Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, FEBRUARI 21, 2024


MASOMO YA MISA, FEBRUARI 21, 2024
JUMATANO, JUMA  LA 1 LA KWARESIMA


SOMO 1
Yon. 3:1-10

Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukaihubiri habari nitakayokuamuru.

Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikiuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu, Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.

Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema. Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng’ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili tusiangamizwe?

Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 51:1-2, 10-11, 16-17 (K) 17

(K) Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.

Ee Mungu, unirehemu,
Sawa na fadhili wako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu. (K)

Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)

Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,
Moyo uliyovunjika na kupondeka. (K)


SHANGILIO
Eze. 18:31

Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosea, Asema Bwana. Jifanyeni moyo mpya na roho mpya.



INJILI
Lk. 11:29-32

Makutano walipokuwa wakimkusanyikia, Yesu alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka nchi za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

1 comment: