Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 18, 2022


MASOMO YA MISA, NOVEMBA 18, 2022
IJUMAA, JUMA LA 33 LA MWAKA WA KANISA

KUTABARUKIWA KWA MABASILIKA YA WATAKATIFU PETRO NA PAULO 

SOMO 1
Ufu. 10:8 – 11

Mimi, Yohane, nilisikia sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi. Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali. Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu. Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 119:14, 24, 72, 103, 111, 131 (K) 103

(K) Mausia yako ni matamu sana kwangu.

Nimeifurahia njia ya shuhuda zako,
Kana kwamba ni mali mengi.
Shuhuda zako ndizo furaha yangu,
Na washauri wangu. (K)

Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
Mausia yako ni matamu sana kwangu,
Kupita asalai kinywani mwangu. (K)

Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele,
Maana ndizo changamko la moyo wangu.
Nalifunua kinywa changu nikatweta,
Maana naliyatamani maagizo yako. (K)


SHANGILIO.
2Kor. 5:19

Aleluya, aleluya,
Mungu alikuwa ndani ya Kristu, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya.


INJILI
Lk. 19:45-48

Yesu aliingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.

Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza; wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment