“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumamosi, Januari 28, 2023
Juma la 3 la Mwaka wa Kanisa
Kumbukumbu ya Mt. Tomas wa Akwino, Padre na Mwalimu wa Kanisa
Ebr 11:1-2, 8-19;
Lk 1: 69-75;
Mk 4: 35-41
KUMWAMINI YESU KWA MAISHA YETU!
Bahari na mawimba yana mtii Mungu kwasababu ni sehemu ya uumbaji wake. Na
wala hakuna tatizo kubwa sana kwa Mungu ambalo anashindwa kulitatua. Hofu zetu
hazina mwisho, matatizo yetu yanatusumbua, kwasababu sisi wenyewe tumechagua
kuyakabili wenyewe kwa nguvu zetu. Wafuasi walikuwa ni watu wa kawaida kama
sisi. Hata wakiwa kati ya Yesu wana ogopeshwa na gharika! Laiti kama Mwanadamu
angelijua kukabidhi hofu zake na maumivu yake kwa Mungu!
Ni rahisi sana kukata tamaa katika maisha. Ni rahisi zaidi kuelekeza
mwelekeo wote kwenye matatizo na kuacha mengine yanayo tuzunguka. Hata kama
ingekuwa ni maneno ya hasira na ya kuumiza kutoka kwa wengine, matatizo ya
kifamilia, matatizo ya umma, ukosefu wa fedha nk. Kuna kila sababu ya kila
mmoja wetu kuanguka kwenye mtego wa hofu, kuchanganyikiwa, kuumia na kuwa na
shauku. Lakini ilikuwa ni kwasababu ya sababu hizi Yesu aliruhusu tukio hili
litokee akiwa na wafuasi wake. Alikuwa kwenye boti na wafuasi wake akaruhusu
wafuasi wakumbwe na gharika kuu, wakati yeye akiwa amelala, ili aweze kuleta
ujumbe wa kufaa kwetu sisi wote.
Katika habari hii, wafuasi walilenga kwenye kitu kimoja tuu: walikuwa
waangamie! Bahari ilikuwa ikiwasukasuka na waliogopa maangamizi makubwa! Lakini
kwa kupitia yote hayo, Yesu alikuwa pale akionekana amelala, akiwasubiri waweze
kumwamsha. Na walipo mwamsha, alikemea gharika na hali ikawa shwari. Hili ni
kweli pia katika maisha yetu. Sisi mara nyingi tunaruhusu matatizo mengi
tunayopata yatutese na kutusukasuka. Ufunguo ni kwamba tunapaswa kugeuza macho
yetu na kumwelekea Yesu. Muone mbele yako amelala, anakusubiri umwamshe. Yupo
daima, akikusubiri na yupo tayari daima. Kumwamsha Bwana wetu ni rahisi kama
ilivyo rahisi kugeuza macho yetu kutoka katika gharika na kusadiki uwezo wake
wa Kimungu. Yote ni kuwa na Imani kwake tu. Imani kamili. Je, una mwamini yeye?
Tumwache Yesu achukue nafasi ya kila kitu katika maisha yetu tuliopo.
Anatupenda na kweli atatujali wote.
Sala: Bwana, ninakugeukia katikati ya changamoto za maisha na ninatamani
kukuamsha uje katika maisha na kunisaidia. Ninatambua upo daima karibu yangu,
ukinisubiri mimi nikuamini wewe kwa kila kitu. Nisaidie nielekeze macho yangu
kwako na kuwa na Imani kamili katika mapendo yako. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment