Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, DESEMBA 13, 2022


MASOMO YA MISA, DESEMBA 13, 2022
JUMANNE, JUMA LA 3 LA MAJILIO

KUMBUKUMBU YA MT. LUCIA, BIKIRA NA SHAHIDI


SOMO 1
Sef. 3:1 – 2, 9 – 13

Bwana asema: Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu! Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini Bwana; hakumkaribia Mungu wake.

Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la Bwana, wamtumikie kwa nia moja. Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya kuishi; waniombao dua, yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu.

Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu. Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini nao watalitumainia jina la Bwana. Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uo0ngo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 34:1 – 2, 5 – 6, 16 – 17, 18, 22 (K) 6

(K) Maskini aliita, Bwana akasikia.

Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wafurahi. (K)

Wakamwelekea macho wakati wa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Masikini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)

Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote. (K)

Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake,
Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao. (K)



SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Uje, Bwana, wala usikawie; Uzisamehe dhambi za taifa lako.
Aleluya.



INJILI
Mt. 21:28 – 32

Siku ile, Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee: Mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu. Akajibu akasema, Naenda, Bwana; asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu, akaenda. Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili.

Basi yesu akawaambia, Amin, nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa sababu Yohane alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini; nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment