Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUSAFISHA NA KUTAKASA HEKALU


“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Ijumaa, Novemba 18, 2022 
Juma la 33 la Mwaka wa Kanisa

KUTABARUKIWA KWA MABASILIKA YA WATAKATIFU PETRO NA PAULO 

Mdo 28:11-16,30-31; 
Zab 118:14,24,72,103,111,131; 
Lk 19:45-48


KUSAFISHA NA KUTAKASA HEKALU 

Injili ya leo inaongelea kuhusu kutakasa hekalu la Yerusalemu. Kwa Wayahudi, Hekalu lilikuwa halina cha kufananisha nacho wala kulinganisha, kwasababu Mungu mwenyewe amepachagua kukaa ndani yake. 

Hekalu la kwanza lililojengwa na Mfalme Solomoni mwaka 960 K.B. (1 Waf 6: 1) liliharibiwa na Nebukadnezza mfalme wa Babuloni mwaka 587 K.B. (2 Mambo ya Nyakati 36). Lilijengwa tena na Zerubabeli baada ya utumwa wa Babeli, lilichafuliwa na Antikus Epifanes mfalme wa Seleucide mwaka 167 K.B. Lilitakaswa tena mwaka 165 K.B na Yuda wa Makabayo na ndugu yake. Herodi ili kupata heshima kutoka kwa Wayahudi aliliboresha na kulijenga vizuri hekalu hili la pili na kujaribu kulirudisha katika hali ya utukufu wake wa mwanzo kazi iliochukua miaka 46 (Yn 2: 20). Baada ya hekalu kubomolewa kabisa mpaka misingi yake na Warumi mwaka 70 A.D, halikuwahi kujengwa tena. Katika eneo hilo kuna msikiti wa Omar. 

Yesu, katika Injili ya leo analitakasa hekalu na anajaribu kulirudisha katika lengo lake la mwanzo. Tunaisha katika nyakati zinazobadilika, kiasi kwamba kanisa siku hizi baadhi ya watu wanaweza kuwa na malengo mengine. 

1.Sehemu ya Makumbusho- watu wanakuja kuona uzuri wa kanisa na rangi zake. 

2. Dukani- watu wanakuja kupata kitu kwa Mungu/kununua kitu kutoka kwa Mungu. 

3. Sehemu ya kulipa kodi-lazima nilipe fungu la kumi nisipolipa nitaadhibiwa mimi na familia yangu. 

4. Sehemu ya Maonesho- sehemu ambayo watu wanakuja kujionesha, aina ya nguo, pete yake mpya, mikufu, gari jipya, nguo mpya, na aina ya maisha ninayo ishi. 

5. Sehemu ya kuabudu-sehemu ambayo watu wanaweza kuhizi uwepo wa Mungu katika hali ya nguvu kubwa tofauti na sehemu nyingine. 

Mungu ameamua kujidhihirisha katika hekalu, si kwa sababu hana sehemu nyingine-kwani yeye ni Mkuu wa ulimwengu mzima. Ni sehemu iliowekwa wakfu ili kutusaidia kujenga tena upya uhusiano wetu naye. Mzaburi anatuambia siku moja hekaluni mwa Bwana ni bora kuliko siku elfu mahali pengine (Zab. 84:10). Je, wewe unaenda kanisani kwa lengo ghani? Kuanzia namba moja hadi tano hapo juu wewe upo wapi? Tujipime na kama tunakosea turudi katika lengo halisi la Hekalu. 

Sala: Bwana Yesu, nitakase mimi na uniweke tena katika hali ya neema na uaminifu. Amina.


Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment