Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, DESEMBA 16, 2022

MASOMO YA MISA, DESEMBA 16, 2022

JUMA LA 3 LA MAJILIO


SOMO 1
Isa 56:1–3, 6–8
Bwana saema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote. Wala mgeni, aambatanaye na Bwana, asiseme hivi, Hakika yake Bwana atanitenga na watu wake. Na wageni walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote. Bwana Mungu, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, Pamoja na hayo nitamkusanyia na wengine, zaidi ya hao walio wake waliokusanywa.


WIMBO WA KATIKATI
Zab 67:1–2, 4, 6–7

(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, watu wote na wakushukuru.


Mungu na atufadhili na kutubariki,
Na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulike duniani,
Wokovu wake katikati ya mataifa yote.
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, watu wote na wakushukuru.

Mataifa na washangilie,
Naam, waimbe kwa furaha,
Maana kwa haki utawahukumu watu,
Na kuwaongoza mataifa walioko duniani.
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, watu wote na wakushukuru.

Nchi imetoa mazao yake;
Mungu Mungu wetu, ametubariki.
Mungu atatubariki sisi;
Miisho yote ya dunia itamcha Yeye.
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, watu wote na wakushukuru.



SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Uje, Bwana, kututembelea katika Amani, ili tufurahi kwa moyo wote mbele yako.
Aleluya.



INJILI
Yn 5:33–36
Siku ile Yesu aliwaambia Mayahudi, Ninyi mlituma watu kwa Yohane, naye akaishuhudia kweli. Lakini mimi siupokei ushuhuda kwa wanadamu; walakini ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka. Yeye alikuwa taa iwakayo na kung’aa, nayi mlipenda kuishangilia nuru yake kwa muda. Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohane; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2022 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment