Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

BWANA AMENITENDEA MAMBO MAKUU, JINA LAKE NI TAKATIFU.


“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Alhamisi, Desemba 8, 2022
Juma la 2 la Majilio


Sherehe ya Bikira Maria Mtakatifu Mkingiwa dhambi wa Asili


Mwa 3:9-15, 20;
Zab 97:1-4;
Efe 1:3-6,11-12;
Lk 1:26-38


BWANA AMENITENDEA MAMBO MAKUU, JINA LAKE NI TAKATIFU.


Kila mtu amezaliwa na dhambi kwasababu ya kushiriki katika dhambi ya Adamu. Lakini katika sehemu zote za maisha kuna neno liitwalo “Upekee”. Hivyo upekee ulitolewa kwa Maria kwasababu alichaguliwa na Bwana kuwa Mama wa Mwanae. Maria hakuzaliwa na hali ya dhambi kama tunayozaliwa nayo sisi. Alikuja ulimwenguni akiwa na uhalisia kamili wa ubinadamu kama ule wa Hawa na Adamu kabla ya kutenda dhambi na kuanguka mbali na neema. Mungu alimpa Maria hali hii kamili ya asili ya ubinadamu sio kwa sababu Maria alifanya kitu kikuu bali kwasababu alikuwa akienda kutenda kitu kikuu. Hivyo wakati wa kupokea kwake mimba kulikuwa ni neema maalumu kutoka kwa Mungu, kisha tokea hapo lilikuwa ni jukumu lake kubakia msafi na bila doa lolote. Hili alilifanya. Sisi sote tumeitwa “kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.” (Efe 1:4).

Utakatifu wa Maria ni matokeo ya neema ya Mungu na utayari wake wa kuwa wazi kwa neema hiyo. Kutokupata dhambi ya asili ni kwasababu ya neema ya Mungu kupitia kwa Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo. Kwahiyo Maria kukingiwa dhambi ya asili sio namna ya kumpa heshima kwa njia yake mwenyewe bali kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo. Kristo kutokuwa na dhambi ni kwasababu ya yeye kuwa nafsi ya pili ya Mungu. Na Maria kutokuwa na dhambi ni kwasababu ya neema ya Mungu pekee na kushirikiana kwake na neema hiyo. Kanisa la kwanza walimheshimu Bikira Maria kwa namna ya pekee kati ya watakatifu wote, kwasababu ya kushiriki kwake katika fumbo la umwilisho wa Mwanae Yesu Kristo na kwasababu ya neema iliotoka katika kushiriki kwake katika fumbo hili.

Neema hiyo hiyo inatolewa kwetu sisi ili tuwe wasafi kupitia damu ya Kristo aliyekufa kwa ajili yetu sisi, lakini je, tumejitoa kama Maria ili tuuishi vema wito wetu?

Sala: Bwana tufanye tuwe wasafi ndani ya mawazo, maneno na matendo yetu. Nisaidie niweze kujenga maisha ya utukufu Mbinguni kwa njia ya kujikabidhi kwenye neema yako. Yesu nakuamini wewe Amina
                                    

Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment