“MBEGU ZA UZIMA”
Tafakari ya kila Jumapili
Jumapili, Januari 29, 2023
Juma la 4 la Mwaka A wa Kanisa
Sef 2: 3; 3: 12-13;
Zab 146: 6-10;
1Kor 1: 26-31;
Mt 5: 1-12.
MAISHA YA FURAHA!
Sisi wote tunapenda kuwa na furaha, na huwa tunajishughulisha kwa hatima hii katika hali mbali mbali. Masomo ya leo yanatuonesha jinsi ya kuwa na maisha ya furaha. Lakini ni kinyume na jinsi tunavyo fikiria. Huwa tunajua kuwa maskini, kuwa mpole na kuonewa haviongozi kwenda kwenye maisha ya furaha. Ila kujiinua kwa ukuu wetu, mafanikio yetu, maisha yanayo zalisha, majivuno yanaongoza kwenye maisha ya furaha.
Katika somo la kwanza tunasikia kuishi katika maisha ya umaskini wa roho maana yake kuishi kwa unyenyekevu itatuongoza kwenda kwenye furaha. Na katika somo la pili tunasikia Mt. Paulo akitujulisha kwamba uchaguzi wa Mungu ni tofauti na uchaguzi wa Mwanadamu wanaofanya. Mungu anachagua wale wanyonge katika jamii na dhaifu mbele ya uso wa Ulimwengu ili kuwanyenyekesha wenye majivuno. Leo katika injili tunamuona Yesu akihutubia mlimani, akitupa njia za kuwa na furaha. Yesu kwa kupitia “heri” anatupa njia sahihi za kuingia kwenye furaha. Zinatuongoza kwanza, katika uhusiano na Mungu na hapo ni Mungu atakaye tubariki ili tuwe na maisha ya furaha. Zinaonesha wazi kwamba sio mwanadamu anaye ongoza kwenye furaha bali ni Mungu na hali zetu kumwelekea yeye.
Katika masomo ya Noeli, Yesu alifunuliwa kama Mwana wa Kifalme wa Daudi na Mwana wa Mungu. Kama Musa alivyowaongoza Waisraeli kupitia bahari ya Shamu na kuwapa sheria ya Mungu katika mlima Sinai, Yesu pia amepita katika maji ya ubatizo na sasa katika Injili, anaenda Mlimani kutangaza sheria mpya- sheria ya ufalme wake. Heri hizi zina ashiria ukamilifu wa Agano la Mungu alilo mwahidia Abrahamu- kwamba kupitia uzao wake mataifa yote yatapokea Baraka za Mungu (Mwa 12:3; 22:18).
Heri hizi sinatufunulia njia ya Kimungu na malengo ya maisha yetu. Kujitahidi kwetu kote kunapaswa kuwa kwa fadhila hizi-kwa maskini wa roho; wanyenyekevu na wenye moyo safi; wenye huruma na watengenezaji wa Amani, watafuta haki inayotoka katika sheria ya Ufalme wa Mungu. Njia ambayo Mungu ameiweka mbele yetu leo ni njia yenye majaribu na mateso. Lakini ana ahidi kutufariji katika huzuni na kutupa thawabu kubwa.
Heri hizi zipo katika mtiririko wa pekee, kuanzia heri ya kwanza ambayo heri maskini wa roho. Ni kwa kuanza kwa kuwa mnyenyekevu mbele ya Mungu na kuruhusu upendo wa Mungu uingie katika maisha yetu. Kwani kwa unyenyekezu wa roho utatufanya tuvumilie yote, kuonewa na kuteswa na kujitahidi katika maisha yetu. Na mwisho wa yote tutapata raha na kuridhika. Mungu amechagua kuwabariki wanyonge na wadogo, wale wanao onekana wajinga na wasiopendwa katika macho ya dunia, kama anavyosema Paulo katika somo la pili. Wale maskini wa roho ni wale wanao fahamu kwamba hawawezi kufanya chochote na kufanikiwa pasipo huruma na neema ya Mungu.
Sisi tupo katika kipindi ambacho tunavutwa sana na raha na kujiridhisha kwa starehe za dunia, kuwa na mali nyingi na mafanikio makubwa. Haya yote yanatupa hali ya shauku kubwa. Lakini ukweli ni kwamba hatujawahi kuridhika na kila kukicha tunatafuta zaidi na zaidi. Tajiri mkubwa, bado anahitaji zaidi, ana kila kitu katika maisha lakini bado hana raha ya maisha. Tumeona maisha ya matajiri wengi katika dunia, hawajawahi kuridhika, daima wanatafuta ili aweze kuwa juu ya wengine na kwa hili hana raha anahangaika daima.
Jumapili iliopita masomo yaliongelea kuhusu wito wetu wa pamoja wa kuwa wafuasi. Tumepewa wito wa kuwa mwanga kwa ulimwengu. Na leo Yesu, anatupa mwanga-maneno ya uzima wa milele. Yesu anatuonesha sisi njia ambayo tunaweza kuiishi sio maneno matupu pekee. Kwasababu yeye mwenyewe aliishi heri zote tangu kuzaliwa mpaka ufufuko wake. Ni njia ya kuelekea kwenye maisha ya furaha ambayo ni maisha ya uzima wa milele. Sio safari rahisi, kwani twaweza kukumbana na umaskini katika maisha, kuumizwa, kuteseka kwa sababu ya haki na kuuonewa. Lakini, ni pale ambapo tutafungua mioyo yetu kwa Yesu tunaweza kupata furaha na kuridhika katika maisha ambayo anatupa sisi kutoka katika upendo wake usio na mwisho.
Heri ni kipimo kamili cha maisha ya furaha na zaidi sana maisha yetu ya Kikristo. Zinatuita kwenda sehemu yenye faraja kamili. Tunapaswa kuwa jasiri na kuwa tayari kwenda kinyume na yale mambo ya wakati huu yanayo pingana na “heri”, tuwe tayari kusema “hapana” kwa maisha ya raha za muda tu na kutupilia mbali tamaduni mbaya, ambazo kwa ukweli zinatupa raha ya muda tu katika maisha.
Sala: Bwana, ninaomba niweze kukumbatia “heri” zote ulizo tupatia sisi. Ninasali, zaidi sana , moyo wangu uweze kukua katika unyenyekevu. Ninaomba ukue katika kuwaonea huruma wanao onewa, wanao umizwa, waliochanganyikiwa na waliobanwa na maisha ya dhambi. Ninakushukuru kwa Baraka unazoendelea kunipa. Yesu, nakuamini wewe. Amina
Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment