MASOMO YA MISA, MEI 4, 2025
JUMAPILI YA 3 YA PASAKA MWAKA C
SOMO 1
Mdo. 5:27-32, 40-41
Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je!
Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni,
mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu
yetu. Petro na mitume wakajibu, wakasema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko
wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika
katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na
Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa
mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio.
Nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru
wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. Nao wakatoka katika
ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa
ajili ya Jina hilo.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 30:1, 3, 5, 10-12 (K) 1
(K) Ee Bwana, Mungu wangu, Nalikulilia
ukaniponya.
Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,
Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
Umeniinua nafsi yangu,
Ee Bwana, kutoka kuzimu.
Umenihuisha na kunitoa
Miongoni mwao washukao shimoni. (K)
Mwimbieni Bwana zaburi,
Enyi watauwa wake.
Na kufanya shukrani.
Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,
Katiak radhi yake mna uhai.
Huenda kilio huja kukaa usiku,
Lakini asubuhi huwa furaha. (K)
Ee Bwana, usikie, unirehemu,
Bwana, uwe msaidizi wangu.
Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;
Ulinivua gunia, ukanivika furaha.
Ee Bwana, Mungu wangu,
Nitakushukuru milele. (K)
SOMO 2
Ufu. 5:11-14
Mimi, Yohane, nikaona nikasikia sauti ya malaika
wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na wale wenye uhai, na za wale wazee,
na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu, wakisema, kwa
sauti, Astahili Mwana-kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima
na nguvu na heshima na utukufu na Baraka.
Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi
na chini ya nchi ya juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake,
nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye
juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-kondoo, hata milele na milele. Na wale
wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka, wakasujudu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Lk. 24:32
Aleluya, aleluya, Bwana Yesu, utufunulie maandiko; uwashe mioyo
yetu unaposema nasi. Aleluya.
INJILI
Yn. 21:1-19
Baada ya hayo Yesu alijidhihirisha tena kwa
wanafunzi wake, penye bahari ya Tiberia, naye alijidhihirisha hivi. Simoni
Petro, na Tomaso aitwaye Pacha, na Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, na wana wa
Zebedayo, na wengine wawili wa wanafunzi wake, walikuwapo pamoja. Simoni Petro
aliwaambia, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe.
Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu.
Hata asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama ufuoni;
walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu. Basi Yesu akawaambia, Wanangu,
mna kitoweo? Wakamjibu, La. Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa
chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa
sababu ya wingi wa samaki. Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda
akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni
Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi,) akajitupa baharini. Nao hao
wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila
yapata dhiraa mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki.
Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa
makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate. Yesu akawaambia, Leteni hapa
baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi. Basi Simoni Petro akapanda chomboni,
aklivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na
ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka. Yesu akawaambia, Njoni
mfungue kinywa. Wala hakuna mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuliza, U
nani wewe? Wakijua ya kuwa ni Bwana. Yesu akaenda akautwaa mkate, akawapa, na
samaki vivyo hivyo. Hiyo ndiyo mara ya tatu ya Yesu kuonekana na wanafunzi wake
baada ya kufufuka katika wafu.
Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni
Petro, Je! Simoni wa Yohane, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam,
Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wanakondoo wangu.
Akamwambia tena mara ya pili Simoni wa Yohane wanipenda? Akamwambia, Ndiyo,
Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia
mara ya tatu, Simoni wa Yohane, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile
alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe
umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.
Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa
kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee,
utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka. Akasema
neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha
kusema hayo, akamwambia, Nifuate.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo
Copyright ©
2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment