Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, OKTOBA 9, JUMAPILI, 2022














MASOMO YA MISA, OKTOBA 9, JUMAPILI, 2022
DOMINIKA YA 28 YA MWAKA  C WA KANISA

SOMO LA 1
2 Fal 5:14-17

Naamani alishuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi. Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako. Lakini akasema, Kama Bwana aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa. Naamani akasema; Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa Bwana.

Neno la Bwana………..Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab 98:1-4

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake wenyewe,
Mkono wake mtakatifu umetenda wokovu

(K) Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa

Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake

(K) Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa

Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu,
Mshangilieni Bwana, nchi yote. Inueni sauti, imbeni kwa furaha

(K) Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa


SOMO LA 2
2 Tim 2:8-13

Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.

Neno la Bwana……………….Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO
Yn 10:27

Aleluya, aleluya
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, asema Bwana: Nami nawajua nao wanifuata.
Aleluya

INJILI
Lk 17:11-19

Yesu alipokwenda njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya. Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika. Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.

Neno la Bwana………………Sifa kwako Ee Kristo

Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.          

1 comment: