Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUMATATU, SEPTEMBA 15, 2025




MASOMO YA MISA, JUMATATU, SEPTEMBA 15, 2025
JUMA LA 24 LA MWAKA


KUMBUKUMBU YA BIKIRA MARIA MTAKATIFU WA MATESO

SOMO 1
Ebr. 5:7 – 9

Kristo, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa wa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mates ohayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
________

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 31:1 – 5, 14 – 15, 19 (K) 16

(K) Uniokoe, Ee Bwana, kwa ajili ya fadhili yako.

Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
Nisiaibike mbele kwa haki yako uniponye.
Unitegee sikio lako, uniokoe hima. (K)

Uwe kwangu mwamba wa nguvu,
Nyumba yenye maboma ya kuniokoa,
Ndiwe genge langu na ngome yangu,
Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge. (K)

Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,
Maana wewe ndiwe ngome yangu.
Mikononi mwako naiweka roho yangu,
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)

Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)
Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako
Ulizowawekea wakuchao;
Ulizowatendea wakukimbiliao
Mbele ya wanadamu! (K)
________

SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Bikira Maria anafurahi yeye ameshinda na kupata nishani ya ushahidi pasipo kufa, alipokuwa chini ya msalaba wa Bwana.
Aleluya.
________

INJILI
Yn. 19:25 – 27

Penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani mwake.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Au

INJILI
Lk. 2:33 – 35

Babaye na mamaye wa Yesu walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga ukaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
________

Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

15th SEPTEMBER 2025


 

14th SEPTEMBER 2025


 

MSALABA WA KRISTO NI TUMAINI NA UKOMBOZI WETU!




“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Jumapili, Septemba 14, 2025 
Juma la 24 la Mwaka

Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu

Hes 21: 4-9 
Zab 77: 1-2, 34-38
Fil 2: 6-11
Yn 3: 13-17


MSALABA WA KRISTO NI TUMAINI NA UKOMBOZI WETU!

Msalaba ni ishara ya Mkristo. Kila Mkristo, mtoto na hata mtakatifu mkubwa kabisa, wanafanya ishara ya Msalaba, kutoa ushuhuda wa nguvu yake na umuhimu wake. Yesu alitoa maisha yake Msalabani na hapo akakomboa ubinadamu. Kwa njia hii hamna tena alama ya mateso na aibu, bali ukombozi. Msalaba ni njia ya kwenda kwenye utukufu, kwahiyo ni changamoto kwa kila Mkristo. Kama Mtakatfiu Paulo anavyosema “Tunamuhubiri Yesu Msulubiwa, kwa Wayahudi ni kikwazo na kwayunani ni upuuzi, bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani ni Kristo, Nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu” (1 Kor 1: 23-24). 

Katika historia ya Ukristo Msalaba aliofia Kristo na kwa njia hii akafufuka, umekuwa niishara wazi ya nguvu ya Mungu ya kuokoa. Mababa wa Kanisa wanalinganisha Msalaba wa Yesu na mti wa uzima katika bustani ya dunia, safina ya Noah, na kuni alizobeba Isaka katika mlima Moriah, na ile ngazi ya Yakobo, na ile Fimbo ya Musa, na yule nyoka ya Shaba. Haya yote katika hali ya juu yanahusishwa na fumbo la ukombozi. Katika Ubatizo kila Mkristo amesulubiwa na Kristo, kufa na kufufuka na Kristo. Mtakatifu Leo Mkuu anasema, “Msalaba ni chanzo cha kila Baraka, chanzo cha mafanikio yote: kwa waamini unawapa nguvu kutoka katika udhaifu wake, utukufu kutoka katika aibu yake, na uzima kutoka katika kifo”.  

Sala: Ee Msalaba juu ya Ulimwengu, kuwa uponyanji na Ukombozi wangu. Amina

Copyright ©2013-2025 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

MASOMO YA MISA JUMAPILI, SEPTEMBA 14, 2025



MASOMO YA MISA 

JUMAPILI, SEPTEMBA 14, 2025
JUMA LA 24 LA MWAKA


SIKUKUU YA KUTUKUKA KWA MSALABA MTAKATIFU


SOMO 1
Hes. 21:4 – 9

Siku zile jangwani, watu walimnung’unikia Mungu, na Musa, mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, tumefanya dambi kwa sababu tumemnung’unukia Mungu, na wewe, utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi, Musa akawaombea watu. Bwana akawaambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo, ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 78:1 – 2, 34 – 38 (K) 7

(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.

Enyi watu wangu, sikilizeni sheria yangu,
Tegeni masikio kwa maneno ya kinywa changu.
Na nifunue kinywa changu kwa mithali,
Niyatamke mafumbo ya kale. (K)

Alipowaua ndipo walipokuwa wakimtafuta;
Wakarudi wakamtaka Mungu kwa bidii.
Wakakumbuka kuwa Mungu ni mwamba wao,
Na Mungu Aliye juu ni mkombozi wako. (K)

Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, 
Wakamwambia uongo kwa ndimi zao.
Kwa maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake,
Wala hawakuwa waaminifu katika agano lake. (K)

Lakini Yeye, kwa kuwa anayo rehema,
Husamehe uovu wala haangamizi.
Mara nyingi huipishia mbali ghadhabu yake,
Wala haiwashi hasira yake yote. (K)


SOMO 2
Fil. 2:6 – 11

Yesu Kristo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama wanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mung alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina, ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Ee Kristu tunakuabudu na kukutukuza, 
kwa kuwa umeikomboa dunia kwa msalaba wako.
Aleluya.


INJILI
Yn. 3:13 – 17

Yesu alimwambia Nikodemo: Hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

MATUNDA MAZURI NA MSINGI MZURI!



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumamosi, Septemba 13,  2025
Juma la 23 la Mwaka wa Kanisa

1 Kor 10: 14-22
Zab 115: 12-13, 17-18
Lk 6: 43-49


MATUNDA MAZURI NA MSINGI MZURI!


Yesu mara nyingi alitoa mfano kutoka katika mazingira ya asili na kuelezea thamani za Ufalme wa Mungu. Katika Injili ya leo tuna mifano ya tini na zabibu. Mtini ilikuwa ni alama ya rutuba, mafanikio na Amani. Zabibu zinatoa divai, alama ya furaha. Yesu anatumia mifano hii na anawaeleza wafuasi wake kwamba mti unajulikana kwa matunda yake. Ni katika hali hiyo hiyo pia mtu anatoa matunda mazuri au mabaya kulingana na mbegu iliyosiwa moyoni mwake. Na zaidi sana inategemea sana tabia ya mtu katika kuzaa matunda mema au mabaya. Wanaoishi na Roho wa Mungu wanazalisha matunda mema kama, furaha, Amani, uvumilivu, kujali, huruma, uaminifu, upole na kuweza kujizuia na kujiongoza (rej. Wagalatia 5: 22- 23). Wale waliyo waaminifu kwa Munguwanajua nguvu zao zipo mikononi mwa Mungu na sio kwao binafsi bali zipo kwa Mungu anayewapa neema tele za kuishi kama wafuasi wake wa kweli. Je nimatunda ghani unayozalisha ili kudhihirisha ulipozamisha mizizi yako? Kwa Mungu au mwili/Dunia?.

Pengine tujaribu kujiuliza matendo yangu yanatoa ishara yeyote ya uwepo wa Kristo ndani yangu? Je matendo yangu yanaendana na Imani yangu? Au tunaishi tu na watu wanashindwa kufahamu sisi ni nani? Hatuwezi kujiita wafuasi wa Kristo wakati hatutendi kama Kristo au kama tunatenda tofauti na mapenzi ya Kristo. Matendo yetu na Imani yetu yaendane ili tuweze kuwa zabibu zinazo zaa zabibu na sio zabibu zinazo zaa mchongoma. Tuimarishe hazina njema ya mioyo yetu wenyewe ili iweze kutoa matunda mema kwa njia hii tutakuwa tumejenga msingi wetu katika Kristo na hivyo tutakuwa imara daima dhoruba ijapo tukitambua kwamba hata dhoruba iweje wa mwisho kutenda dhambi ni mimi mwenyewe, hakuna mtu anayemsaidia mtu kutenda dhambi, kwani dhambi huanzia ndani ya moyo wa mtu. Hata vingekuwepo vishawishi vya aina ghani, inabaki kwamba wa mwisho kutenda dhambi ni mtu mwenyewe. Tujenge mzingi mzuri ndani ya Yesu ili tuweze kungara kwa matunda mema.


Sala: Yesu nisaidiye niweze kuzaa matunda mema ya Imani, matumaini na upendo. Amina

Copyright ©2013-2025 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

MASOMO YA MISA, SEPTEMBA 13, 2025






MASOMO YA MISA, JUMAMOSI, SEPTEMBA 13, 2025
JUMA LA 23 LA MWAKA


SOMO 1
1Tim. 1:15-17

Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika katika mimi. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristu audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele. Sasa kwa Mfalme wa milele, asiyeweza kuona uharibifu, asiyeonekana, Mungu peke yake, na iwe heshima na utukufu, Mungu peke yake, na iwe heshima na utufufu milele na milele.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
________

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 113:1-7 (K) 2

(K) Jina la Bwana lihimidiwe tangu leo na hata milele.

Aleluya.
Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
Lisifuni jina la Bwana,
Jina la Bwana lihimidiwe
Tangu leo na hata milele. (K)

Toka maawio ya jua hata machweo yake
Jina la Bwana husifiwa.
Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote,
Na utukufu wake ni juu ya mbingu. (K)

Ni nani aliye mfano wa Bwana,
Mungu wetu aketiye juu;
Anyenyekeaye kutazama,
Mbinguni na duniani?
Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Na kumpandisha maskini kutoka jaani. (K)
________

SHANGILIO
Lk. 8:15

Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya.
________
INJILI
Lk. 6:43 – 49

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.
Na kwa nini mnaniita, Bwana, walakini hamtendi nisemayo?

Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake. Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri. Lakini yule aliyesikia ila hakutenda, mfano wake ni mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mto ukaishukia kwa nguvu, ikaanguka mara; na maangamizi yake nyumba yakawa makubwa.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
________

Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

13th SEPTEMBER 2025




 


12th SEPTEMBER 2025


 

MASOMO YA MISA, IJUMAA , SEPTEMBA 12, 2025





MASOMO YA MISA,
IJUMAA, SEPTEMBA 12, 2025
JUMA LA 23 LA MWAKA



SOMO 1
1 Tim 1:1-2, 12-14

Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu, taraja letu; kwa Timotheo, mwanangu hasa katika imani. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake;ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani. Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

________

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 16:1-2, 5, 7-8, 11

(K) Bwana ndiye fungu la posho langu.

Mungu, unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu;
Sina wema ila utokao kwako.
Bwana ndiye fungu la posho langu,
Na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu. (K) 

Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. (K) 

Utanijulisha njia ya uzima;
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele. (K)
_______

SHANGILIO
Zab. 111:7, 8

Aleluya, aleluya,
Maagizo yako yote, Ee Bwana, ni amini, yamethibitika milele na milele.
Aleluya.
________

INJILI
Lk. 6:39-42

Yesu aliwaambia wanafunzi wake mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili? Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
________

Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com