Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUCHAGUA FUNGU LILILO JEMA


 “ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Kila siku
Jumapili, 17 Julai, 2022
Juma la 16 la Mwaka

 

Mwa. 18 : l-10
Zab 15: 2-5
Kol 1: 24-28
Lk 10: 38-42 


KUCHAGUA FUNGU LILILO JEMA


Utangulizi

Ndugu zangu wapendwa, dominika ya leo ni ya 16 ya mwaka, tunakaribishwa kutafakari juu ya umuhimu wa kusikiliza sauti ya Bwana kabla ya kufanya mambo mengine yatukabiliyo. Jambo la kuchagua kile kilicho chema ni jambo muhimu sana ktk maisha yetu ya kiroho, tunahitaji neema na Baraka za mwenyezi Mungu kabla ya kuamua na kutenda jambo lolote.

Hotuba

Ndugu zangu wapendwa,  kuna utani mdogo juu ya masista, ninaamini hakuna masista waliopo hapa pamoja nasi. Siku moja masista watatu watawa walikuwa wanasafisha Kanisa dogo, mada ya maongezi yao ilikuwa ni namna gani ya kumtumikia Mungu. Sista wa kwanza alisema: “Ninataka kuwa kama mishumaa hii ili wakati wote niweze muda wote kumsindikiza Yesu na mwanga wangu.” Wa pili alisema, “Natamani kuwa kama maua haya ili niweza kutoa uzuri wangu na harufu yangu nzuri kwa Bwana.” Wa tatu alisema, “Ninataka kuwa kitambaa cheupe ambacho kinachofunika altare.” Wale wengine wawili walishangazwa. “Na kitambaa kitafanya nini ktk kumtumikia Bwana?” Macho yake yakiwa yameng’aa, sista alisema, “Ili Baba aweze kunibusu mimi kila siku kabla na baada ya Misa.”

Ndugu zangu wapendwa, kama hawa masista watawa, Martha na Mariamu walikuwa na mawazo yao juu ya kumtumikia Bwana. Martha alikwendaa moja kwa moja jikoni na aliharakisha kuandaa chakula kwa ajili ya mgeni wake maalumu. Alikuwa na shauku na wasiwasi kwasababu alikuwa anafanya kila kitu yeye mwenyewe na alikuwa nje ya muda. Kwa upande mwingine, Mariamu hakujihusisha juu ya kazi za jikoni. Alikaa chini miguuni mwa Yesu na alisikiliza kila neno lake. 

Martha anawakilisha utume wenye shughuli, wakati Mariamu utume wa tafakari. Je, lipi kati ya haya mawili lilipendwa na Yesu? Wakati Martha alipoanza kulalamika yakuwa dada yake alikuwa hamsaidii, kwa utaratibu Yesu alimfariji: “Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amechagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”

Je, hii inamaanisha kuwa Yesu alichukulia maisha ya tafakari kuwa ni ya muhimu sana zaidi ya maisha ya shughuli? Kwa hakika, hapana, yote ni muhimu katika maisha ya kila Mkristo. Ingawa Yesu aliweka uhakika kuwa tunaweka sawa tuyapendayo: kitu cha kwanza ni kwanza. Alipoulizwa juu ya amri kuu ni ipi, Yesu aliweka bayana kuwa: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, na kwa akili yako yote na kwa nguvu zako zote. Hii ndiyo ya kwanza. Ya pili ndiyo hii: Mpende jirani yako kama nafsi yako” Mungu kwanza; majirani wanafuata.

Mariamu alichagua sehemu iliyo bora, sio kwamba Martha alichagua iliyo mbaya. Badala yake, Mariamu alikuwa na nafasi ya haki. Alikaa chini na kusikiliza maneno ya Bwana. Kabla ya kufanya chochote kile, alihakikisha kuwa alikuwa na maelekezo na mwanga wa Bwana. Kwa upande mwingine, Martha “alisumbuka na kufadhaika juu ya mambo mengi” kwa sababu alikimbilia katika kazi zake bila ya kuomba busara na nguvu kutoka kwa Bwana.
 
Hivyo, haikuwa ni swala la lipi ni muhimu zaidi kati ya mawili. Kazi na sala vyoni ni muhimu. Ni zaidi ya swala la lipi kati ya haya mawili lianze kwanza. Injili inatueleza kuwa ni sala ndiyo inayotakiwa ianze kwanza ili kazi zetu ziwe na ulinzi na ubunifu kutoka kwa Mungu. Msemo unasema, “Wakati mtu anapofanya kazi, ni mtu pekee anayefanya kazi. Lakini wakati mtu anaposali, Mungu anafanya kazi.” Hii inatukumbusha juu ya kifungu cha maandiko, “Bwana asipoijenga nyumba waijengao wafnya kazi bure. Bwana asipoulinda mji yeye aulindaye akesha bure.”(Zaburi 127 (126): 1). Yesu alisema, “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Mbali yangu hamuwezi kufanya kitu.” Hakika Mungu ndiye anayeweka vitu viwezekane, ndiye anayefanya kazi zetu ziwe na matunda.

Kuna habari juu ya wakata mbao. Mkata mbao wa kwanza anafanya kazi masaa nane kwa siku. Wa pili anafanya kazi tu masaa matano. Lakini wote hao wana namba ya magogo iliyo sawa wakikata kwa misumeno yao. Siri ya uzalishaji wao iliulizwa, mkata mbao wa pili alisema, “Ni kwa sababu Napata muda wa kupumzika na kuurutumisha mwili wangu, na wakati napumzika, ninaunoa msumeno wangu.”

Siku hizi, watu wanatakiwa wakumbushwe juu ya fundisho hili, walio wengi kati yetu wana ugonjwa katika Kiingereza unaitwa STD – Stress, Tension na Depression: yaani wasiwasi, mashaka na huzuni. Watu wanafanya kazi kwa nguvu sana ili tu kukidhi mahitaji yao. Wanakimbilia kuuwai mstali wa mwisho uliotolewa ofisini; wanakimbia asubuhi na mapema kuchukua usafiri ili wawahi kazini, kuwahi kwa muda muhafaka ktk ratiba au shughuli zao. Mwishoni mwa siku, walio wengi wanakuwa wamechoka, wametumika vibaya na wangali watupu. Na hii hutokea kila siku kwa miaka. Maisha yamekuwa ni ya gharama sana kuyaishi, watu hata hawafikirii kuchukua muda fulani mbali na kazi. Iliyo mbaya zaidi ya yote ni kwamba wengi wao wanasema kuwa hawana muda hata wa kwenda Kanisani au kusali. Wao wametingwa tu. Sasa Bwana anatuambia: “Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi! Kuwa na amani. Njoo kwangu, na Nitakupatia pumziko!” Tunahitaji kuja kwa Yesu kupata pumziko fulani pamoja na maboresho mengi.

Kumbuka: Yesu ndiye mti; sisi tu matawi. Tawi haliwezi kuzaa tunda kama halijaunganika na mti. Tunakuwa hatuna nguvu na wenye maisha duni kama hatujaunganika kwa Yesu. Tuna kazi nyingi sana za kufanya na majukumu mengi ya kuyatimiza. Ndio, tunapaswa kufanya kazi kwa bidii. Ila kwanza, basi tuhakikishe kwanza tunapata muda wa kukaa chini katika miguu ya Yesu na kuyasikiliza maneno yake, kuangaziwa kwa roho yake na kuhimarishwa kwa neema. Kisha kazi inakuwa nyepesi, matunda ya nguvu zetu yanakuwa matamu na mengi. Basi tuuchukuwe nyumbani moto wa Mt. Benedicto: “Ora et labora.” Pray and work, yaani “Sala na Kazi”.

Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment