MASOMO YA MISA DESEMBA 8, 2022
ALHAMISI JUMA LA 2 LA MAJILIO
SHEREHE YA BIKIRA MARIA MTAKATIFU, MKINGIWA DHAMBI YA
ASILI
SOMO 1
Mwa. 3:9-15,20
Adamu alipokwisha kula matunda ya mti, Bwana Mungu
alimwita, akamwambia Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini,
naliogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya
kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu
akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti
huo, nikala.
Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya?
Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.
Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo,
umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni;
kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka
uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda
kichwa, na wewe utamponda kisigino.
Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye
aliye mama yao wote walio hai.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98:1-4 (K) 1
(K) Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo
ya ajabu.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)
Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
Miisho yote ya dunia imeuona,
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha. (K)
SOMO 2
Efe. 1:3-6, 11-12
Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo,
aliyetubariki kwa Baraka zote za rohoni, katika ulimwengu war oho, ndani yake
Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya
ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.
Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo,
sawasawa na Uradhi wa mapenzi yake. Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo
ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku
tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo
yote kwa shauri la mapenzi yake. Nasi katika huyo tupate kuwa sifa ya utukufu
wake, sisi tuliotangulia kumwekea Kristo tumaini letu.
SHANGILIO
Lk. 1:28
Aleluya, aleluya,
Salamu, Mariamu, ulipewa neema. Bwana yu pamoja nawe!
Umebarikiwa katika wanawake.
Aleluya.
INJILI
Lk. 1:26-38
Malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa
Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu,
jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu.
Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe.
Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni
ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema
kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake
utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu
atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata
milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.
Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana
hujui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na
nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho
kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako
Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi
huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana
kwa Mungu.
Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe
kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment