Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

Sasa Mimi ni Nani?

 


“KUFUFUKA NA KRISTO”
Tafakari ya Pasaka
Jumapili, Mei 4, 2025, 
Juma la 3 la Pasaka


Mdo. 5:27-32, 40-41
Zab. 30. 1, 3, 5, 10 -12 (K) 1
Ufu. 5:11-14
Yn. 21:1 - 19.



Masomo ya somo la kwanza katika kipindi hiki Paska yanatoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume. Ni vyema kuelewa kuwa kazi za mitume zinaongozwa na Roho Mtakatifu baada ya Pentekoste. Lakini Injili bado inatuletea matukio ya Yesu kujihakikisha kwa wanafunzi wake. Yafaa tukumbuke kuwa, bado katika Injili wanafunzi hawajapokea Roho Mtakatifu. Yaani yaani Injili inatangulia somo la kwanza ndiyo maana katika somo la kwanza wanafunzi ni jasiri, wanafanya maajabu lakini katika Injili tunawaona bado ni waoga wanaosuasua katika imani na wito wao kwa sababu matukio haya ni ya kabla ya Pentekoste.

Injili ya leo ni refu. Ina matukio makuu matatu na kila tukio lafaa liwe na mahubiri yake tofauti ama hata semina yake. Tukio la kwanza ni lile la Petro kurudi kwenda kufua samaki na wanafunzi wengine wanamfuata. La pili ni idadi na karamu ya mkate na samaki kama kifungua kinywa na tukio la tatu ni lile la Yesu kumuuliza mara tatu Petro kama kweli anampenda. Wakati tukio la tatu, Yesu anamhoji Petro, kama anampenda. Petro anashindwa kufikia kiwango cha upendo ambacho Yesu anatarajia. Kwa Kigiriki upendo una maana maarufu tatu, philia, agape, and eros zote zilitumika wakati tofauti kwani zilikuwa na maana tofauti na ukweli bado upendo hata kwa kiswahili una maana tofauti ila tunatumia neno moja tu. Baba anavyompenda mkewe (eros) siyo sawa na anavyompenda marafiki zake (philia) na nitofauti na anavyompenda watoto wake (agape). Yesu anamuuliza Petro, unanipenda upendo wa usio na masharti (agape) huu ni upendo ambao mtu anaweza kujitolea bila kutegemea kitu kutoka kwa mtu unayempenda kama mzazi anavyompenda mtoto ama Mungu anavyotupenda. Lakini Petro anajibu ninakupenda kama rafiki (philia), kwa sababu tayari hakuweza kusima pamoja naye bali alimkana alipokuwa na shida, upendo wa kirafiki ndivyo ulivyo. Kukiaribika unakimbia na ndiyo maana Petro anasisitiza urafiki wake siyo wa agape kama alivyo ahidi hapo mbele, ‘nitatoa nafsi yangu kwa ajili yako (agape) (Yn. 13:37). Bali kutokatana na yaliyotokea Petro amekubali kuwa upendo wake kwa Yesu ni wa kirafiki tu (philia). Yesu anamuuliza tena kama ana upendo kwake usio na masharti, (agape), Petro anarudia tena kuwa upendo wake ni wa kirafiki (philia), na Yesu kwa mara ya tatu anauliza, unanipenda kama rafiki (philia) Petro anajibu, ninakupenda kama rafiki (philia). Yaani Yesu ameshuka chini. Hivyo tayari unaanza kujua ni kitu gani kinaendelea, pamoja na upendo huo wa kirafiki Yesu anamuachia mamlaka ya kuliongoza kanisa lake. Tunaweza kujifunza jambo moja muhimu, bila Roho Mtakatifu haitakuwa rahisi kumpenda Yesu kwa upendo wa (philia), upendo usio wa kujitoa kwa ajili ya yule umpendaye bila kutegemea chochote kutoka kwake.

Tukio la pili likikuwa, Yesu kuwakaribisha wanafunzi wake katika kifungua kivywa. Tukio hili litawakumbushia wanafunzi wake siku aliyoongeza mikate mitano na samaki wawili na kuwashibisha maelfu ya watu. 


Ninaenda Kuvua Samaki

Simoni Petro aliwaambia, naenda kufua samaki. Ninaenda kufua samaki ulikuwa uamuzi wa mwisho baada ya kila kitu kwenda vibaya. Petro alipoitwa na Yesu alikuwa anavua samaki. Uvuvi ndiyo iliyokuwa kazi yake kama zilivyo kazi za udereva, ujenzi ama ualimu. Ndiyo kazi aliifanya kumpatia kipato cha kuishi kabla ya kuiacha na kuamua kuwa mwanafunzi wa Yesu. Tunapoziacha kazi zetu za awali kwa hiari yetu kama alivyofanya Petro ni kuwa tuna matumaini makubwa kwa kazi ama shughuli mpya tunayojiingiza. Watu wameacha kazi za kuajiriwa na kuanza kufanya biashara kwa kuwa wanaona biashara ina manufaa zaidi katika maisha yao. Hivyo ndiyo ilivyokuwa kwa Petro. Lakini kutokana na yake yaliyotokea Ijumaa Kuu, kila kitu kilianguka, asingeweza tena kuendelea kuwa mwanafunzi wa Yesu kwa sababu Yesu ameakamatwa na kuuawa.

Tatizo analokumbana nalo Petro siyo tu kifo cha Yesu na yeye mwenyewe kushindwa kusimama kidete kama mwanafunzi shujaa na kumtetea Yesu hata kama ingemgharimu kifo la, tatizo ni kuwa, Yesu alikufa na ndoto zake zote katika maisha. Hawa ni watu waliomfuata Yesu wakiwa na Malengo tena malengo makubwa. Lakini malengo na ndoto hizo zote ziliuliwa na kifo cha Yesu. Kifo cha Yesu kiliwaondolea utambulisho wao. Walikuwa wamezoea kujitambulisha kuwa wao ni wanafunzi wa Yesu sasa watajitambulisha kama wao ni nani. “Utambulisho wao ulikufa na Yesu.”

Sasa Mimi ni Nani?

Sasa mimi ni nani ni swali linaloulizwa na watu wengi waliokumbwa na majanga makubwa yanayotishia utambulisho wao. Mwalimu anapofukuzwa kazi anapata utata wa utambulisho. Akikutana na mtu anakuwa na wasiwasi, nimwamibie mimi ni nani? Nilikuwa mwalimu sasa mimi ni nani? Ama mke aliyefiwa na mume wake mpendwa anakuwa na tatizo hilo hilo. Kama alijizoesha kujitambulisha kwa kutumia jina la mume wake, bi..., itamchukua muda kutafuta utambulisho mpya. Wanafunzi wa Yesu wanakumbwa na utata wa utambulisho, “watajiita wafuasi wa nabii mfu?” hasha utakuwa utambulisho unaowakumbushia mambo mabaya yaliyoyatokokea, kama isivyokuwa kawaida kumkuta mkwe alivyefiwa na mume akijitambulisha, mimi ni mjane wa fulani mtu aliyekuwa maarufu ambaye kwa sasa hayupo tena. Tena siyo kama amekufa kwa bahati mbaya bali katika hali ya aibu kabisa, kifo msalabani.

Wakati wanahoji utambulisho wao bado wanajihoji wenyewe, kweli yule Yesu alikuwa Masiha kweli ama alitudanganya? Ni katika hali hii ambayo Petro anaamua kurudia kazi yake ya zamani. Anaamua kurudi kuvua samaki kwani anakumbuka hata kabla ya kukutana na Yesu alikuwa mvuvi nitarudi. Anarudi na hata samaki wanamkimbia, usiku kucha hapati chochote nao utambulisho wa zamani umepotea, ni mvuvi gani bila samaki.

Utambulisho wa Petro umejikita katika uhusiano wake na Kristo. Anapopewe Roho Mtakatifu anaweza kutoka nje tena na kuhubiri bila woga na kuikabili hali ilivyokuwa inamfanya aogope kabla. Watu wengi wamejaribu kutafuta utambulisho sehemu mbali mbali wanapopatwa na utata wa utambulisho. Sehemu hizo zote kama hazija angaziwa na nuru ya Kristo mfufuka haziwezi kutupatia utambulisho wa kweli. Unapoiacha familia, ama kikundi cha dini kwa sababu kuna matatizo bila kujitolea kabisa katika upendo ambao Yesu mfufuka anataka Petro amshuhudie nao, (agape) hauta pata utambulisho wa kweli. Utapoteza muda mwingi na nguvu nyingi kama walivyofanya wanafunzi wa Yesu bila mafanikio. Utambulisho wetu wakristo unatokana na kulisikia neno la Kristo Mfufuka. Maamuzi yetu yaelimishwe na Neno la Kristo lililojaa na zawadi ya Roho Mtakatifu inayoimarishwa na ushiriki wetu wa Sakramenti Takatifu za Kanisa.


Copyright ©2013-2025 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment