“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne, Desemba 13, 2022
Juma la 3 la Majilio
Kumbukumbu ya Mtakatifu Lusia Bikira na Mfiadini
Sef 3: 1-2, 9-13;
Zab 34: 2-3, 6-7, 17-19, 23;
Mt 21: 28-32
JE, WEWE NI MDHAMBI?
Somo la leo kutoka katika kitabu cha nabii
Sefania, linatoa onyo na ole kwa wale wanaokataa kusahihishwa, wanaokataa
kusikia, na kuitika wito wa kumwamini Mungu. Katika somo la Injili, Yesu
anasema kwamba ‘Watoza ushuru na wenye dhambi wataingia katika Ufalme wa Mungu
kabla ya viongozi wa dini’. Je, ni kweli kwamba watoza ushuru na wenye dhambi
waliingia katika Ufalme wa Mungu kabla ya viongozi wa dini ya Wayahudi? Je,
Yesu alikuwa anasema kweli kwamba utakatifu wa watoza ushuru na makahaba
ulizidi ule wa viongozi wa dini? Ndio, ilikuwa hivyo kwasababu majivuno
yaliwafanya viongozi wa dini kuwa na moyo mgumu wa kupokea ujumbe wa Ufalme wa
Mungu alioleta Yesu mwenyewe kwa maneno yake. Walifikiri juu ya ukubwa wao sana
na walipenda wengine wawaze juu ya ukubwa wao. Walikuwa wamejiridhisha wenyewe
kwa utakatifu wao wenyewe, nakujiona wema kabisa, jambo ambalo ni mbaya kweli.
Lakini Yesu anayaona yote hayo, na anawanyanyua watoza ushuru na wenye dhambi
kwa utayari wao wakutubu na kumpokea, Yesu anawapandisha kwenye thawabu ya
Ufalme wa Mungu.
Tujitafakari sisi wenyewe kama tunamfanano na
tabia ya viongozi wa dini wa Wayahudi wa kipindi hicho au tuna tabia ya hawa
watoza ushuru na wenye dhambi waliokubali kupokea maneno ya Yesu. Pengine, ni
vigumu kukubali. Pengine tumejitengenezea tabia ya kujitambulisha sisi wenyewe
kama watu wazuri na wasio na kosa na wenye haki. Yesu anataka tujione wenyewe
katika kundi hili la watoza ushuru na wenye dhambi. Hii ni kwasababu sisi wote
ni wadhambi. Tunaweza tusiwe katika hali ya kuumia moyoni kama wao walivyoumia,
lakini ukweli ni kwamba tunaumia kwasababu ya dhambi zetu, tunapaswa kukiri
hili. Na kwakweli, kama tunashindwa kukubali dhambi zetu na madhaifu yetu,
hatuna tofauti na viongozi hawa wa dini ya Kiyahudi. Tutakuwa tumebaki katika
majivuno yetu na kujihesabia haki wenyewe.
Sala: Bwana, jaza moyo wangu kwa unyenyekevu. Na
kwa unyenyekevu, naomba unisaidie niweze kujiona mwenyewe kama nilivyo.
Nisaidie niweze kuona dhambi yangu lakini pia unisaidie kuona juhudi zangu za
kukutafuta. Nisaidie niweze kuacha dhambi zangu nikurudie ili niweze kufurahia
furaha na uhuru wa kuingia katika Ufalme wako. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya
Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment