Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, MACHI 12, 2023


MASOMO YA MISA, MACHI 12, 2023
JUMAPILI YA 3 YA KWARESIMA


MWANZO:
Zab. 25:15 – 16

Macho yangu humwelekea Bwana daima, naye atanitoa miguu yangu katika wavu. Uniangalie na kunifadhili, maana mimi ni mkiwa na mteswa.



SOMO 1
Kut. 17:3 – 7

Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung’unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu? Musa akamlilia Bwana, akisema, Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe.

Bwana akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende. Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa.

Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli. Akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu au sivyo?

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 95:1 – 2, 6 – 9 (K) 8

(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu.

Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)

Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)

Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ya Masa Jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)



SOMO 2
Ru. 5:1 – 2, 5 – 8

Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika Imani, na tuwe na Amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya Imani kuifikia neema hii ambayo tunasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu.

Na tumanini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyeshe pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.



SHANGILIO
Yn. 4:15

Bwana, hakika wewe ndiwe Mwokozi wa ulimwengu,
unipe maji yale ya uzima, nisione kiu kamwe.



INJILI
Yn. 4:5 – 42

Yesu alifika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu, mwanawe. Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu amechoka kwa safari yake, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita. Akaja mwanamke Msamaria kuteka maji. Yesu akamwambia, Nipe maji ninywe. Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula. Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria).

Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungalijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai.

Yule mwanamke akamwambia, Bana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai? Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?

Yesu akajibu, akamwambia, Kila anyway maji haya ataona kiu tena; walakini yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.

Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka.

Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa. Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume; kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli. Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia. Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu. Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi. Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote. Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye.

Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye? Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akamwambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo? Basi wakatoka mjini, wakamwendea.

Huko nyuma wanafunzi wakamsihi wakisema, Rabi, ule. Akawaambia, Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi. Basi wanafunzi wake wakasemezana, Je! Mtu amemletea chakula? Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Hamsemi ninyi, Bado miezi mine, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja. Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine. Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao.

Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke, aliyeshuhudia kwamba, Aliniambia mambo yote niliyoyatenda. Basi wale Wasamaria walipomwendea, walimsihi akae kwao; naye akakaa huko siku mbili. watu wengi zaidi wakaamini kwa sababu ya neno lake. Wakamwambia yule mwanamke, Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu; maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment