MASOMO YA MISA, MEI 21, 2023
DOMINIKA YA 7 YA PASAKA
SHEREHE YA KUPAA BWANA
MWANZO:
Mdo. 1:11
Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama
mbinguni? Atakuja vivyo hivyo mlivyomwona akienda zake mbinguni, Aleluya.
SOMO 1
Mdo. 1:1-11
Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, Theofilo,
katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha, hata siku ile
alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale
mitume aliowachagua; wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi,
baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na
kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu. Hata alipokuwa amekutana nao
aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia
habari zake kwangu; ya kwamba Yohane alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa
katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache.
Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je!
Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi
yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.
Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa
mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata
mwisho wa nchi.
Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama,
akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho
mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu
nao, wenye nguo nyeupe, wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama
mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni,
atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 47 : 1-2, 5-6, 7-8, (K) 5
(K) Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana
kwa sauti ya baragumu. au: Aleluya
Enyi watu wote, pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe,
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote. (K)
Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Mwimbieni Mungu, naam, imbeni;
Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni. (K)
Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote,
Imbeni kwa akili.
Mungu awamiliki mataifa,
Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu. (K)
SOMO 2
Efe 1 : 17-23
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa
utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya
mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa
utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa
uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za
uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono
wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na
mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni
humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake,
akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili
wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Mt. 28:19-20
Aleluya, aleluya,
Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa
wanafunzi, na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote.
Aleluya.
INJILI
Mt. 28:16-20
Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya
mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi
yao waliona shaka. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawambia, Nimepewa mamlaka
yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na
Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi;
na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment