MASOMO YA MISA, JANUARI 30, 2026
IJUMAA YA 3 MWAKA
SOMO 1
2 Sam. 11:1-10, 13-17
Ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakauhusuru Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu.
Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kasha akarudi nyumbani kwake. Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, Ni mjamzito.
Ndipo Daudi akapeleka kwa Yoabu, akisema, Unipelekee Uria, Mhiti. Naye Yoabu akampeleka Uria kwa Daudi. Uria alipomwendea DAudi, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, na habari za watu, na habari za vita. Daudi akamwambia Uria, Hay, shuka nyumbani mwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme. Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake.
Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake. Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hata wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake.
Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria. Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kasha ondokeni, mmwache, ili apigwe, akafe. Ikawa Yoabu alipokuwa akiuhusuru mji, akamweka Uria mahali alipojua ya kuwa pana mashujaa. Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 51: 1-5, 8-9 (K) 1
(K) Uturehemu, Ee Mungu, kwani tumekosa.
Ee Mungu, unirehemu, sawasawa na fadhili zako;
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu. (K)
Maana nimejua mimi makosa yangu,
Na dhambi yangu I mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,
Na kufanya maovu mbele za macho yako.
Wewe ujulikane kuwa una haki unenapo
Na kuwa safi utoapo hukumu.
Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu,
Mama yangu alinichukua mimba hatiyani. (K)
Unifanye kusikia furaha na shangwe,
Mifupa uliyoipondwa ifurahi.
Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu,
Uzifute hatiya zangu zote. (K)
SHANGILIO
Mt. 11:25
Aleluya, aleluya,
Utukuzwe, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewafunulia watoto wachanga mafumbo ya ufalme wa mbingu.
Aleluya.
INJILI
Mk. 4:26-34
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara aupeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika.
Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake.
Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment