“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Jumamosi, Machi 11, 2023,
Juma la 2 la Kwaresima
Mika 7:14-15,18-20;
Zab 103;1-4, 9-12;
Lk 15: 1-3, 11-32
KUMRUDIA MUNGU!
Katika mfano wa Mwana mpotevu tunaona ujasiri wa huyu Mwana kwa kuchagua
kurudi kwa Baba yake. Ni kweli, alitambua udhaifu wake na akaamua kurudi kwa
Baba yake kuomba msamaha na kumuomba amfanye kama mmoja wa wafanyakazi wake.
Alifanikiwa kurudi.! Swali la kujibu “kwanini?”
Ni vyema kusema kwamba huyu mtoto alirudi kwa Baba yake, kwanza kabisa
kwasababu alitambua kutoka moyoni mwake tabia ya Baba yake. Baba alikuwa Baba
mwema. Alionyesha kujali na kuwa na upendo kwa mtoto daima katika maisha yake.
Ingawaje mtoto alimkimbia Baba yake, haikubadilisha ukweli kwamba yeye
alitambua kuwa Baba yake alikuwa mtu mwema na kwamba anampenda. Pengine
hakutambua ni kwa jinsi ghani, hadi alipo tambua mwenyewe. Ni wazi kwamba ni
kwasababu ya utambuzi huu kutoka moyoni mwake unaompa ujasiri wa kurudi kwa
Baba kwa matumaini ya upendo wa Baba yake.
Hili linafunua kuwa, upendo wa kweli unafanya kazi. Daima unafanya kazi.
Hata kama mtu akikataa upendo mtakatifu tunaompa, lazima daima una ongeza kitu
katika maisha yao. Upendo wa kweli usio na masharti ni vigumu kuukataa na
kuutupilia mbali. Mwana mpotevu alitambua hili, na sisi pia tunapaswa kuwa
hivyo. Huu ndio upendo alionao Baba yetu wa Mbinguni kwa kila mtu. Yeye sio
Mungu mkali na mgumu. Ni Mungu anayependa kuturudisha kwake na kutupatanisha
naye. Anafurahi tunapo mrudia na kuomba mahitaji yetu kwake. Ingawaje tuna wasi
wasi, yeye hana wasi wasi kwa upendo wake, daima anatusubiri sisi, na sisi
wenyewe kutoka ndani kabisa tunatambua hilo.
Kwaresima ni kipindi kizuri sana kwa sakramenti ya kitubio. Na sakramenti
hiyo ndio ujumbe wote katika mfano huu. Ni mfano wa sisi kwenda kwa Baba yetu
na dhambi zetu na atatupokea kwa huruma. Inaweza kuogopesha na kuwa na wasi
wasi kwenda kwenye sakramenti ya kitubio, lakini tukiingia katika sakramenti
hiyo kwa uaminifu na katika kweli, tunaona furaha tunayopata na Amani kuu.
Tunajisikia Amani na kuacha mizigo iliyo tuelemea rohoni. Mungu, anatukimbilia,
na kunyanyua mizigo yetu na kuitupa nyuma yetu. Usikubali kipindi hichi cha
kwaresima kipite bila kuungama! Hakuna na tena, wala hakuna sehemu nyingine
waweza kupata furaha hii ya kuunganika na Mungu katika kweli. Usijioneee huruma
kwa kujibembeleza kwamba nitamweleza tu Mungu mwenyewe nikiwa chumbani kwangu.
Nenda kaungame katika hali ya uaminifu na kweli kadiri ya Imani yetu. Mungu
anakusubiri. Usikubali kubaki katika gereza la dhambi. Fanya uamuzi kama Mwana
mpotevu.
Sala: Baba, nilienda kinyume na wewe na kufuata njia zangu mwenyewe. Sasa
ni muda wa kurudi kwako katika hali ya uwazi na uaminifu wa moyo. Ninaomba
unipe ujasiri huo ili niweze kukumbatia sakaramenti ya kitubio. Yesu nakuamini
wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment