warumi, inalenga
juu ya uhusiano wetu na waamini wengine. Paulo alikuwa anawaandikia Wakristo
waliokuwa wa kanisa la Roma. Kwetu sisi uhusiano wetu ni sawa na uhusiano wa
viungo vya mwili. Kama vile viungo vya mwili vinavyo fanya kazi kwa ushirikiano
na kwa umoja, sisi pia ni jumuiya ambayo tunapaswa kukaa na kutenda kwa umoja.
Ukuwaji wetu wa ndani unategemea sana jinsi tunavyo fanya kazi pamoja, tukiwa
na mtazamo wa Kikristo kwa utukufu mkuu wa Mungu.
Kwa kufanya hili, tunapaswa kufahamu vitu vitatu vinavyo jenga uhusiano na
huduma katika jumuiya ili kujenga mwili wa Kristo: cha kwanza uelewa wa mtu
binafsi: kila Mkristo anapaswa kufahamu vipaji vyake alivyopewa na Mungu ili
kujenga jumuiya na kanisa kwa ujumla. Hili halina maana ya kujifikiria mwenyewe
na kukandamiza vipaji vya wengine. Hili lina maana kutambua pia vipaji vya
wengine na mapaji ya wengine katika jumuiya ili jumiya iweze kujengwa katika
fadhila za Kikristo, Imani, matumaini na Mapendo.
Pili: umoja na ushirikiano: kila mkristo anapaswa kuonesha vipaji vyake kwa
Imani. Tunaweza tusione matunda mara moja, lakini Mungu anayaona na
anayabariki. Mapaji yetu yanapaswa kuletwa pamoja ili kujenga uzuri wa kanisa
zima, hili linawezekana tu kwa umoja na kushirikiana katika kweli.
Tatu, uaminifu na ukarimu. Kwa uzuri wa mwili wa Kristo, damu katika mwili
huo inapaswa kuwa mapendo na uaminifu. upendo unasaidia viungo vyote/watu wote
wafanye kazi kwa umoja. Upendo huu unapaswa kuwa wa kweli sio unafiki.
Katika Injili tunaona wageni walio alikwa walikuwa wamejifunga na mambo yao
binafsi, hawakuchukulia mwaliko huu kwa makini, wakitoa sababu za kuwa na vitu,
familia na mahusiano binafsi. Sisi pia katika majukumu yetu katika kanisa
kujenga mwili huu wa Yesu, huwa tunasababu mbali mbali, mahusiano yetu, mambo
yetu binafsi hata tunakataa mwaliko wa Yesu. Leo tunaitwa tuweze kuangalia
mambo machache: je, nimetumia kipaji nilicho pewa na Mungu kwa ajili ya Mungu?
Je, nimechangia katika kujenga mwili wa Yesu? Je, nimekuwa mtu wa kutoa
visingizio na sababu mbali mbali wakati nikiwa nimeitwa kwa majukumu ya kanisa?
Je nipo tayari kufanya mabadiliko katika maisha yangu ili niweze kuwa kiungo
kinacho fanya kazi pamoja na wengine katika mwili wa Yesu?
Sala: Bwana Yesu, nisaidie mimi niweze kusikia njia mbali mbali unazoniita
mimi niweze kushiriki katika maisha ya neema na huruma. Nisaidie niweze
kutambua daima karamu ulioniandalia na daima niweze kuweka lengo hilo kuwa la
kwanza kabisa. Yesu nakuamini wewe. Amina
No comments:
Post a Comment