MASOMO YA MISA, JANUARI 29, 2023
DOMINIKA YA 4 YA MWAKA A
MWANZO:
Zab. 106:47
Ee Bwana Mungu wetu, utuokoe, utukusanye kwa
kututoa katika mataifa, tulishukuru jina lako takatifu, tuzifanyie shangwe sifa
zako.
SOMO 1
Sef. 2:3, 3:12 – 13
Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa
dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu;
huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana.
Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na
masikini, nao watalitumainia jina la Bwana. Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu,
wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana
watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya.
Neno la Mungu… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 146:6b – 10 (K) Mt. 5:3
(K) Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa
mbinguni ni wao.
Huishika kweli milele.
Huwafanyia hukumu walioonewa,
Huwapa wenye njaa chakula;
Bwana hufungua waliofungwa. (K)
Bwana huwafumbua macho waliopofuka;
Bwana huwainua walioinama;
Bwana huwapenda wenye haki;
Bwana huwahifadhi wageni. (K)
Huwategemeza yatima na mjane;
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. (K)
SOMO 2
1Kor. 1:26 – 31
Ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si
wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo
walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye
hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye
nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa,
naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye
yote asije akajisifu mbele za Mungu. Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika
Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu,
na ukombozi; kusudi, kama ilivyoandikwa, Yeye aonaye fahari na aone fahari juu
ya Bwana.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Yn. 14:5
Aleluya, aleluya,
Tomaso akamwambia Bwana, Sisi hatujui uendako,
nasi twaijuaje njia?
Aleluya.
INJILI
Mt. 5:1-12
Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na
alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake,
akawafundisha, akisema,
Heri walio maskini war oho; Maana ufalme wa
mbinguni ni wao.
Heri wenye huzuni; maana hao watafarijika.
Heri wenye upole; maana hao watairithi nchi.
Heri wenye njaa na kiu ya haki;
Maana hao watashibishwa.
Heri wenye rehema; maana hao watapata rehema.
Heri wenye moyo safi; maana hao watamwona Mungu.
Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa
Mungu.
Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; maana
ufalme wa mbinguni ni wao.
Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na
kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia;
kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are
a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment