MASOMO YA MISA, JANUARI 28, 2023
JUMAMOSI, JUMA LA 3 LA MWAKA
KUMBUKUMBU YA MT. THOMAS WA AKWINO
SOMO 1
Ebr. 11:1 – 2, 8 – 19
Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo,
ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Maana kwa hiyo wazee wetu walishuhudiwa.
Kwa Imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke
aende mahali pale atakapopata kuwa urithi; akatoka asijue aendako. Kwa Imani
alikaa nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi
pamoja naye wa ahadi ile ile. Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi,
ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.
Kwa Imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa
kuwa na mimba, alipokuwa amepita wakati wake, kwa kuwa alimhesabu yeye
aliyeahidi kuwa mwaminifu. Na kwa ajili ya hayo wakazaliwa na mtu mmoja, naye
alikuwa kama mfu, watu wengi kama nyota za mbinguni wingi wao, na kama mchanga
ulio ufuoni, usioweza kuhesabika.
Hawa wote wakafa katika Imani, wasijazipokea
zile ahadi bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba
walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi. Maana hao wasemao maneno kama hayo
waonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. Na kama wangaliikumbuka nchi
ile waliyotoka, wangalipa nafsi ya kurejea. Lakini sasa waitamani nchi iliyo
bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana
amewatengenezea mji.
Kwa Imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka
awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanwe, mzaliwa
pekee; Naam, yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya
kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa
mfano.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Lk. 1:69 – 75 (K) 68
(K) Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,
kwa kuwa
amewajia watu wake.
Ametusimamishia pembe ya wokovu
Katika mlango wa Daudi mtumishi wake.
Kama alivyosema tangu mwanzo
Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu. (K)
Tuokolewe na adui zetu
Na mikononi mwao wote wanaotuchukia:
Ili kuwatendea rehema baba zetu,
Na kulikumbuka agano lake takatifu. (K)
Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu,
Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu,
Na kumwabudu pasipo hofu
Kwa utakatifu na kwa haki
Mbele zake siku zetu zote. (K)
SHANGILIO
Yn. 14:23
Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu,
na baba
yangu atampenda, na sisi tutakuja kwake.
Aleluya.
INJILI
Mk. 4:35-41
Siku ile kulipokuwa jioni, Yesu akawambia, Na
tuvuke mpaka ng’ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika
chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya
upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe
alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu,
si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari,
Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa
waoga? Hamna Imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu,
basi, hata upepo na bahari humtii?
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment