
“KWARESIMA YA UKARIMU”
Jumamosi, Machi 15, 2025,
Juma la 1 la Kwaresima
Kumb 26: 16-19;
Zab 119: 1-2, 4-5, 7-8;
Mt 5: 43-48
KUTAMANI KUWA MKAMILIFU!
Liturujia ya leo inalenga katika Sheria ya Mungu, ambayo Mungu
ametupa kwa njia ya Musa ili kuifuata kwa moyo na nafsi nzima. Katika Injili,
tunaona Yesu, analeta upendo wenye athari kubwa, zaidi kuliko wowote ule ambao
waliutenda kabla. Kumpenda kila mtu, bila kuwa na fikra au sababu yeyote ile,
bila kujali kama wao wanatupenda sisi au la, bila kufikiria wanatuwazia mabaya
au mazuri?
Yesu wakati alipokuwa dunia hii, alikabiliwa na upinzani sana,
kutoka kwa mamlaka ya kidini, kutoka kwenye mamlaka ya kisiasa, kutoka mji wake
mwenyewe, kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wake mwenyewe. Hata hivyo, yeye
amewapenda daima wote. Ujumbe wake wa huruma au wa kubadilika mara zote ulijawa
na upendo mkuu. Hata juu ya Msalaba, aliwatazama kwa huruma watesi wake. Upendo
kwa Mungu na kwa jirani huenda pamoja, na hauwezi kutenganishwa. Mt. Yohane
anaweka wazi kwamba, “Mtu akisema, “Nampenda Mungu,” naye anamchukia ndugu
yake, ni mwongo (1Yoh 4:20).
Leo tunapewa changamoto na upendo huu wa Yesu Kristo. Tumekuwa
mara nyingi sana watu ambao tunabagua wengine, juu ya rangi, dini, jinsia,
kabila, juu ya tabaka, utaifa, juu ya hadhi ya jamii, utamaduni, elimu, kiasi
cha mali ulicho nacho nk, Je, tunaweza kuamua kumwiga Yesu kuanzia sasa na kuendelea?
Je, tunaweza kuwapenda wale wote ambao wametuumiza katika maisha yetu? Wale
wanaotutesa kwasababu ya utamaduni wetu, dini yetu,au mawazo yetu? Yesu
alishinda haya yote kwa upendo wake, Je, sisi twaweza kufanya hivyo tushinde
kwa njia ya upendo?
Sala: Bwana, ninataka kuwa mtakatifu. Ninataka kuwa mtakatifu kama
wewe ulivyo mtakatifu. Nisaidie niishi kila wakati kwa ajili yako. Ninatoa muda
wangu wote kwa ajili yako. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment