MASOMO YA MISA, MACHI 11, 2023
JUMAMOSI, JUMA 2 LA KWARESIMA
SOMO 1
Mik. 7:14-15, 18-20
Walishe watu wako kwa fimbo yako, kundi la
urithi wako, wakaao peke yao, mwituni katikati ya Karmeli; na walishe katika
Bashani na Gileadi, kama siku za kale. Kama katika siku zile za kutoka kwako
katika nchi ya Misri nitamwonyesha mambo ya ajabu.
Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe
uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira
yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema. Atarejea na kutuhurumia;
atayakanyaga maovu yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi yva
bahari. Wewe utamtimilizia Yakobo kweli yako, na Ibrahimu rehema zako,
ulizowaapia baba zetu tangu siku za kale.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 103:1-4, 9-12 (K) 8
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
Ee nafsi yangu umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote. (K)
Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema. (K)
Yeye hatateta sikuzote,
Wala hatashika hasira yake milele.
Hakututenda sawa na hatia zetu,
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. (K)
Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. (K)
SHANGILIO
Yn. 6:64, 69
Maneno yako, Ee Bwana, ni roho, tena ni uzima;
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
INJILI
Lk. 15:1-3, 11-32
Watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa
wakimkaribia Yesu wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika,
wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao. Akawaambia mfano
huu, akisema,
Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo
akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu
vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri
kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.
Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu
iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji
mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa
akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa
kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu
wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka,
nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele
yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.
Akaondoka, akaenda kwa babaye.
Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona,
akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana
akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana
wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo
bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteeni ndama yule
aliyenona mkamchinje nje; nasi tule na kufurahi; kw akuwa huyu mwanangu alikuwa
amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza
kushangilia.
Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na
lipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo.
Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia,
Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu
amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye
alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema. Tazama, mimi nimekutumikia
miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wowote, lakini hujanipa mimi
mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako
aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.
Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami siku
zote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa,
kwa kuw ahuyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea,
naye ameonekana.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment