MASOMO YA MISA, MACHI 5, 2023
JUMAPILI YA 2 YA KWARESIMA
SOMO 1
Mwa. 12:1 – 4a
Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi
yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi
nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na
kulitukuza jina lako; nawe uwe Baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye
akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.
Basi Abramu akaenda, kama Bwana alivyomwamuru.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 33:4 – 5, 18 – 20, 22 (K) 22
(K) Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe.
Kama vile tulivyokungoja Wewe.
Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)
Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)
Nafsi zetu zinamngoja Bwana;
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe. (K)
SOMO 2
2Tim. 1:8b – 10
Uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili,
kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si
kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema
yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele, na sasa
inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili
mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Mt. 17:5
Sauti ya Baba ilitoka katika wingu jeupe: “Huyu
ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.”
INJILI
Mt. 17:1 – 9
Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohane
nduguye, akawaleta juu yam lima mrefu faraghani; akageuka sura yake mbele yao;
uso wake ukang’aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Na tazama,
wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye.
Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri
sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na
kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.
Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe
likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni
Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye. Na wale wanafunzi
waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana.
Yesu akaja, akawagusa, akasema, Inukeni, wala
msiogope. Wakainua macho mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu
yeyote habari ya maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment